HALMASHAURI YA JIJI la Mwanza hatarini kushindwa kutekeleza mradi wa Tanzania Stragic Cites Projecty (TSCP) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia wa zaidi ya Sh. Bilioni 3.7 wa uboreshaji wa Dampo la taka eneo la Kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana jijini hapa.
Hatari hiyo inatokana na kuwepo mkanganyiko uliojitokeza hivi karibuni wakati Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, alipofanya ziara ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, kukagua miradi na kujitambulisha kwao katika Wilaya ya Nyamagana, ambapo akiwa Kata ya Buhongwa wananchi walitaka kujua lini watalipwa fidia ya maeneo yao wanayotakiwa kuachia Jiji.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa Mulongo aliambatana na Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula (CCM), Mkurugenzi wa Jiji hilo, Halifa Hida baadhi ya wajumbe wa Kamati za ulinzi na usalama Mkoa na Wilaya hiyo, wataalamu wa Jiji, Mameneja wa Tanesco, Tanroad, Mkurugenzi wa MWAUWASA na viongozi wa CCM Wilaya ya Nyamagana.
Baada ya kero hiyo ya fidia kuelezwa na wananchi, RC Mulongo alimtaka Afisa wa Idara ya Mipango miji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Deo Kalemenzi, kujibu hoja hiyo ambayo ilionekana kushangiliwa na wananchi waliokuwa wamefurika kumsikiliza katika viwanja vya shule ya msingi ya Buhongwa.
Kalemenzi akijibu hoja hiyo, alifafanua kuwa katika eneo hilo la dampo la Buhongwa kulifanyika utafiti wa kina na Jiji ili kutekeleza mradi wa TSCP kwa mwaka huu wa fedha wa 2015/2016, kufanya uthamini wa ardhi katika maeneo yasiyo ya makazi yanayozunguka eneo hilo la dampo Buhongwa. “Uthamini uliofanyika katika maeneo hayo ulizingatia taratibu, kanuni na sheria ya Mipango miji na ukadiriaji thamani chini ya kifungu Na 179 cha sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 sura ya 133, pia kuzingatia bei ya soko ambapo kila Hekri 1 ikilipwa kiasi cha Sh. Milioni 3 katika maeneo ambayo siyo ya makazi ikiwa ni mashamba,”alisema.
Kufatia majibu hayo ya kitaalamu zaidi, RC Mulongo aliagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kuacha kulipa fidia ndogo na kuutaka kulipa fidia ya kiwango cha Sh milioni 12 kwa Hekri 1 kwa wananchi wato ambao maeneo yao yataguswa na kupitiwa na mradi huo wa TSCP.
Hatua ambayo Jiji limedai kuwa halitaweza kutekeleza mradi huo wa TSCP kutokana na kiwango hicho kuwa kikubwa na kutofuata taratibu, kanuni na sheria ya Mipango miji iliyopo ikiwa ni pamoja na bei ya soko ukizingatia pia kuwa eneo hilo siyo la makazi bali la dampo la kuhifadhi taka kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji na Manspaa ya Ilemela.
“Tusipotekeleza mradi huu kutokana na mkanganyiko huu Halmashauri ya Jiji itakosa fedha iliyokuwa ipate zaidi ya Sh. 3,711,165,142.67/= bilioni, pia mtambo wa kuchakata taka zote zinapelekwa dampo hilo, magari ya kuzolea taka, vifaa vya kuhifadhia taka kabla ya kuchukuliwa kupelekwa dampo na vifaa vya kufanyia usafi maeneo yote ya Jiji hili,”alisema Afisa Afya wa Jiji Danifrod Kamenya.
Naye Mkurugenzi wa Jiji, Halifa Hida, alisema kuwa watamwelewesha zaidi RC Mulongo kutokana na agizo lake hilo kuwa pengine amechanganya bei ya viwanja vya makazi na maeneo yanayochukuliwa kwa ajili ya shughuli za taasisi za Afya, Elimu na Uwekezaji ili kunusuru hali iliyopo sasa kwa wananchi wa maeneo hayo ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo mkubwa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.