ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, November 6, 2013

TIDO MUHANDO NI MGENI RASMI TUZO YA DAUDI MWANGOSI ITAKAYO TOLEWA JIJINI MWANZA ALHAMISI HII

Jumla ya wageni 120 toka ndani na nje ya nchi, watahudhuria hafla ya kutunuku TUZO YA UANDISHI WA HABARI ZA KISHUJAA NA UTUMISHI ULIOTUKUKA, YA DAUD MWANGOSI, shughuli itakayofanyika kesho Alhamisi ya Tarehe 07 NOV 2013 katika ukumbi wa JB Belmonte.
Akizungumza jana na waandishi wa habari wa jijini Mwanza, Rais wa Umoja wa vyama vya waandishi wa habari nchini Tanzania UTPC Keneth Simbaya amesema kuwa tuzo hizo licha ya kutumiaka kama sehemu ya kumuenzi hayati Mwangosi na kukemea vitendo visivyofaa wanavyo tendewa wanahabari pia ni muendelezo wa harakati za UTPC  kuzithamini juhudi za waandishi wa habari wanaoitetea tasnia ya habari kwa ustawi wa jamii.
Kwa mshindi ambaye atakuwa amekidhi vigezo vilivyowekwa basi tuzo itakuwa yake, tukio litafanyika hiyo kesho katika Hoteli ya JB Belmonte, kuanzia saa 3.00 asubuhi.
Tuzo hii ilianzishwa rasmi kwa azimio la Bodi ya Wakurugenzi ya UTPC, nambari 11.1 katika kikao chake kilichofanyika tarehe 20/3/2013.
Mshindi wa Tuzo hii atatangazwa na Jopo la Majaji ambao liliundwa na Bodi ya Wakurugenzi ya UTPC, tarehe 29/6/2013.
Wajumbe wa Jopo hili la Majaji ni:-
Nkwabi Ng’wanakilala       :           Mwenyekiti
Leila Sheikh                           :           Mjumbe
Hamza Kassongo                 :           Mjumbe
Dr Ayoub Rioba                   :           Mjumbe

Jopo hili la Majaji lilifanya kazi kwa kipindi cha miezi miwili (2), wakiongozwa na hadidu za rejea zilizoundwa na Bodi.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mwananchi Communications Ltd, Tido Mhando. Wageni wengine wanatoka kwenye ofisi za kibalozi zilizoko nchini, viongozi wa klabu za waandishi wa habari (press clubs), viongozi wa dini, wahariri wa vyombo vya habari, asasi za kiraia na viongozi wa vyama vya kisiasa.
Tuzo inatolewa kwa mara ya kwanza, katika historia ya tasnia ya habari nchini, ili kuwaenzi na kuwatambua waandishi wa habari, ambao wanateswa, wanadhalilishwa, wanapigwa na hata kuuwawa kwa ajili ya kazi zao za uandishi wa habari.
Tuzo hii imepewa jina la Daud Mwangosi, Mwenyekiti wa Iringa Press Club, ambae pia alikuwa anakitumikia kituo cha televisheni cha Channel 10, ambae aliuawa 2 Septemba, 2012, katika kijiji cha Nyololo akifanya kazi yake ya uandishi wa habari.
Ni mwandishi wa habari wa kwanza Tanzania, kuuawa akifanya kazi yake ya uandishi wa habari. Ni wajibu wetu waandishi wa habari nchini Tanzania kuwaongoza wapenda amani nchini kumuenzi na kumkumbuka marehemu Mwangosi Daima.
Aidha ni wajibu wetu kulaani unyama huu aliyofanyiwa Mwangosi kwa nguvu zetu zote. Ni matarajio yangu kwamba waandishi wa habari wa Tanzania, wataungana na UTPC kuhakikisha mkondo wa sheria unachukua nafasi yake ili haki ya Mwangosi ipatikane.
Waheshimiwa wanahabari, kama nilivyoeleza katika taarifa hii, kwamba Siku ya kumtangaza na kumtunuku tuzo mshindi imewadia. Anayemjua mshindi wa tuzo hii ni Jopo la Majaji ambao siku hiyo ya tarehe 7/11/2013 mbele ya umma wa Watanzania watamtangaza mshindi huyo.
Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya UTPC, na viongozi wote wa Klabu za waandishi wa habari nchini, nawapongeza Jopo la Majaji kwa kazi nzuri waliyofanya, ya kumchagua mshindi.
Mwisho nawaomba mtusaidie kuwaarifu Watanzania juu ya hafla hii.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Kenneth Simbaya

Rais








Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.