Musoma,
Wazazi wanaodaiwa kuwatelekeza watoto wao watatu na kuwasababishia kuishi
maisha ya kutangatanga mitaani leo wamejisalimisha katika kituo kikuu cha Polisi
mjini Musoma kitengo cha dawati la jinsia na watoto baada ya vyombo vya Habari
kutangaza tukio hilo huku kila mmoja akimtupia mwenzake lawama kwa kile
kilichosababisha watoto hao kuishi maisha hayo.
Akizungumza mbele ya jopo la wana dawati pamoja na waandishi wa habari,mama
wa watoto hao Paulina kichere alimshushia lawama mzazi mwenzake Kichere Sangi
kwa kile alichokieleza mara baada ya kutaarikiana mwaka 2007 mahakama ilimtaka
kukaa na watoto hao kutokana na mama kutokuwa na uwezo wa kuwatunza lakini mara
baada ya mzazi mwenzake kuoa wanawake wengine wawili watoto hao wamekuwa
wakilalamika kutokuwa na malezi mazuri.
Amesema mara kadhaa watoto hao wamekuwa wakimfata na kulalamika kupewa kazi
zinazowazidi uwezo mara baada ya kutoka shuleni huku watoto wengine ambao
mwanaume huyo amezaa na wanawake wengine aliowaoa wakipata muda wa kusoma na
kushindwa kufanya kazi nyingine za nyumbani.
Paulina amesema licha ya mji ambao waliangaika kuujenga kwa pamoja katika
maisha yao ya ndoa kuuacha kwa ajili ya malezi ya watoto anashangaa kitendo cha
mzazi mwenzake kuacha watoto wakiteseka mtaani huku akijua yeye kwa upande wake
hana uwezo wowote wa kuwatunza kutokana na kutokua na kazi ya kumuingizia kipato
chochote.
Amesema yeye kwa upande wake hawezi kuangalia watoto wake wakiishi maisha
ya kuangaika kama angekuwa na uwezo wa kuishi nao na kuomba vyombo vya sheria
viweze kuliangalia suala hilo kwa mapana ili kuwaepusha watoto hao na maisha ya
mitaani.
Kwa upande wake baba wa watoto hao Justine Kichere (14) James Kichee (13)
na Gerald Kichere (12) Kichere Sangi amesema licha ya kuwa anashinda katika
shughuli zake muda mwingi hana uhakika kama watoto hao wanaishi maisha ya
kuteswa kutokana na kutokupata taarifa hizo.
Amesema licha ya kutengana na mama wa watoto hao amekuwa akiishi nao bila
kubaguliwa na kudai kuwa watoto hao waliondoka nyumbani bila yeye kuwa na
taarifa na alijua walikuwa wamekwenda kwa mama yao kama ambavyo wamekuwa
wakifanya mara kwa mara.
Afisa mmoja katika kitengo cha dawati la jinsia na watoto kutoka jeshi la
Polisi ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa sio msemaji amesema baada ya
kufika kwa wazazi hao katika ofisi hiyo walizungumza nao huku kila mmoja
akimlushia lawama mwenzake juu ya malezi ya watoto hao na walichokiamua cha
kwanza ni kulipeleka suala hilo katika ofisi ya afisa Maendeleo ya Jamii kwa
hatua zaidi juu ya malezi ya watoto hao.
Amesema licha ya kulipeleka suala hilo katika ofisi ya afisa Maendeeo ya
Jamii wataendelea kulifuatilia kwa karibu kujua hatima ya watoto hao na malezi
yao ili kuweza kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani na ofisi ya dawati la
jinsia na watoto halita sita kuwafungulia mashitaka wazazi wote ambao bila
sababu za msingi wanazalisha wtoto wa mitaani.
Siku tatu zilizopita Watoto
hao watatu waliwafikisha wazazi wao katika kituo kikuu cha Polisi Mjini Musoma
kitengo cha dawati la jinsia na watoto wakidai kutelekezwa na kuwafanya kuishi
maisha ya kutangatanga mitaani ili hali wazazi wao wakiwepo na kuendelea na
maisha ya kila siku bila kujua wao wanaishi vipi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.