ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, April 14, 2010

TAHARIRI: usimamizi thabiti utapunguza ajali za wachimbaji wadogo.


Tumepokea kwa masikitiko na mjonzi makubwa vifo vya wachimbaji madini wadogo wadogo 16 katika machimbo ya dhahabu yasiyo rasmi katika kijiji cha Sabola, kata ya Kasame, wilaya ya Geita, mkoani Mwanza.
Huu ni msiba mkubwa mwingine ndani ya mwezi mmoja kutokea ktk machimbo ya dhahabu kanda ya ziwa, ambapo wachimbaji wengine watatu walifunikwa na kifusi katika mgadi wa dhahabu Buzwagi, wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Hili ni tatizo na linakuwa tatizo kubwa zaidi pale wachimbaji wadogo wadogo ambao hawana mafunzo yoyote ya usalama ktk migodi wanapofikwa na ajali kama hizo, kwani msaada unakosekana hata ule wa huduma ya kwanza.
Inavyoonekana, wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu mbali ya kutokuwa na ujuzi wa masuala ya usalama migodini, hawana chama chao, kama kipo basi uongozi una mapungufu.
Nasema hivyo kwa sababu, siyo rahisi idadi kubwa ya wachimbaji madini ikaendesha shughuli zake bila kuwa na uongozi wa kuhakiki taratibu, kanuni na sheria za usalama kama zinazingatiwa kwenye maeneo hatari kama hayo.
Mazingira ya vifo vya wachimbaji hao katika shimo walimofia ni kwamba, mara baada ya taarifa kuenea kuwa shimo hilo lilikuwa likitoa dhahabu nyingi, wachimbaji walikimbilia humo kiasi kwamba hakuna aliyejali usalama wa mwenzake.
Ufumbuzi unatakikana haraka ili wakati mwingine hali kama hii isije jirudia, kwani suala zima la uchimbaji si baya kwa kuwa dhahabu ni madini yenye thamani kubwa ambayo yanaboresha maisha ya wachimbaji.
Hiyo ni rasilimali yao, ni mali ambayo Serikali kupitia Wizara inayohusika inapaswa kuwasaidia kwa mafunzo, uwezeshwaji katika kuunda vikundi vinavyoweza kuweka taratibu za jinsi ya kupata maeneo na uchimbaji kwa ujumla.
Yote haya yamekuja kutokana na kukosekana kwa taratibu za uchimbaji na kama zipo basi kutosimamiwa vilivyo na watendaji wake ndiko kumepelekea wachimbaji kujiendesha bila kuwepo mipaka ya uchimbaji.
Tunawapa pole wananchi wa kijiji cha Sabola, familia za wachimbaji waliopoteza maisha yao kwani Taifa limeondokewa na nguvu kazi muhimu katika ujenzi wake. Mungu azilaze mahala pema peponi Roho za marehemu wote. Amina.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.