UMOJA wa Wamiliki wa Maduka ya Dawa Mwanza (UWAMADAMWA) wataka Baraza la Famasi kuyafungua maduka yote yaliyofungwa wakati wa zoezi la ukaguzi maalumu, kwa madai ya ukiukwaji wa ukaguzi huo jijini Mwanza.
Kikao cha pamoja baina ya wanachama wa UWAMADAMWA, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Baraza la Famasi na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa chini ya uenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, kilichoagizwa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe.
Akisoma risala kwa Mgeni rasmi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala wa Mkoa, Faizal Issa (RAS), katika kikao hicho Mwenyekiti wa UWAMADAMWA wa Jiji la Mwanza, Robert Nganga alisema kuwa wanasikitishwa na kitendo kilichofanywa Baraza la Famasi la kufunga maduka yao.
Nganga alisema kuwa pamoja na zoezi hilo kufanyika halikuhusisha wenyeviti wa mitaa yalipo maduka hayo na hata uongozi wa UWAMADAMWA jijini hapa jambo lililopelekea viongozi kwenda Wizarani kulalamikia hatua hiyo na kupata fursa ya kuonana na Naibu Waziri, Dk Kebwe na kuagiza kikao hiki kifanyike Mwanza.
“Tulifanyiwa vitendo vya viovu wakati wa ukaguzi maalumu na wafamasia ambao ni watumishi wa Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela (Baraza la Famasi) walifikia hatua ya kutudhalilisha ikiwemo kuwavua nguo baadhi ya wamiliki wa maduka kidendo hiki tunakilaani na waliohusika wachukuliwe hatua kali,”alisema.
Nganga alisema kuwa baadhi ya wafamasia wa Jiji, Manispaa ya Ilemela, Hospitali ya Mkoa ya Seko-Toure, Hospitali ya Wilaya ya Butimba na Hospitali ya Rufaa ya Bugando wanamiliki maduka ya dawa mhimu na kuwa vyanzo vya wizi wa dawa za serikali na kufunga maduka haya ni kuwapa nafasi ya wao kufanya biashara katika maduka yao wanayomiliki.
Kwa upande wake RAS, Issa alisema kuwa pamoja na tuhuma za UWAMADAMWA kwa wafamasia hao ambao ni watumishi wa serikali wataunda tume ya uchunguzi ili kuchunguza tuhuma hizo, pamoja na madai ya kukamatiwa dawa na kutozwa faini bilas kupewa risti za serikali za malipo na kuvuliwa nguo wakati wa utekelezwaji wa zoezi la ukaguzi kama zina ukweli wowote.
“Tumepokea malalamiko yenu na tutafanyia uchunguzi kujilidhisha kama tuhuma hizo zina ukweli na ikithibitika serikali ya Mkoa itachukua hatua za kimaadili kwa watumishi hawa wa umma,”alisisitiza.
RAS, Issa aliwataka wamiliki wa maduka hayo wanachama wa UWAMADAMWA pia kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za uanzishwaji na umiliki wa maduka ya dawa baridi na muhimu kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwemo majengo ya kutolea huduma na watoa huduma kuwa na sifa na vigezo vinavyotakiwa.
Naye Mwakilishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mtoroki Majaliwa, alisema kuwa katika kikao hicho kilichoagizwa na Naibu Waziri Dk Kebwe , hakikuonyesha tija na muafaka wowote kutokana na UWAMADAMWA kutoa shutuma tu na kutotoa nafasi kwa Wizara kutoa maelekezo ya serikali na badala yake wameleta madiwani na wenyeviti wa mitaa na kuwaacha kuwa wasemaji wao huku wausika wakiwashangilia na kuonyesha kikao kiligubikwa na wanasiasa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.