ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, September 20, 2015

MGOMBEA WA CCM JIMBO LA ULYANKULU AHIDI KWA WANANCHI WAKIMCHAGUA ATAPIGANIA KUANZISHWA HALMASHAURI NA WILAYA

Mgombea Ubunge wa Jimbo jipya la Ulyankulu Wilaya ya Mkoa wa Tabora kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Kadutu (kushoto) akitambulishwa na mgombea urais kupitia tiketi ya CCM John Pombe Magufuli (kulia)
Na PETER FABIAN, ULYANKULU.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo jipya la Ulyankulu Wilaya ya Mkoa wa Tabora kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Kadutu amewaomba wananchi kumchagua ili kuendelea kupigania ombi la kuanzishwa Halmashauri ya Ulyankulu na kuwa Wilaya kama alivyofanya hadi kupewa jimbo jipya la Ulyankulu na serikali ya Rais Dkt Jakaya Kikwete inayomaliza muda wake.


Kadutu alitoa kauli hiyo katika maeneo ya Kata za Seleli, Kona nne na Ilege wakati wa mikutano ya kampeni ya kujinadi na kuomba kuchaguliwa ili kutekeleza ahadi yake hiyo kwa kuhakikisha hoja ya kuomba kuanzishwa Halmashauri na Wilaya ya Ulyankulu inatekelezwa na serikali ya awamu ya tano kutokana na kukidhi kwake kwa lengo na kurahisisha huduma kwa wananchi.


Alisema kwamba akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua anayemaliza muda wake waliwasilisha ombi hilo mwaka 2013 kwenye ngazi ya Mkoa na Ofisi ya Waziri Mkuu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) lakini walifanikiwa kupata jimbo la Ulyankulu na endapo akichaguliwa atahakikisha hoja ya Halmashauri na Wilaya zinafanikiwa.


“Hili nitalipigania ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, Ofisi ya Waziri Mkuu na ikiwezekana kumuona Rais wa serikali ya awamu ya tano ili kuwezesha wananchi kupata huduma kwa ukaribu na mgombea Urais Dk John Magufuli alipofika kuwaomba kura nilimwomba,”alisema.


Kadutu aliongeza kwa kusema kwamba endapo Rais atakuwa Dk Magufuli aliyemwomba kukubaliana na ombi hilo la wananchi atahakikisha anamsumbua hadi ahadi hiyo inatekelezeka kwa vitendo lakini pia kutasaidia kuleta maendeleo na huduma ya haraka kwa wananchi wa jimbo la Ulyankulu katika sekta zote.


“Tulikuwa jimbo la Urambo Magharibi sasa jimbo la Ulyankulu lakini eneo yaliyokuwa Ofisi za kuhudumia Wakimbizi tutariboresha na kuwa makao makuu ya Halmashauri au Wilaya ili wananchi waanze kupata huduma badala ya kutembea umbali mrefu hadi wilayani Kaliua kupata huduma  hiyo,”alisisitiza.


Aliongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imekuwa ikiongoa kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Halmashauri na Manispaa kwa Mkoa wa tabora hivyo kwa kupitia kigezo hicho kitakuwa ni ishara njema kwa serikali kufikilia kutekeleza hoja hiyo ili kuwezesha wananchi wananufaika kwa kupata huduma za Halmashauri kwa haraka na ukaribu zaidi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.