ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, July 31, 2012

KWA NINI MWALIMU ANADHARAULIKA?

Watoto wanauliza wafanyeje?
Na Katila Mkumbo
MIMI nionavyo Mwalimu ni sawa na kibao kielekezacho mtaa. Yaani unapokuwa katika makutano ya barabara unatafuita njia ya kwenda uendako na kando yako huna mtu wa kuuliza basi utakuta kuna kibao, hiki kitakusaidia sana kuelekea uendako.

Angalia hata wakati unapokuwa safarini na njia hiyo umeanza kuipita kwa mara ya kwanza, na upo mahari hujui umefika wapi, bahati mbaya unamuuliza jirani yake pembeni ya kiti anakujibu pia kuwa ajui hapo ni wapi, lakini unaona kibao kielekezacho mtaa, utakisoma na kutambua kuwa kumbo upo katika kijiji cha Nshamba.

Ukweli ni kuwa kibao kiuelezeao mtaa kina faida sana, lakini bahati mbaya sana faida yake ipo wakati ule kihitajikapo kuelekeza mtu. Ndiyo huu ndiyo ukweli, angalia, Ukijua kule uendako huhitaji kuelekezwa tena na kibao.sasa ingawa kitakuwepo faida ya kibao kile haionekani, hivyo kuficha umuhimu wake!

Hebu rudi nyuma, kule uliko soma shule ya msingi, pengine miaka 30 au fanya hata 45 iliyopita, ukiwa hujui kusoma na kuandika, mambo yalikuwaje na pima na sasa wakati ambapo unaandika na hata kusoma mamabo mbalimbali halafu fikiria kama ungekuwa hujui kusoma na kuandika, nini ungekuwa umepungukiwa? Je, katika fikra zako umebahatika kufikiri aliyekufanya ujue hayo? Basi hicho ni ‘kibao’ kilichokufanya uelewe.

Juzi nilirejea kijijini kwetu Busisi na kukuta mabadiliko makubwa sana kwanza nilikuta barabara ya lami ikiwa imejengwa na nyumba zile nilizokuwa nimezizoea zilikuwa zimebomolewa na kujengwa mpya, kwa hakika mji ulikuwa umebadilika sana. Sikujua nianzie wapi, lakini niliogopa kuuliza kwani, kama ningekosea na kuuliza kwa mtu ambaye nilicheza naye utotoni sijui ingekuwaje, nadhani ngenicheka na hata kunibeza kuwa nimesahau kwetu kutokana na kukulia mjini.

Nilijipa uhakika wa kutembea huku nikijaribu kuangaza angaza iwapo nitapata kumbukumbu ya eneo ambalo lingerejeleza kumbukumbu na taswira ya kule niendako. Kama hatua chache baada ya kutembea nilibahatika kuona kibao cha shule kilichokuwa kimeandikwa Shule ya Msingi Busisi.

Nilipata faraja, na kuanza kuvuta taswira ya enzi hizo nikiwa mwanafunzi. Nilisimama na kukiangalia, ukuta wake ulikuwa ni ule wenye maandishi. Tena bahati nzuri niliweza kuyakumbuka kuwa ni yale tuliyoandika miaka ile iliyopita. Nilisita, na kusimama kwa muda kukiangalia, lakini si kwa kukipatia heshima kibao licha ya kunipa kumbukumbu za uelekeo wa nyumbani kwetu, bali kukumbuka ya miaka iliyopita wakati nikisoma.

Sasa nilijua wapi niendako, sikuhitaji kuelekezwa na kibao cha kuelekeza ulekeo wa shule au jina la shule, cha nini kwangu tena? Lakini kimenisaidia kujua wapi nielekee.

Wakati nikielekea nilikutana na mzee mmoja sura yake haikuwa ngeni kwangu, nilimtizama kwa muda kasha nikataka kuendelea na safari lakini nilisita kwani kumbukumbu zilinijia, alikuwa ni Mwalimu wangu. Mbona yuko hivi, sikujua, lakini baada ya kumsogelea nilitambua kuwa alikuwa vile kutokana na hali ya maisha tu. Ila mfukoni alikuwa na chupa mbili za bia zikiwa na kimiminika, nadhani pombe aina ya Gongo.

Moyoni nilijiuliza, ndiye, ni mwalimu, tena aliyenifundisha a, e, I, o, u, lakini nilisha jua kusoma na kuandika simhitaji. Na wala sihitaji tena kujifunza kusoma na kuandika na mwalimu wa masomo hayo ana faida gani kwangu?

Nilianza kuondoka kuendelea na safari yangu huku mwalimu Yule nikimpuuza kama mlevi nisiyemjua, lakini looo..! alikuwa makini kumbu aliweza kunitambua, aliniita jina langu na kunieleza, "Fred umekua, najua umehitimu chuo kikuu, lakini mimi ndiye kibao chako kilichokuonyesha njia ya kufika huko, japo ungenisoma tu, kuliko kunipita hivyo" Nilisimama.

Nikakumbuka kibao cha awali jinsi kilivyonisaidia kujua uelekeo wa nyumbani kwetu, nikajiopna mpumbavu kwa kutomsaliamia hata mwalimu wangu ambaye alinitoa katika elimu ya UPE aliyenifundisha kwa bidii zake zote, na hatmaye kuhitimu elimu ya juu, leo nikiwa mkurugenzi wa kampuni ya D.

Mwalimu hubadilika umri, umbile, lakini habadiliki maana na umuhimu wake kwa mfano wa kibao kilekezacho mtaa. Mwalimu ni mwanafunzi wa kudumu, Mwalimu huendelea kujifunza na kufundisha kwa uvumilivu wote, raha yake siyo malipo ya mshahara wa shilingi bali ni kuona aliyemfundisha a, e, i, o, u akiwa katika mafanikio. Mwalimu halisi hufundisha kwa wito na mvuto na si kwa faida ipimwayo na uwingi wa fedha. Ndiyo maana aliyenifundisha miaka hiyo bado mpaka leo yupo, hajaacha kukimbilia kazi kama yangu.

Isipokuwa sisi tuliofundishwa na walimu walio sawa na vibao nilivyovielezea hapa ndiyo tubadilikao kutoka katika hali tete na ujinga hadi na kufikia kupata maarifa mengi ya hali ya juu na kukosa nidhamu hata kudiriki kusahau njia tuliyopitia, achilia mbali kumtengenezea mshahara mzuri mwalimu.

Walimu amesahaulika na sisi wote kabisa siyo serikali tu. Ndiyo sisi wote! Wanafunzi tukiwakumbuka na kuwaenzi walimu katika maisha yao ya kila siku watasahaulikaje?. Nani mwenye cheo kikubwa sana hapa Tanzania liyefika hapo alipo hakukunjwa akingali mbichi na walimu na kupewa ujanja wote alionao leo? Siyo anayeandaa mishahara wala anayehusika na kuwalipa mishahara. Masikini Mungu atuhurumie kwani sisi wanafunzi tumejaa dharau kubwa na kiburi hii ndiyo asili ya walimu kudharauliwa.

Watu wengi tunachukia kwenda tuliko soma, wale wa umriwangu na zaidi wanadai maeneo ya shule yanawakumbusha mboko walizo rambwaenzi zile hadi kutoa mchozi mbele ya ndito zao (washikaji) wapowaliozichukia jumla leo wanazililia kwa kukosa elimu. Wengine walikuwa nachuki biafasi na walimu wao.

Angalia wabunge wanavyokopeshwa magari, mwalimu mhmm! Angalia wanavyosotea mishahara wakati wabunge wao kule kumaliza tu kikao cha bunge miaka mitno kiinua mgogo anakilamba mapema bila bugudha, tena anatumbukiziwa beki haraka. Mwalimu je, yeye mshahara wake mpaka tarehe 49 masikini! Tumewasahau ukweli walimu, na hata kama tukikwakumbuka, tunawaita na kuwafanya mashahidi wa kusimamia kura zetu katika uchaguzi ili waone jinsi utakavyoingia Bungeni kulamba mkopo wa gari na kiinua mgogo cha milioni 46 baada ya miaka mitano.

Ni ukweli, tumewasahau walimu! Tumesahau walimu kwa sababu tulichotaka walisha tupatia siku nyingi, na sasa wamekuwa kama ganda la muwa la jana ambalo ulishalifyonza usukari wake wote na kulitupa sasa walikanyaga.

Ndipo baada ya fikra zote hizo nilipoweka mkono mfukoni mwangu na kutoa noti ya sh. 5,000 na kumpatia mwalimu wangu na kuendelea na safari yangu. Nilimwambia; Pole mwalimu, naye kunijibu ‘asanate lakini siku utakayoamka, Sijui!?’.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.