Bi Scholastika Mhagama akiwa katika mlango wa nyumba yake. |
---------------------
Na Oswald Ngonyani wa demashonews
- Peramiho.
Wahenga walisema ‘Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni;’ Jamii inazidi kujawa na chuki na
ukatili ndani yake, imekuwa kawaida siku hizi kusikia fulani kamuua fulani kwa
kisa kisichokuwa na maana.
Maalbino wanakatwa viungo vyao kwa visingizio vya
kupata utajiri kwa watu wasiokuwa na huruma, watoto wadogo wananyimwa haki zao
na kuwekwa ndani ya maboksi na wengine kuishi maisha yao katika uvungu za
kitanda yote haya ni mambo ya kutisha yanayotendeka katika jamii zetu.
Hali imekuwa tete amani na upendo vinazidi kuyeyuka
kama barafu, watu hawana utu tena, wamejivika ngozi za kondoo wakati mioyo yao
ni ya Simba, hakuna tena roho ya huruma kwa wanadamu wa dunia ya leo.
Choo cha bibi Scholastika Mhagama |
Wakati haya yote yanaendelea kutendeka katika jamii
zetu ni kama vile tunazidi kuugeuza ulimwengu tunaoishi kuwa ‘Uwanja wa dhambi’
ulimwengu wa kutojaliana tena, wanadamu
wamebadilika na kuwa kama wanyama na tena hata zaidi ya mnyama.
Katika hali isiyo ya kawaida Bibi mmoja ambaye ni
mlemavu wa miguu na mzee sana anayeishi peke yake katika kibanda ambacho kwake
ni kama gereza ambalo hataweza kutoka tena maisha yake yote, amejikuta akifanya
kitu kisicho cha kawaida kwa binadamu wa kawaida.
Jeneza la bibi likitolewa ndani kwake na wanachama wa Kombination Camp. |
Namzungumzia Bibi Scholastica Mhagama mwenye umri
unaokadiriwa kufikia (76), ambaye ni mlemavu wa miguu anayejongea kwa kutambaa ambaye
anaishi peke yake katika kibanda chake katika kijiji cha Lundusi mtaa wa Linga
huko Peramiho Songea mkoani Ruvuma. Ni jambo la kusikitisha sana kwa bi kizee
kama huyu kuishi peke yake akiwa hana msaada wa kueleweka kutoka kwa jamii
inayomzunguka.
Bibi huyu anayeishi kwa uchungu na majonzi amekata tamaa
kabisa ya maisha hali iliyomfanya aamue kuchonga jeneza lake mwenyewe akijiandaa
kufa siku yoyote.Bibi huyu anaishi na jeneza hilo chumbani kwake.
“Maisha yangu ni magumu sana, naishi kama mnyama,
sipendwi na ndugu zangu wala na jamii inayonizunguka. Wamenichoka sina raha
natamani hata Mungu anichukue sasa hivi ili nikapumzike, nasali kwa sala zote
natubu na kujuta kila siku lakini wala Mungu hanichukui, sijui kwanini” Anasema
Bi Scholastica Mhagama kwa uchungu.
Jeneza la Bi Scholastika Mhagama |
Akielezea historia ya maisha yake Bi Scholastika
anasema alizaliwa akiwa na miguu yote lakini alipata bahati mbaya ya kugongwa
na nyoka alipokuwa darasa la pili hali iliyomfanya kukatwa mguu ili kuepusha
madhara mengine kama vile kifo. Hivyo maisha yake yalibadilika na tangu hapo
akawa mlemavu.
Hali hiyo ya
ulemavu lakini pia uzee alionao vimemfanya ashindwe kujihudumia kwa lolote
zaidi ya kupika tu. Hata hivyo anakosa mahitaji muhimu kama vile maji na chakula
hali inayomfanya alale na njaa kwa baadhi ya siku.
Kwa hali aliyo nayo ni wazi kuwa Bi Scholastika
anahitaji baiskeli ya miguu mitatu (wheel chair) ambaye itamwezesha kutembea
kwa kuwa hivi sasa anatambaa na kupata maumivu makali kutokana na nyama
iliyobakia kwenye nyonga baada ya kukatwa mguu.
Bi Scholastika anazidi kueleza kuwa kuna watu waliwahi
kufika kumuandikisha jina lake na kumuingiza katika orodha ya watu wanaostahili
kupata msaada lakini anasikia misaada inafika kwa jina lake lakini yeye
mwenyewe hajawahi kuipata.
Vipi kuhusu Sera ya Wazee?
Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003
inaweka bayana kuwa suala la uzee na kuzeeka limekuwa lenye umuhimu mkubwa
ambapo karne ya ishirini imeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wazee.
Kwa kurejelea takwimu zilizopo ni kwamba, ifikapo
mwaka 2050 idadi ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 nchini hapa
itaongezeka na kufikia wazee milioni 8.3 (Sawa na asilimia 10 ya watanzania
wote)
Kama hiyo haitoshi, Taarifa ya Umoja wa Mataifa ya
mwaka 1999 inaeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wazee duniani
na kwamba ongezeko hilo linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea (Tanzania
ikiwepo) ambapo viwango vya ongezeko hilo havilingani na uwezo wa rasilimali
zilizopo za kuwahudumia.
Rasilimali hizo zinajikita zaidi katika Nyanja za
msingi katika makuzi ya binadamu yoyote zikiwemo Nyanja za afya, lishe na
huduma nyingine za msingi zisizoweza kuepukwa na binadamu yeyote.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.