CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa kimeitaka Wizara ya Elimu na Wakurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Manispaa na Wilaya zote mkoani Mwanza, kulipa haraka malimbikizo ya walimu wanayodai ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.
Pia kimeonya baadhi ya watu wanaokipaka matope wakiwemo wanasiasa na wanaharakati kwa kutumia mgongo wa walimu wanaodai hawalipwi kwa wakati kwa sababu ya CCM, waache upotoshaji huo kwani madai hayo hayana uhusiano na Chama hicho japo kuwa kinatawala kwa kuunda serikali.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, kwa nyakati tofauti juzi wakati akizungumza na watendaji wa Halmashauri za Manispaa ya Ileme na jiji la Mwanza baada ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Halmashauri hizo mbili. “Deni la walimu limekuwa likiongezeka siku hadi siku, CCM hatujawahi kuzuia au kutumia fedha za walimu au za serikali kwa ajili ya shughuli zetu, wala hatujafanya vikao na kuiambia serikali isilipe walimu au watumishi wowote, wanaodai hivyo waache uzushi,” alisema.
Mtaturu alisema kwamba kutokana na hali hiyo serikali haina budi kufatilia kwa karibu fedha inazozitoa kwa ajili ya kulipa malimbikizo na stahiki za walimu katika maeneo mbalimbali nchini ili kusaidia walimu kutokuwa na hasira na malalamiko kwa kudhani CCM ndo inawacheleweshea kulipwa kwao.
Katibu huyo aliwashukia watendaji hao kuwa kitendo cha kuchelewesha kulipa stahiki halali za Walimu na watumishi wengine hakitaweza kuvumiliwa na CCM wakati Serikali Kuu inaleta fedha za kuwalipa, hivyo kuwataka wakurugenzi wawalipe haraka watumishi hao baada ya kuhakiki madai yao na kuacha visingizio.
“Kuna tetesi kuwa baadhi ya Halmashauri mnazitumia fedha hizo kwa matumizi mengine kwanza halafu ndiyo mkusanye na kuwalipa, CCM hatujawahi kukaa na nyie tukawambia msiwalipe kwanza walimu, walipeni haraka madai yao.” aliagiza Katibu huyo.
Aidha aliongeza kuwa, watumishi na watendaji wa serikali kuzingatia utumishi bora kwa kufuata maadili, huku pia serikali ikizingatia dhana ya utumishi bora hakutakuwa na kelele za madai ya walimu kwa kulipa kwa wakati na kuondoa ongezeko hilo la deni.
Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Walimu (CWT) nchini, Gratina Mukoba hivi karibuni alieleza kuwa hadi mwisho wa mwaka jana Serikali ilikuwa ikidaiwa na walimu zaidi ya shilingi bilioni 10 ikiwa ni malimbikizo ya nauli, uhamisho, kupandishwa madaraja na matibabu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.