Jiji la Manchester lina timu tatu ambazo ni Manchester United , Manchester City na FC United. Soka la England hivi sasa limehamia jiji la Manchester . Hii haimaanishi kuwa jiji hili limekuwa kimya , hapana kwani Manchester United miaka yote wamekuwa wakiipeperusha bendera ya jiji hili peke yao lakini sasa kuna mtu mwingine ameongezeka naye ni Manchester city .
City walianza kampeni yao ya kuijenga upya klabu yao na kuifanya kuwa moja ya vigogo vya soka nchini England na baadae ulaya kama misimu miwili iliyopita na kwa muda mfupi wameleta mapinduzi ya kweli . Hapo awali ilikuwa miujiza kuwakuta City wakisajili wachezaji bora kuli United, Arsenal , Chelsea , Liverpool na hata watu kama Tottenham . Lakini City leo hii wanamsajili Sergio Aguerro huku wakitishia kuinyima United nyota ambaye wamekuwa wakihangaika kumsajili muda mrefu Wesley Sneijder , kweli mambo yamebadilika.
Kwa muda mrefu mechi ya kufungua dimba msimu wa soka nchini England kiutamaduni ya Ngao ya Jamii ambayo hapo awali ilikuwa inafahamika kama Ngao ya hisani ilikuwa inagombaniwa na timu kama Chelsea na Man United au Arsenal na Liverpool, ni mara chache sana umekuta timu nyingine tofauti na hizi nne zikicheza mechi hii kama ilivyokuwa kwa Portsmouth miaka michache iliyopita walipofanikiwa kutwaa ubingwa wa FA na sasa Manchester city nao wameingia kwenye mchezo huu wakiwa mabingwa wa kombe la FA na wanakutana na mahasimu wao wakubwa Manchester United .
Manchester City wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa wamepania kudhihirisha kuwa wao si majirani wapiga kelele kwa Manchester United bali ni wapinzani wa ukweli ambao wanaweza kuwania si tu sifa za kuwafunga watani wao wa jadi bali kuwania ubingwa wa ligi kuu na ligi ya mabingwa .
Kikosi cha City kimeenea kila idara japo atakosekana mfungaji bora wa msimu uliopita Carlos Tevcez ambaye suala lake bado halijapata ufumbuzi. Lakini hii haitawapa City “majotroo” kwani mtu aliyekuwa anayemuweka Benchi Tevez kwenye timu ya taifa ya Argentina Sergio Kun Aguerro atakuwepo kuziba pengo lake japo anatazamiwa kuanzia benchi huku nyota wengine wapya wa City kina Gael Clichy na Stefan Savic wakitarajiwa kucheza pia.
Manchester City wanatarajiwa kuingia na kikosi kitakachotumia mfumo wa 4-3-3 na kikosi kinachotarajiwa kuanza ni hiki hapa:- Hart; Richards, Kompany, Lescott, Clichy; Milner, De Jong, Toure Yaya; Silva, Balotelli, Aguero.
Manchester United wao wamesajili kuliko timu zote nchini England , na walimaliza shughuli hiyo mapema wakimsajili kipa David De Gea , beki Phil Jones na kiungo Ashley Young huku wakiwa kwenye harakati za kumsajili Wesley Sneijder ambaye City pia wanamnyatia . Manchester United wanaingia kwenye mchezo huu kama bingwa mtetezi wa ngao ya jamii baada ya kuwafunga Chelsea kwenye mchezo wa msimu uliopita .
Mashabiki wa United hawatarajii kumuona Javier Hernandez ambaye aliumia kwenye mazoezi wakati United wakiwa kwenye maandalizi ya msimu japo Sir Alex Fergusson mwenyewe amesema kuwa hata kama angekuwa fiti asingecheza kwenye mchezo huu kwa kuwa angekuwa kwenye mapumziko baada ya kushiriki kwenye kombe la CONCACAF GOLD . Michael Carrick na beki Rafael wamepata majeraha madogo ambayo yatamaanisha kuwa hawatatumika kwenye mchezo huu.
Wachezaji wote waliosajiliwa wanatarajiwa kuonekana huku De Gea akianza mchezo wake wa pili nchini England , Phil Jones na Ashley Young wote wataonekana. Kikosi cha United kinatarajiwa kuwa kama hivi .
Manchester United (4-4-2): De Gea; Jones, Vidic, Ferdinand, Evra; Young, Jones, Anderson, Nani; Rooney, Berbatov.
Manchester City na Manchester United walikutana mara tatu msimu uliopita huku kila timu ikishinda mara moja na wakitoka sare mara moja pia .
Kwenye mchezo huu watani hawa wamewahi kukutana mara moja ambayo ilikuwa mwaka 1956 ambapo United walishinda kwa 1-0 , na mara nyingine pekee ambayo Man city walicheza kwenye mchezo huu ilikuwa dhidi ya Burnley mwaka 1973 ambapo walifungwa 1-0 .
Kwa upande wa Manchester United historia ya mchezo huu wa ngao ya jamii ( zamani ngao ya hisani) iko upande wao . United ndio timu iliyotwaa ngao hii mara nyingi kuliko timu zote wakifanya hivyo mara 18 na kwa miaka kumi ilyopita United wamecheza mara 6 kwenye pambano hili huku mchezo dhidi ya City jumapili ukiwa wa 7 na Ryan Giggs ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi za ngao akicheza mara 13 na akishinda mara 8 .
Je itakuwa City ambao wataendeleza kelele zao kama majirani wa United waliojiondoa kwenye kivuli au Man United watakaodhihirishia City kuwa wao ndio wafalme halisi wa jiji la Manchester ? Majibu yatapatikana kwenye uwanja wa Wembley.
Unono wote tembelea http://www.shaffih.blogspot.com/
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.