Hadi dakika 90 zinamalizika ubao ulisomeka Liverpool 5, Arsenal 1. |
LIVERPOOL imewadhalilisha waliokuwa vinara wa ligi kuu ya England, Arsenal baada ya kuwaangushia kipigo kikali cha magoli 5-1 katika uwanja wa Anfield.
Arsenal ambao waliwasili Merseyside wakijiamini kutokana na kuongoza ligi hiyo kabla ya mchezo huo, walijikuta wakiambulia kipigo cha magoli 4-0 katika muda wa dakika 20 tu tangu kuanza kwa mchezo.
Skirtel akipachika magoli yake katika dakika ya 1 na 10, Sterling akiongezea machungu kwa Arsenal kwa kupachika goli la tatu katika dakika ya 16 na Sturridge akihitimisha karamu ya magoli ya Liverpool kwa dakika 45 za kwanza za mchezo kwa kupachika goli katika dakika ya 20.
Kana kwamba haitoshi, mitutu ya Arsenal ilishindwa kabisa kufyatuka kwani katika dakika ya 52, Sterling tena alipachika goli la pili, likiwa la tano kwa Liverpool. Hata hivyo, vijana hao wa London, hawakukubali kutoka mikono mitupu, kwani katika dakika ya 69, Arteta alipachika mkwaju wa penalti na hivyo kukamilisha mechi hiyo kwa jumla ya magoli 5-1.
Matokeo hayo yalibadilisha msimamo wa ligi hiyo. Chelsea baada ya ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Newcastle, kuliwapandisha kileleni mwa ligi hiyo, ikiwa imejikusanyia pointi 56, Arsenal ikiteremka na kukalia nafasi ya pili ikiwa na pointi 55, Manchester City nayo imeteremka na kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54 baada ya kubanwa mbavu na Norwich ambao walitoka nao sare ya kutofungana.
Liverpool kwa sasa imejikusanyia pointi 50 na kutulia nafasi ya nne baada ya michezo 25 kwa timu zote hapo juu.
Manchester United leo inakipiga na Fulham inayozibeba timu zote 19, ikiwa ni ya 20. Pia mchezo mwingine mkali unatarajiwa kuwa kati ya Tottenham yenye pointi 44 dhidi ya Everton yenye pointi 45 ikiwa nafasi ya tano.
Everton ikishinda itabakia nafasi yake ya tano kwani itakuwa na pointi 48, lakini Tottenham ikishinda basi itachukua nafasi ya sasa ya Everton kwa kufikisha pointi 47. Ushindi wa Manchester United dhidi ya Fulham hautabadili nafasi yake ya saba, mbali na kujiongezea pointi. Kwa sasa ina pointi 40.
CHANZO: BBC SWAHILI.Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.