Akizungumzia maandalizi kwa ujumla ya mchezo huo katika ofisi za makao makuu ya klabu jijini Dar es Salaam, Afisa habari wa Simba, Haji Manara amesema.
“Mechi ya kesho tumepunguza viingilio kwa bei ya kawaida sana ili kuwezesha umma wa watu kujaa, kwasababu mechi itachezwa jioni saa moja, kama tulivyofanya kwenye Simba Day au kama watu wa Namungo (Ruangwa), Arusha na juzi Mwanza walivyofanya. Tunataka tujae tena kesho”.
Manara amevitaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh 15,000 kwa VIP A, Sh 10,000 kwa VIP B, jukwaa la mzunguko ni Sh 3,000 pamoja na Sh 1,500 kwa watoto ambao watakuwa wametoka kwaajili ya kuja kufurahia siku kuu ya Eid al-Adha.
Pia amezungumzia kuhusu hali ya kikosi cha Simba kuelekea mchezo huo ambapo itawakosa mchezaji raia wa Zambia, Cletus Chama na Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao bado ITC zao hazijawasili TFF huku wachezaji wengine wakiwa katika hali nzuri wakiwemo John Bocco na Emmanuel Okwi aliyeumia katika mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Mtibwa Sugar.
Simba itaanza kampeni yake ya kutetea ubingwa kwa mchezo wa nyumbani, ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza wa ligi msimu uliopita dhidi ya Ruvu Shooting kwa kipigo cha mabao 7-0, mshambuliaji Emmanuel Okwi akifunga mabao manne.
Rekodi ya Simba katika michezo ya ufunguzi ya ligi kuu ni ya ushindi kwa takribani misimu 10 iliyopita tangu ilipopoteza mchezo wa ufunguzi msimu wa 2007/08 kwa kufungwa bao 1-0 na Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.