ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 22, 2011

TAMKO LA VIONGOZI WA DINI NA MADHEHEBU MBALIMBALI NCHINI LAFUKUNYUA MADHAIFU MENGI SEKTA YA MADINI.

Kamati ya viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali inayojishughulisha na masuala ya kijamii, kiuchumi haki na uhifadhi wa mazingira iliyoundwa kwa ajili ya kutetea haki za wananchi wanaoishi katika maeneo ambako serikali imewekeza katika sekta ya madini imeitaka serikali kuhakikisha kwamba shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo husika zinaendana na haki za binadamu. Kutoka kushoto ni Bishop Dr. Benson Bagonza (CCT), Arch Bishop Paul Ruzoka ambaye ni mwenyekiti na Sheik Salum Fereji BAKWATA.
Hayo yamesemwa Leo asubuhi na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo la Tabora Paul Ruzoka wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa hoteli ya G & G jijini Mwanza.

Amesema katika ziara ya kamati hiyo ambayo inajumuisha wajumbe kutoka Afrika ya Kusini, Botswana, Zambia, Canada na Norway iligundua mapungufu mbalimbali yanayofanywa na wawekezaji katika sekta hiyo ukiwemo uchafuzi wa mazingira, unyanyasasi wa wananchi, ukiukwaji wa haki za binadamu na matumizi ya sheria za ardhi na kutokuwepo kwa mpangilio mzuri wa ulipaji fidia.

Amesema kamati hiyo ilibaini kuwepo kwa baadhi ya wananchi na waathirika waliopisha shughuli za uchimbaji za mgodi wa madini ya dhahabu wa kampuni ya Geita Gold Mine hadi sasa hawajalipwa fidia baada ya kuondolewa katika makazi yao hadi sasa hawana makazi maalum ya kuishi wala hawajui nini hatma yao.

Askofu Luzoka amesema kwa upande wa Mgondi wa Nyamongo ulioko mkoani Mara, kamati hiyo imebaini kuwepo kwa uchafuzi mkubwa wa mazingira na wananchi ambao wanazunguka mgodi huo hawapati maji safi na salama licha ya uongozi wa mgodi huo kuweka magari ya matanki ya kusomba maji safi kwa ajili ya wananchi hao jambo ambalo waliitaka serikali kwa kushirikiana na uongozi wa mgodi huo kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Aidha kamati hiyo imetoa ushauri kwa serikali kupitia wakuu wa wilaya na mikoa ambapo migodi hiyo inapatikana kuhakikisha kuwa shughuli zinazofanywa na migodi hiyo haziathiri mazingira ya mahali husika, sheria iliyotungwa hivi karibuni ya fidia ya ardhi pia iwaguse wale ambao walihusika na zoezi la uhamishaji wananchi ili nao waweze kupata fidia pamoja na serikali kuhakikisha kuwa fidia wanaolipwa wananchi husika inawanufaisha wananchi kwa kujenga nyumba bora za kisasa.

Pia kamati hiyo imeyaomba mashirika ya kimataifa ambayo yanahusika na haki za binadamu kuhakikisha kuwa wananchi ambao wanaishi karibu na migodi wanahakikishiwa usalama wa afya, maisha na mali zao na kuhakikisha kuwa haki inatendeka.

Kamati hiyo inaundwa na wajumbe kutoka Baraza la Maaskofu wa katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT) na wajumbe wake ni kutoka nchi za Afrika Kusini, Botswana, Zambia, Canada na Norway.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.