ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, August 27, 2012

MWANAHABARI AJITOSA KUWANIA UJUMBE NEC ILEMELA

Nashon Kennedy akirudisha fomu kuwania ujumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa wilaya ya ilemela kwa katibu wa ccm wilaya ya Ilemela Mhe. Daniel Ole Porokwa.

 Na. F.pluss
MCHAKATO wa kuwania nafasi za uongozi katika Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Ilemela umechukua sura mpya baada ya Mwandishi wa Habari Leo wa jijini Mwanza Nashon Kennedy kuchukua fomu mwishoni mwa wiki ya kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia wilaya hiyo.


 Akizungumza jana muda mfupi baada ya kuchukua fomu katika ofisi za chama wilaya,  alisema kuwa ameamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kama haki ya kikatiba kama mwana CCM lakini pia kushiriki kikamilifu katika kutoa mchango wake katika chama hasa kwa wakati huu ambao chama kimefanya mabadiliko makubwa ya kimfumo.

  “Nia yangu kama mwana CCM ni kushiriki katika kukisaidia chama hasa kuanzia ngazi ya mashina na matawi, ambako naamini ndiko kuna wanachama wengi waliko na kutokana na mabadiliko ya mfumo yaliyofanywa, naamini sasa chama kinahitaji nguvu mpya ya vijana ya kupambana na hoja kutoka upinzani”, alisema Kennedy na kuwataka wanachama wa CCM wilaya ya Ilemela wamuunge mkono kwa kumchagua ili aweze kutimiza azma yake ya kukitumikia chama.

  Alisema kutokana na mabadiliko ya kimfumo wa Chama makao makuu kubadilisha nafasi ya Ujumbe wa NEC kutoka mkoa hadi wilaya ni ishara njema ya kukirudisha chama kwa wananchi wa hali ya chini tofauti na siku za nyuma, jambo ambalo ni la kujivunia katika chama na hatua hiyo inahitaji viongozi makini wa kutekeleza ilani ya chama na kuwajibika kwa wanachama katika ngazi za matawi, shina na kata.

  “Ninaposema wananchi wa hali ya chini nina maana kuwa kwa sasa chama kimetoa fursa pana kwa mwanachama mwenye sifa na uwezo kutumia haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi na kuchaguliwa, na mimi naona sifa hizo ninazo”, aliongeza

  Alifafanua kuwa katika mabadiliko ya mfumo wa vyama vingi, CCM haina budi kuwachagua viongozi ambao wako tayari kukitumikia Chama Kwa manufaa ya chama  bila ya ubaguzi wa jinsia,dini ,rangi na matabaka.

  “Hivi sasa watu wanazungumza udini, ukabila na matabaka, mambo ya namna hii hayatufai katika chama na nikichaguliwa kwa kushirikiana na viongozi na wana CCM wenzangu nitahakikisha kuwa chama chetu hakiwi na sura hiyo”, alisema.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.