Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka, amesema tabia hizo zimekuwa ikiwafanya wananchi wakate tamaa, kwa sababu inawasababisha viongozi wenye tamaa kushindwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na hivyo kugeuka kama maadui wao kwani wanashindwa kutenda haki.
Akihubiri katika Ibada ya Krismasi Kitaifa jana katika Kanisa la Mtakatifu Theresia Mtoto wa Yesu mjini Tabora, Askofu Ruzoka, pia aliwataka viongozi kuhakikisha kuwa utekelezwaji wa sera ya Kilimo Kwanza nchini, haiathiri wananchi na kuwaacha bila ya kuwa na ardhi.
Akizungumzia athari za kutokuwepo kwa Azimio la Arusha, alisema ni pamoja na kuwepo kwa mbio za utajiri baina ya viongozi, kutofuatwa kwa maadili ya uongozi, kutokuwa na miiko, kuongezeka kwa posho katika vikao vingi na kuibuka kwa mrabaha katika kazi mbalimbali za kiserikali na kukithiri kwa tamaa.
Naye Mchungaji Mwaipopo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kanisa Kuu, Dodoma Mjini, amewataka wabunge kuacha ubinafsi wa kujilimbikizia posho kwani hali ngumu ipo kwa kila Mtanzania.
Alisema anashukuru viongozi kutambua maisha ya Dodoma yako juu kiasi kwamba hawawezi kuishi kwa posho ya Sh 70,000 kwa siku.
Alisema maisha ni magumu Dodoma kwa kila mtu si kwa wabunge tu, iweje kundi hilo dogo lisikilizwe je wananchi wakimbilie wapi?
“Kuna kukata tamaa kila kona, kuna majanga ya kutisha, mafuriko, ajali sasa hivi kifo kimetawala duniani kote.” Alisema Mchungaji Mwaipopo.
Naye Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Godfrey Mhogole wa Kanisa la Anglikana, amemlalamikia Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma kwa kufuta matokeo ya watoto waliofaulu darasa la saba mwaka huu.
Alisema iwapo ofisa huyo hataondolewa, yuko tayari kumshitaki kwa kiongozi wa nchi. Alisema kuna haja kwa Ofisa Elimu Mkoa kuangalia kwa kina suala hili kwani halileti picha nzuri katika sura ya elimu nchini.
Alisema katika Shule ya Msingi ya Bishop Stuart DCT iliyopo Msalato mwaka huu walifaulu wanafunzi wanne tu, hali iliyoleta mshtuko kwao.
Alisema kwa miaka mingi shule hiyo imekuwa ikifaulisha sana wanafunzi, lakini anashangaa mwaka huu wanafunzi waliofaulu wamefutiwa matokeo.
Aidha, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha watendaji wa Serikali ‘wachakachuaji’ wanaohusika kwa namna moja ama nyingine kuruhusu wananchi kujenga makazi mabondeni na waliosababisha udanganyifu katika mtihani wa Darasa la Saba.
“Yaliyotokea kwa wenzetu walioathiriwa na mafuriko baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, ni janga kubwa sana na wanahitaji kusaidiwa na Watanzania wote, lakini ninaunga mkono kauli ya Rais Kikwete aliyowaambia waliojenga mabondeni wahame,” alisema Askofu Mkude.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameonya kile alichosema ni baadhi ya watu kuwageuzia na kuwatungia maneno watu wanaojitokeza kupinga dawa za kulevya.
Amesisitiza kuwa dawa za kulevya ni janga la taifa ambalo mapambano dhidi yake hayapaswi kubezwa na mtu yeyote kutokana na namna zinavyoathiri vijana na pia watu wazima.
chanzo: Gazeti la Habari leo
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.