Ni moja kati ya eneo linalo ripotiwa mara kwa mara kutokea ajali. |
TANROAD Mkoa wa Mwanza imeanza oporesheni ya kuvunja majengo, vioski na kuwaondoa watu waliovamia na kujenga kando ya barabara ikiwemo kufanyabiashara ndani ya hifadhi ya barabara za Jijini Mwanza na zile zilizopo kwenye Wilaya zote za Mkoa huo.
Meneja wa TANROAD Mkoa wa Mwanza Mhandisi Leonard Kadashi alieleza toka ofisini kwake kwamba muda wa wiki tatu uliokuwa umetolewa tayari umekwisha kwa watu waliovamia hifadhi kuondoka kwa hiari.
“Tulitoa wiki tatu na zimeisha hivyo leo tunaanza rasmi zoezi la kuwaondosha watu wote waliovamia na kufanya ujenzi pamoja na wale ambao wamekuwa wakipanga bidhaa zao kandokando ya barabara kwa lengo la kufanya biashara ikiwemo pia sehemu za kuoshea magari, mashine za kusaga na kukoboa nafaka zoezi ambalo litakuwa maalum kama safisha barabara zinazomilikiwa na wakala wa barabara Mkoani hapa”alisisitiza.
Mhandisi Kadashi alisema kwamba baadhi ya barabara zilizo chini ya TANROAD Mkoani Mwanza zimevamiwa na watu ambao wamekuwa wakivunja sheria na kuamua kufanya ujenzi na biashara holela pia wamekuwa wakikaidi kuondoka ama kuacha kuendelea na ujenzi katika maeneo mbalimbali pamoja na kuwekewa alama za X.
“Tunazingatia sheria kwa hili hivyo naomba wananchi na watu waliovamia barabara hizo kuwa ndani ya hifadhi, watuelewe na maandalizi ya zoezi la kuwaondoa tayari yamekamilika na leo tunaanza rasmi tukienda sanjari na ubomoaji ”alisema Kadashi.
Hatua hiyo ya TANROAD kuwaondosha waliovamia kandokando ya barabara zake ilifuatia hoja iliyowasilishwa na Mhandisi Kadashi Machi 21 mwaka huu wakati wa vikao viwili ngazi ya Mkoa cha Bodi ya barabara na kile cha Kamati ya ushauri Mkoa wa Mwanza (RCC) na kukubaliana na hoja hiyo kisha kutoa maazimio ya kutekelezwa haraka zoezi hilo ili kuokoa maisha ya watu pindi magari yanapopata ajali.
Jeh karakana hii ya mashine ya kusaga na kukoboa iliyo pembezoni mwa barabara eneo la Mabatini itasalimika? |
Alizitaja baadhi ya barabara ambazo ziko Jijini Mwanza zitakazohusika na zoezi hilo ni pamoja na barabara ya Kenyata kwenda Mkoa wa Shinyanga, barabara ya Nyerere hadi Mkoani Mara na Simiyu, barabara ya SAUT Nyegezi na zingine zote zilizo chini ya TANROAD zikiwemo zile za kuunganisha Makao makuu ya Wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Meneja, Mhandisi Kadashi ametoa rai kwa watu waliovamia barabara hizo kutojaribu kufanya mgomo wa kuondoshwa katika maeneo ya hifadhi ambayo ni mita 30 kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na badara yake waanze kuondoka wenyewe kabla ya kukumbwa na zoezi hilo na watakaokaidi watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kulipa garama za ubomoaji wa majengo na vioski na hakuta kuwa na fidia yoyote baada ya zoezi hilo kutekelezwa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.