Picha kutoka maktaba. |
Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WANAWAKE wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kusafirisha mabinti kutoka Tanzania kwenda Kenya kwa ajili ya kuwafanyisha ngono.
Washtakiwa hao Jackline Milinga (23) na Mary Amukowa (29) ambaye ni Mkenya walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka ya kuwasafirisha mabinti 10.
Wakisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema na Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori na Selestine Makoba walidaiwa kutenda makosa hayo Septemba 4 mwaka huu.
Nyantori alidai washtakiwa kwa pamoja, Septemba 4 mwaka huu maeneo ya Magomeni na Makumbusho waliwaajiri mabinti hao kumi na kuwasafirisha.
Inadaiwa waliwaajiri Najma Suleiman, Leah Mussa, Zulfa Ally, Rahma Mohammed, Salima Komba, Angelina Banzi, Leila Chorobi, Elizabeth Nalimu, Amina Abdi na Sada Hussein.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwasafirisha mabinti hao kutoka Tanzania kwenda Kenya kwa shughuli za ngono huku wakijidai kuwa waliwapeleka kufanya kazi.
Inadaiwa mabinti waliokuwa wakipelekwa Kenya ni wenye umri kuanzia miaka 18 mpaka 22.
Washtakiwa waliposomewa mashtaka hayo walikana kuhusika lakini walirudishwa rumande kwa sababu mashtaka hayo hayana dhamana.
Hakimu lema aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
CHANZO: MTANZANIA
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.