Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Job Masima, Jenerali Kiaro amefariki dunia saa 4.20 asubuhi kwa ugonjwa akiwa katika Hospitali ya Bugando Mwanza.
Masima alisema mipango ya mazishi inafanywa kwa pamoja kati ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na familia ya Marehemu. Aidha, alisema ratiba ya mazishi itatolewa baadaye.
Jenerali Kiaro alikuwa ni Mkuu wa Nne wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania kati ya mwaka 1988-1994.
Katika hatua nyingine, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jakaya Kikwete amemtumia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Jenerali Mstaafu Kiaro.
Katika salamu zake kwa Jenerali Mwamunyange, Rais Kikwete amemwomba Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi kumfikishia salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa familia ya Jenerali Mstaafu Kiaro na kwa makamanda na wapiganaji wote wa Majeshi ya Ulinzi kwa kumpoteza mdau, mwenzi wao na kiongozi wao.
Rais Kikwete amesema katika salamu zake, “Nimepokea kwa huzuni nyingi na majonzi mkubwa taarifa ya kifo cha Jenerali mstaafu Ernest Mwita Kiaro ambaye ameaga dunia asubuhi ya leo (jana) katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza, ambako alikuwa amelazwa.
“Nilimfahamu vizuri na nilifanya kazi na Jenerali Kiaro wakati wa enzi ya uhai wake. Alikuwa Mtanzania mzalendo wa kuigwa, mwadilifu na mwaminifu kwa taifa lake, mchapakazi hodari na mpiganaji na Kamanda wa mfano kabisa kwa waliokuwa chini yake,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Alithibitisha sifa zake hizo katika kipindi chote cha miaka 50 na miezi 11 alipokuwa katika ulinzi wa nchi yetu, tokea alipokuwa mpiganaji hadi alipopanda na kuwa Kamanda na hatimaye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha miaka minne kati ya 1988 hadi Februari 25, 1992, alipostaafu utumishi wa Jeshi. Tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi kwa utumishi wake uliotukuka kwa taifa letu.”
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.