Vipiii? |
Kubadilishana mawazo.... |
Washindi wa Airtel ‘Mimi Ni Bingwa’ wakwea pipa kwenda Old Trafford
Na Mwandishi Wetu
WASHINDI wa tiketi wa awamu ya kwanza ya promosheni ya Airtel Mimi ni Bingwa jana waliondoka nchini kwa safari iliyogharamiwa kila kitu kwenda Old Trafford.
Wakisindikizwa na Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando, washindi na wenza wao waliowachagua watakuwa na nafasi ya kuangalia mechi baina ya Manchester United na Cardiff City moja kwa moja ‘live’ itakayochezwa Jumanne saa 12 jioni majira ya Afrika Mashariki.
Awamu ya kwanza inayowajumuisha Leonard Dickson Lyatuu kutoka Arusha, Andrew Muta Temwa mkazi wa Bukoba, Ashraf Mohamed Adam kutoka Tanga na Salma Farid Mugheiry kutoka Dar es Salaam na wenza wao, pia watapata nafasi ya kufanya ziara katika uwanja wa Old Trafford na kuzungumza na wachezaji wa Manchester United.
Washindi hawa hawakusita kuelezea furaha yao na hamu ya kukutana na wachezaji maarufu wa kimataifa wa mpira wa miguu pamoja na hari ya kuwa sehemu ya mashabiki katika uwanja huo maarufu duniani wakati wa moja ya mechi za ligi kuu ya Uingereza inayoangaliwa zaidi duniani.
“Hii ni nafasi ambayo sikuwahi kuiota katika maisha yangu. Kutokana na hali yangu ya kiuchumi, sikuwahi kufikiria kuwa siku moja nitasafiri kwenda Uingereza na hususani kuingia katika uwanja wa Old Trafford. Nina furaha sana. Naishukuru Airtel kwa kunipa nafasi hii, ambayo pia imenisaidia kuonyesha upendo kwa mwenza wangu kwa kumpa nayeye nafasi ya kwenda Uingereza,” alisema Lyatuu.
Salma, ambaye ni mshindi kutoka Dar es Salaam alisema, “Hii ni kama ndoto ambayo imekuja kutokea kweli. Nilipotaarifiwa kuwa nimeshinda tiketi mbili kwenda Old Trafford, sikuamini hadi nilipokamata tiketi yangu mkononi. Nataka niwahakikishie wananchi na wateja wa Airtel kuwa promosheni hii ni ya kweli na inaweza kukupa fursa ambayo kamwe hukuwa ukihitarajia.”
Akidokeza kuhusiana na safari hiyo, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando, alisema kampuni hiyo ya simu itagharamia safari yote, chakula pamoja na gharama za malazi hadi washindi hao watakaporejeshwa makwao.
“Bado kuna safari nyingi zaidi zinakuja. Mpaka sasa, tunaandaa baadhi ya hati za kusafiria za washindi wengine waliojishindia tiketi za promosheni ya Airtel Mimi ni Bingwa kwenda Old Trafford na zikiwa tayari, wataondoka mapema. Promosheni bado inaendelea lakini muda umebaki mchache kabla ya kuchezesha droo ya kumpata mshindi wa shilingi milioni 50. Wakati wa kushiriki ndo sasa.
“Mbali na tiketi, bado kuna zawadi nyingi zaidi kushindaniwa kila siku na kila wiki, ikiwa ni pamoja na zawadi kubwa ya shilingi milioni 50 mwishoni mwa droo. Kila mshiriki wa promosheni ya Airtel Mimi ni Bingwa ana nafasi ya kushinda zawadi hizi. Unachohitaji ni kutuma ujumbe mfupi (SMS) wenye neno “BNGWA” kwenda namba 15656, kwa kujibu maswali mengi iwezekanavyo,” alisema.
Bw. Mmbando alisema safari hiyo itachukua siku tano ikiwa ni pamoja na siku za safarini na washindi wanatarajiwa kurudi nchini ifikapo Alhamis ya tarehe 30 mwezi huu.
Washindi hao watakaoelekea Old Trafford toka promosheni ilipoanza mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana ni pamoja na Edwin Edmund Kajimbo kutoka Iringa, Michael Joseph Shirima kutoka Kinondoni jijini Dar es Salaam, Shaibu Rashid Dege, Mtendaji wa Kijiji cha Nang’olo wilayani Kilwa mkoani - Lindi, Leonard Dickson Lyatuu kutoka Arusha, Joseph Steven Mambo kutoka Kawe jijini Dar es Salaam, Emmanuel Mahenge Jacob kutoka Njiro mkoani Arusha, Rashid Jacob Kagombola kutoka Bukoba mkoani Kagera, Harrison Wilson Mwambogolo kutoka Kigogo jijini Dar es Salaam na Salma Farid Mugheiry kutoka Dar es Salaam.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.