HATIMAYE mwili wa
aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu Sylivester Marsh
umewasili jioni ya leo ukitarajiwa kuagwa kesho katika Uwanja wa Mirongo Jijini Mwanza, kabla ya
kwenda kuzikwa katika katika makaburi ya Igoma Jijini hapa.
BOFYA PLAY KUSIKILIZA TAARIFA
Badrudin Nsubuga ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Marehemu
Marsh, amesema kuwa shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu unatarajiwa kufanyika kesho
kuanzia majira ya saa 06:00 asubuhi hadi saa 12:00 mchana katika Uwanja wa
Shule ya Msingi Mirongo, ambapo kuanzia muda huo mwili huo utapelekwa nyumbani
kwao Igoma kabla ya kwenda kupumzishwa katika nyumba yake ya Milele katika
Makaburi ya Igoma.
Mjane wa Marehemu Marsh Bi.Asha Sylivester Marsh (wa pili kutoka kushoto) akiwa na watu wake wa karibu waliofika msibani kumpa pole. |
Mjane wa Marehemu Marsh Bi.Asha Sylivester Marsh ameelezea kupokea kwa
masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Marehemu Mars ambapo amebainisha kuwa
bado alikuwa akimhitaji zaidi Marsh kwa ajili ya malezi ya watoto ambao bado ni
wadogo na wanasoma.
Zaidi amewahusia wanamichezo nchini kufuata nyayo za Marehemu Marsh
katika utendaji wake wa kazi sanjari na kuwapenda na kuwashauri vyema watu wote
kubwa zaidi kupenda kuibua na kuendeleza vipaji kwa wanamichezo kama Marehemu
Marsh alivyokuwa akifanya.
Nae Jumaine Shengelo ambae ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa
wa Mwanza MZFA amemuelezea Marehemu Mwalimu Marsh kuwa katika enzi za uhai wake
wakati akicheza mpira, alikuwa ni kijana mtulivu na mwenye nidhamu uwanjani
ambae alikuwa na mwamko wa kimichezo hali iliyomsukuma pia kuanzisha kituo cha
michezo pamoja na Timu ya Soka ya Marsh Athletic Academy.
Aidha ameongeza kuwa jambo ambalo angependa kuliweka wazi ni kwamba
Timu ya Marsh Athletic Academy haitakufa, kwa sababu ameacha watu ambao
wataweza kuiendeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Nae Samiry Omary ambae ni Mchezaji wa timu ya Soka ya Marsh Athletic
Academy amesema kuwa wachezaji wa timu hiyo wameupokea kwa masikitiko makubwa
msiba wa Marehemu Mwalimu Marsh kwa kuwa bado walikuwa wakimhitaji na walikuwa
wameahidiana mambo mengi ya kimichezo ambapo wamewaomba wadau michezo
wajitokeze katika kuiendeleza aliyoiacha ya Marsh Athletic Academy.
Akizungumza kwa masikitiko Makubwa Hamza Yusuph Shido ambae ni Mdau wa
Michezo na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Utemini Kata ya Mirongo ulipo
Msiba wa Marehemu Mwalimu Marsh, amesema kuwa wanamichezo wamesikitishwa kwa
kitendo cha mwili wa Marehemu Mwalimu Marsh kusafirishwa kwa njia ya barabara
(Kwa gari/ Coaster) kutoka Jijini Dar es salaam ukilinganisha nafasi aliyokuwa
nayo katika Soka la Tanzania.
Amesema amesikitishwa namna Chama cha Soka Mkoani Mwanza MZFA pamoja
na Shirikisho la Soka nchini TFF walivyoshindwa kumuenzi Marehemu Mwalimu Marsh
hususani kwa namna mwili wake ulivyosafirishwa sanjari na katika michezo ya
ligi kuu ya Tanzania bara iliyochezwa jana kushindwa kuonyesha ishara ya aina
yoyote ya kumuenzi marehemu Marsh.
Mchezaji wa zamani wa Yanga Africans Edibilly Jonas Lunyamila (kushoto) akiwana rafiki yake wa dhati ambaye pia ni mchezaji wa zamani toka klabu ya Pamba na Taifa Stars Juma Amir Maftah. |
Marehemu Mwalimu Sylivester Marsh alizaliwa mwaka 1960 na alifariki
juzi jumamosi March 14 alfajiri akiwa katika Hospitali ya Taifa Mhimbili kwa
ajili ya Matibabu ya Saratani ya Koo ambapo enzi za Uhai wake aliwahi kuwa
mchezaji wa timu mbalimbali za soka hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kufundisha
Klabu kadhaa za Soka ambazo ni pamoja na Kagera Sugar pamoja na Azam FC ambapo
pia amewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Soka.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.