ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 30, 2013

KUSIMAMISHWA KWA KIVUKO CHA MV SAMER THREE, WANANCHI WA SENGEREMA WADAI WIZARA YA UCHUKUZI IMEKURUPUKA.

Wananchi takribani 3000 kati ya 5000 hadi 6000 ya wanaovuka kwa siku kwa wilaya ya Sengerema na mkoa wa Mwanza watapaswa kutafuta mbinu mbadala kupata huduma ya kivuko toka jijini Mwanza hadi Kamanga wilayani Sengerema kutokana na Serikali kusimamisha huduma za kivuko cha MV.  Samar 3.


 Blogu hii, leo kuanzia asubuhi imeweka kambi katika eneo la Kamanga ambako kuna kivuko cha Samar 3 na kukuta mamia ya abiria wakihaha kwenye mvua wakilalama na kulaumu juu ya usitishwaji wa safari hizo na wasijue jinsi ya kuweza kuwahi makazini, nao wafanyabiashara hususani mama lishe wakilalamika kupata hasara kutokana na kukosa wateja. 


Msikilize Bi Wema Binti Said. Kwa kubofya play...
Sikiliza machungu ya mama Joyce Mlobi, yanayotokana na kusitishwa kwa huduma ya kivuko hicho. Msikilize


Msikilize Mfanyabiashara huyu aitwaye Ernest Masha ambaye naye kaathirika kibiashara kufuatia hatua hiyo.. Msikilize




Mnamo tarehe 29 mwezi January 2013 (jana) Uongozi wa TPA Mwanza ulituma barua ya kusimamishwa ukodishaji wa eneo la Mwanza Kaskazini kwa mmiliki wa kivuko cha MV. Samar 3 ukimtaka mmiliki huyo kuhamia kwenye ramp ya bandari ya Kaskazini iliyokuwa ikitumiwa na MV. Serengeti, eneo linalohitaji marekebisho makubwa ili usafirishaji uanze.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kivuko cha MV. Samar 3, Bw.  Salum Ally amesema kuwa kabla ya  barua hiyo ya jana alikuwa na order ya Mahakama Kuu Mkoa wa Mwanza iliyotolewa mnamo tarehe 23/12/2012 iliyoamuru kivuko hicho  kuendelea kutoa huduma kufuatia kusimamishwa kufanya shughuli zake kwa mara ya kwanza mnamo tarehe 19/12/2012.

Lakini anashangaa juu ya maamuzi hayo Serikali kupitia Wizara yake ya Uchukuzi, kuitoa kampuni yake kwenye utoaji huduma bila kufuata taratibu za utawala bora na kuwaacha wananchi wakitaabika.


Msikilize ...




Naye Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Bandari wa Kanda ya Ziwa (TPA) Bw. Richard Msechu licha ya kukiri kushuhudia kuona wananchi wakitaabika kupitia uamuzi huo wa Serikali, amesema ofisi yake inatekeleza agizo iliyopewa toka Wizarani hivyo inahaha kuhakikisha kuwa eneo jipya linakamilika… Msikilize

Hili ndilo eneo jipya ambalo linahitaji matengenezo makubwa na kwa takwimu za haraka litachukuwa zaidi ya wiki mbili kukamilika ili shughuli ya usafirishaji ipate kuanza, swali ni kwamba kwanini serikali isingekamilisha kwanza ujenzi wa eneo hili na kuwa salama kwa kupaki kivuko kisha ikatoa tamko la kuhama kwa kivuko cha Samer toka eneo la zamani, au ndiyo kukomoana? Hii haiingii akilini.

Kivuko cha MV. Samer kikiwa kimepaki mara baada ya kupigwa stop kutoa huduma kisa kukatisha katika sehemu ya njia za treni ielekeayo bandari ya Kaskazini, ambayo hata hivyo hakuna jengo lililojengwa juu yake zaidi ya magari kupita juu ya reli kitendo ambacho ni kawaida na vilevile treni za mizigo bado hazijaanza kufika bandarini kupakia mizigo ya bandari zote zikikomea stesheni kuu ya Mwanza .
Msongamano eneo la Kamanga.

Kivuko kilichobakia sasa katika utoaji huduma ya usafirishaji cha Kamanga kimeonekana leo kuzidiwa kwa mabasi na abiria kufurika hadi njia kuu kwani kina uwezo wa kubeba abiria 250 tu kwa safari ile hali kivuko cha Samar 3, kina uwezo wa kubeba abiria 390 na tani 320 za mizigo kwa safari na kwa siku kikivusha abiria 2500 hadi 30000.

Jumla ya  wastani wa abiria 5000 hadi 6000 hutumia vivuko vyote viwili.

Hivyo kuondolewa kwa MV. Samer 3 katika utoaji huduma ni athari kubwa kwa maendeleo na uchumi wa wakazi wa wilaya ya Sengerema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.