ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 14, 2012

MAUAJI YA KUTISHA MARA,WATU WAKATWA VISHWA, SERIKALI YADAIWA KUTUMIA WAANDISHI UCHWARA NA WENYE NJAA KUKANUSHA UKATILI HUO


TUNAOMBA RADHI KWA PICHA HII
Na George Marato,Musoma
Kufuatia mauji ya kinyama na kutisha kuibuka mkoani Mara, hatimaye jeshi la Polisi mkoani humo, limetoa tahadhari kubwa kwa wananchi wa Mkoa huo hasa  Wanawake wa maeneo ya vijijini kuwa makini  wakati wakiwa katika shughuli kilimo na utafutaji wa kuni.

Pamoja na tahadhari hiyo pia wananchi hasa wanawake wameombwa kutoa taarifa polisi pindi tu wanaposhuku kuwepo kwa jambo lolote ambalo linahatarisha maisha yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mara SSP Japhet Lusingu,ametoa taadhari hiyo juzi ofisi kwake mjini hapa wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na matukio ya mauji ambayo yameibuka katika siku za hivi karibuni mkoani Mara hasa katika wilaya ya Butiama na Manispaa ya Musoma .

Alisema tayari jeshi la polisi linawashikiria watu sita kuhusiana na mauji ya Sabina Mkireri mkazi wa kijiji cha Kiemba ambaye aliuawa kwa kuchinjwa kisha wauji kuondoka na kichwa chake Desemba tatu mwaka huu.

“Nachukua nafasi hii kuwatoa hofu wananchi kuhusu mauji haya,lakini natoa taadhari kwa wakina mama hasa wa maeneo ya vijijini wanapokuwa katika shughuli za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema pindi tu wanaposhuku kuwapo kwa jambo lolote lisilo la kawaida”alisema kaimu kamanda huyo ambaye pia ni afisa mnadhimu wa jeshi la polisi mkoa wa Mara.

Aidha alisema Desemba mbili mwaka huu majira ya saa moja usiku Brandina Peru alikutwa polini akiwa amekufa baada ya kuchinjwa.

Kaimu kamanda huyo wa polisi mkoa wa Mara,alisema marehemu kabla ya kuuawa kikatili aliondoka nyumbani kwake desemba mosi mwaka huu akiwa peke yake kwenda porini kukata kuni na hakuweza kurudi nyumbani hadi alipokutwa amekufa kwa kuchinjwa.

Hata hivyo alisema kabla ya kuchinjwa wauaji hao walimvua nguo zote na kuweka kando kisha kumbaka na kwamba hakuna mtu yoyote aliyekamatwa hadi sasa na chanzo cha tukio bado kinachunguzwa.

Kwa sababu hiyo alisema jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kwaajili ya kuwasaka watu wanahusika na vitendo hivyo huku akiwaamba waandishi wa habari na viongozi wa kisiasa kutowatia hofu wananchi kwa kutoa taarifa bila kuthibitishwa na vyombo vya dola.

Kuhusu taarifa za viungo hivyo vya binadamu kutumika kwa imani potofu kwa shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi wa samaki alisema jeshi hilo linachunguza ukweli wa taarifa hizo.

Wakati huo huo,kamanda Lusingu,alisema mwanafunzi mmoja Hamis Lazaro wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Etaro ameuawa kwa kushambuliwa,mawe na kukatwakatwa na mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alisema tukio hilo lilitokea saa 11.30 katika kijiji cha Kwikerege kata ya Etaro wilaya Butiama baada ya kukutwa chini ya uvungu wa kitanda kilichokuwa kikitumiwa na Nyakongo Nyangata ambaye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi.

Hata hivyo kamanda huyo alisema mbali na madai ya marehemu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo mwenzake lakini wananchi walijichukulia sheria mkononi baada ya kuisi kuwa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya mauji ya kinyama katika eneo hilo.


UCHUNGUZI
 SAKATA la mauji ya kinyama mkoani Mara,imani za kishirikina ni moja ya sababu kubwa ambazo zimetajwa kuwa chanzo kikuu cha mauji hayo ambayo yameibuka kwa kasi kubwa katika mkoa huu hasa kwa wilaya za Butiama na Musoma mjini huku wauaji wakichukua baadhi ya viungo vya binadamu kwa madai ya kusadia shughuli za uvuvi wa samaki na uchimbaji wa dhahabu.

Imedaiwa kuwa wauji hao wengi wamekuwa wakitoka mkoa wa Kigoma wakiwa ni wenyeji wa nchi jirani ya Congo ambao wamekuwa wakishirikiana na wenyeji katika maeneo hayo kisha kufanya mipango ya mauji hayo ya kinyama.

Baadhi ya wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini,wamedai kuwa wauji hao wamekuwa wakiuza vichwa vya watu kwa imani za kishirikina kwaajili ya shughuli za uchimbaji wa dhahabu huku ndimi,matiti na sehemu za siri vikitumika kwaajili ya uvuvi katika ziwa Victoria.

Aidha imedaiwa kuwa baadhi ya Mangariba pia kutoka eneo la Tarime na Kiagata wamekuwa wakiwauzia wavuvi viungo vya mwanamke baada ya kuwakeketa jambo ambalo limetajwa kuwa chazo cha kusababisha wimbi la mauji ya watoto wa kike ambao wamekuwa wakiuawa kisha kunyofolewa viungo hivyo yakiwemo na matiti.

Hata hivyo baadhi ya wavuvi ambao wameomba kuhifadhiwa majina yao kutoka visiwa ndani ya ziwa victoria wakizungumza kwa njia ya simu na Nipashe Jumapili kwa nyakati tofauti,wamedai kuwa pamoja na matajiri wao kununua viungo hivyo kutoka kwa baadhi ya watu lakini hakuna mabadiliko yoyote ambayo wamekuwa wakiyapata.

“Kweli kuna wakati watu wanakuja eti ni waganga kisha wanakwenda ziwani usiku na matajiri na mwakilishi wa wavuvi kwa kila mtumbwi ili  kuonyesha nyavu zilipo wakifika wanachukua vitu kama nyama wanasugua kila mwesho wa nyavu lakini hatujawahi kuona mabadiliko ya kuongeza samaki”alisema mmoja ya wavuvi.

Wavuvi hao waliongeza kuwa watu hao wanaoisi kuwa ni waganga wamekuwa wakiwazuia kuongea kitu chochote wakati wa zoezi la kufanya mitambiko hiyo huku wao wakizungumza lugha na maneno wasio yaelewa hadi zoezi hilo linapo malizika.

Walipohojiwa ni kwanini wanashindwa kutoa taarifa hizo kwa vyombo vya dola wavuvi hao walidai kuwa wanashindwa kufanya hivyo kwa kuhofia maisha yao kwa vile wamiliki wengi wa zana hizo za uvuvi wana mahusiano makubwa na baadhi ya maafisa ambao wako katika vyombo vya dola.

Hata hivyo wachimbaji hao wa dhahabu wameshindwa kuwa wazi kila walipoulizwa ili kuthibitisha viungo hasa vichwa vya binadam vimekuwa vikitumika wakati gani na kwa maeneo yapi.

Kwa upande wake mbunge wa Musoma vijijini Nimrod Mkono,pamoja na kutoa pole kwa wote ambao wamekumbwa na janga hilo,lakini alisema jeshi la polisi linapaswa kuwachunguza wanasiasa kwani alisema wakati mwingine wamekuwa wakishiriki katika ushirikina huo kwaajili ya kujipatia fedha.

“Hali hii inatisha inawezekana vitu hivi vikatumika kwa ushirikina katika madini na uvuvi lakini miongoni mwetu wanasiasa ni vyema tukachunguzwa kwani wengini hawamuogopi mungu wanaweza kufanya mchezo huo mchafu kwaajili ya kupatafuta pesa za uchaguzi na wengine kufanyia mitambiko ya biashara zao”alisema Mkono kwa njia ya simu na kuongeza

“Hilo ni jambo kubwa haiwezekani mtu wa kawaida tu akaenda kumchinja mtu na kuondoka na kichwa chake bila ya kuwapo kwa mkono wa watu wenye uwezo,hivyo ni vyema jeshi la polisi likafanya uchunguzi wa kina kuhusu hali hii”alisema.

Juzi mbunge Musoma mjini Vicent Nyerere(Chadema) alimtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP)Said Mwema kuchukua hatua sasa kuhusu mauji mauji ya kikatili ambavyo yameibuka katika Manispaa ya Musoma na wilaya ya Butiama.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema katika kipindi cha mwezi mmoja tu zaidi ya watu kumi na saba wameuawa huku wengine wakichinjwa kicha waujia kuondoka na vichwa na viungo vyao vingine vya miili yao.

Alisema pamoja na hali hiyo ambayo imechangia hofu kubwa kwa wananchi lakini hakuna jitihada zozote zinazochukuwa kwaajili ya kukabiliana na vitendo hivyo vya kinyama.

Aidha mbunge huyo alimtaka pia Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua kwa wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wa wilaya hizo ambao amedai baadhi yao wameshindwa kusimamia majukumu yao na kubaki kuendesha siasa wakati wananchi wakizidi kuawa kinyama na wengine kuachwa na vilema vya maisha.

“Ni tatizo kubwa ndani ya mwezi mmoja tu watu kumi na saba wameuawa kinyama na wengine kuchinjwa lakini mbali na vyombo vya dola kukaa kimya hata nyinyi waandishi mmeshindwa kujulisha umma kuhusu ukatili huu”alisema Nyerere na kuongeza.

“Rais mtoe mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya(DC) hapo Musoma amekalia siasa na kuacha majukumui ya serikali katika kulinda raia na mali zao hii ni hatari kubwa”aliongeza.

Hata hivyo wakati mbunge huyo akitoa kauli hiyo,mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Butiama Angelina Mabula,ameliagiza jeshi la polisi kufanya kazi usiku na mchana katika kuhakikisha linawatia mbaloni watu wote ambao wanahusika na mauji ya kikatili ya raia.

Mabula ambaye ni mkuu wa wilaya ya Butiama,alitoa agizo hilo juzi jioni baada ya kuokotwa kwa mama mmoja Sabina Mkereri (46)ambaye alichinjwa na wauji kuondoka na kichwa chake katika kijiji cha Kabegi kata kata ya Nyakatende.

“Nawaomba wananchi mtoe ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wahusika wote wanasakwa na kuanzia sasa naagiza kuanza kwa vikundi vya ulinzi shirikishi kwaajili ya kufanya kazi ya kuwasaka watu hawa usiku na mchana…jamani tunaipeleka wapi Tanzania yetu yenye amani kwa kufanya matendo haya ya kinyama”alisema DC Mabula.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mara SSP Japhet Lusingu,akizungumza na gazeti hili pamoja na kukiri baadhi ya watu kuchinjwa na viungo vyao kuchukuliwa lakini alisema idadi inayotajwa si sahihi.

Alisema tayari jeshi la polisi limechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vitendo hivyo vya kinyama huku akisema jeshi lake linachunguza kuhusu viungo hivyo kutumika kwa shughuli za uvuvi na ushirikiana.

Hata hivyo aliwaomba waandishi na viongozi wa siasa kuacha kutoa taarifa ambazo si sahihi bila kuthibitishwa na jeshi hilo ili kutowaweka katika hali ya hofu wananchi. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.