Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam. |
Dar es Salaam. Serikali imetangaza ongezeko la mahujaji wanane waliopoteza maisha kwenye mkanyagano uliotokea kwenye mji mtakatifu wa Makka mwishoni mwa mwezi uliopita na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufikia 20.
Mkanyagano huo ulitokea Septemba 24 kwenye mji wa Mina wakati mahujaji hao wakiwa kwenye eneo la kufanyia alama ya kumpiga shetani kwa kumrushia mawe. Taarifa za awali zilieleza kuwa Watanzania 12 ni kati ya zaidi ya mahujaji 800 waliopoteza maisha, ingawa kulikuwa na baadhi waliokuwa hawafahamiki walipo.
Jana, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilitangaza kugundulika kwa miili ya watu wanane ambao ni miongoni mwa Watanzania waliokuwa wanatafutwa baada ya ajali hiyo. “Mahujaji wengine wanane kutoka Tanzania ambao walikuwa hawonekani tangu ajali ilipotokea wametambuliwa. Hii inafanya idadi ya waliofariki kutokana na tukio hilo kufikia 20,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imewataja waliofariki kuwa ni Hamida Llyas Ibrahimu (Khidmat Islamia), Farida Hamis Mahinda (Ahlu Daawa), Archelaus Anatory Rutaluyunga (Khidmat Islamaya) na Said Abdulhabib Ferej (Ahlu Daawa).
Wengine ni Awadh Saleh Magram (Khidmat Islamiya), Salama Rajab Mwamba (Khidmat Islamiya), Nuru Omar Karama (Ahlu Daawa) na Saida Awaadh Ali (Ahlu Daawa).
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Serikali ya Saudi Arabia inaendelea kufanya uchunguzi na itakuwa inatoa taarifa za miili itakayogundulika au majeruhi na wizara itakuwa ikitoa taarifa hizo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.