ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, September 1, 2011

BARAZA LA IDDI: JK ATUNISHA MISULI AONYA, MAHAKAMA YA KADHI HAITATEKELEZA SHARIA

RAIS Jakaya Kikwete amelikataa ombi la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) la kuitaka serikali iwarejeshee shule ambazo walikuwa wakizimiliki kabla ya kutaifishwa miaka michache baada ya uhuru.Kikwete alitoa msimamo huo ambao alikiri kwamba unaweza ukawakera baadhi ya Waislamu wakati akihutubia kwenye Baraza Kuu la Iddi lililofanyika kitaifa katika Msikiti wa Gaddafi mjini Dodoma jana.

Badala yake, Rais Kikwete alizitaka taasisi za Kiislamu kuweka msisitizo katika kuzijenga shule mpya kwani maombi yao ya kutaka warejeshewe shule walizokuwa wakizimiliki yamekuja yakiwa yamechelewa.

Alisema uamuzi wowote wa kuzirejesha shule za Waislamu leo unaweza ukasababisha mgogoro mzito kutokana na ukweli kwamba wakati wa utaifishwaji serikali ilichukua shule zilizokuwa zikimilikiwa na taasisi tofauti za kidini na watu wa rangi tofauti.

Akifafanua, Rais Kikwete aliwalaumu Waislamu kwa kuwa mstari wa mbele kunung’unika kwamba wanaachwa nyuma katika masuala ya maendeleo kama yale ya elimu tangu mwaka 1992 pasipo kuchukua hatua zozote.

Kikwete aliyeonekana kuzungumza kwa namna iliyoonyesha kuchukua msimamo mkali na wa wazi dhidi ya maombi ya BAKWATA yaliyowasilishwa kupitia katika risala yao, iliyosomwa na Sheikh Mkuu wa Dodoma, alisema serikali kama si juhudi kubwa zilizofanywa na waasisi wa taifa hili hali ya ustawi wa elimu uliopo leo usingefikiwa.

“Tumeshirikiana vema na taasisi za dini, naamini bila ushirikiano huo baadhi ya maeneo wasingepata huduma za afya, elimu, maji na miundombinu…napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kitu chochote ambacho serikali itatoa na kuwabagua wengine.

“Baada ya uhuru Mwalimu Nyerere alitaifisha shule hizo ili kuweka uwanja sawa kwa watoto wa rangi, dini na kabila zote kwa sababu zilikuwa za serikali.

“Ninyi kama mnataka jengeni shule na vyuo serikali itawasaidia kama inavyofanya kwenye shule na vyuo vya wenzetu Wakristo, shule za Azania na Kihindu…mfano ni mkopo unaotolewa na serikali kwa wanafunzi waliopo katika vyuo vya Wakristo.

Alisema wanaomcha Mungu ni watu wa upendo siku zote kwa sababu wanawahudumia vema wananchi wanaowahubiria amani na upendo, hali inayovipunguzia kazi ya kupambana na uhalifu vyombo vya dola.

Aidha, aliwataka Waislamu kuunda Mahakama ya Kadhi bila kuitegemea serikali huku akibainisha kwamba ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Profesa Ibrahim Juma, ambaye ni mtaalamu wa Sharia na Sheria za Kiislamu.

Alisema mahakama hiyo ya kadhi itakayoundwa haitahusika na kesi za jinai na kwamba haitakuwa na utaratibu wa kutoa hukumu kama zile za kukatwa mikono kwa wezi na za watu kupigwa mawe hadi kufa ambazo zimekuwa zikitumika katika mataifa yanayofuata Sheria za Kiislamu (Sharia).

Hata hivyo, aliwaomba viongozi wa dini kuacha kukashifiana na kubainisha kwamba njia bora ya kufikia malengo ya mafanikio ni kupitia meza ya mazungumzo huku akiwataka kutimiza wajibu wao bila woga wala kuoneana.

Aliwataka viongozi wa dini zote kurejesha utaratibu wa mazungumzo katika meza moja na kubainisha kwamba nguvu ya dola inatumika pale amani inapotoweka.

Aliipongeza BAKWATA kwa utaratibu bora wa kila mwaka kuwapeleka Makka Mahujaji na kuwatia moyo waendeleze utaratibu huo ili ifike mahali baraza hilo liwe chaguo la hiyari la mahujaji.

Kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya, aliwataka viongozi wa dini zote kuwahamasisha waamini wao kushiriki bila kuwepo kwa ushabiki wa kidini na kusema suala hilo linawezekana iwapo viongozi hao wataamua na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani.

Alitumia fursa hiyo kuwaonya waumini wa Kikristo na Kiislamu kutougeuza mjadala wa mabadiliko ya Katiba kuwa mdahalo au malumbano ya kutaka kuingiza masilahi ya dini hizo mbili ndani ya katiba.

Akizungumzia tatizo la dawa za kulevya, Rais Kikwete alisema tatizo hilo lipo kila mahali, hivyo serikali imejipanga kukabiliana nalo huku akiomba ushirikiano kwa viongozi wa dini ambao miongoni mwao wanahusika.

Akionyesha namna tatizo hilo linavyokua, alisema wafanyabiashara hao wameshaanza kuwalenga vijana wa vijijini, ambapo iwapo hatua za kudhibiti hali hii hazitachukuliwa, hasa na viongozi wa dini, basi tatizo litazidi kuongezeka na kukithiri.

“Ni tatizo la kweli, hakuna mji ulionusurika, sasa hivi wanakwenda kuwauzia vijana wa vijijini…kazi iliyo mbele yetu ni ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa dini na waumini wao.

Alitumia fursa hiyo kuwajibu viongozi wa dini akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakimtaka awataje hadharani viongozi wa dini aliosema wamekuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Akirejea kauli alizopata kuzitoa katika maeneo mawili tofauti ya Kanisa Katoliki, Rais Kikwete alisema alifanya hivyo kama njia ya kutoa rai na tahadhari baada ya kupata taarifa ambazo zimekuwa zikiwataja viongozi wa dini kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

“Nilisema hili kama tahadhari, tumewakamata masheikh, wachungaji, maalhaji. Mmoja alikuwa anakwenda Brazil akakamatwa na kesi ipo mahakamani. Sikusema maaskofu bali watumishi wa Mungu…maaskofu na viongozi wa dini, niliwaomba tushirikiane..Nikaona wengine wanachukia,” alisema Kikwete pasipo kutaja jina la kiongozi yeyote wa dini.

Alisema wito wake huo kwa viongozi wa dini haukuwa na lengo la kuwakejeli au kuwashutumu bali alifanya hivyo kutokana na kutambua namna walivyo na uwezo wa kuvuta hisia za watu wengi wanaohudhuria mahubiri yao.

“Sikuwakejeli wala sina sababu ya kuwakejeli viongozi wa dini, sasa hili mkiliona baya wenzangu mnanikatisha tamaa na ninyi mnasikilizwa kwa sababu mna uwezo wa kukusanya watu wengi, mkawahubiria wakawaelewa,” alisema.


Hisani ya Tanzania Daima.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.