Sehemu ya msaada toka Mega Trade Investiment Limited. |
KAMPUNI ya utengenezaji pombe za vinywaji vikali ya Mega Trade Investiment Ltd ya Arusha kupitia tawi lake la jijini Mwanza, imetoa misaada ya chakula na nyenzo za usafi kwa kituo cha malezi ya wazee kilichopo Bukumbi wilayani Misungwi nje kidogo ya jiji la Mwanza, ikiwa ni utaratibu wa kampuni hiyo unaofanyika kila mwaka kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii hasa iliyo na changamoto za kuishi mazingira magumu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni moja na laki tatu Meneja wa Mauzo wa Mega Trade Investiment Limited tawi la Mwanza James Njuu alisema kuwa kampuni yake imeamua kuchukua hatua hiyo lengo likiwa ni kuwafariji wazee hao ambao jamii ya watanzania imewasahau.
Njuu aliongeza kuwa watanzania wanatakiwa kubadilika sasa na kuwajali wazee hao wanaoishi kwenye kambi ya pamoja kutokana na eidha kutelekezwa na familia zao au kuporomoka kimaisha hali iliyowasababisha kukimbilia kituoni hapo ili kupata msaada.
Amewataka wananchi kutenga muda wao kukaa na kuzisikiliza changamoto za wazee hao ikiwa ni pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali ili wasijione kuwa ni wapweke na watu walio telekezwa.
"Serikali yetu bado inachangamoto nyingi za kukuza uchumi na vipato vya wananchi wake na wakati huo huo inakabiliwa na ujenzi wa miundombinu, sasa tukiitegemea pekee ijikite kuwahudumia watu hawa na kituo hiki tutasubiri sana, hili ni jukumu letu kwani pamoja tunaweza" Alisema James Njuu.
Aidha aliongeza kuwa ni vyema jamii ikajenga utamaduni wa kuwatembelea kila mara na kuwasaidia wazee hao na isiishie misimu ya kipindi cha sikukuu tu kwani wanamahitaji ya chakula kila cha kila siku.
Licha ya msaada huo kituo hicho cha kulea wazee cha Bukumbi kilichopo nje kidogo ya jiji la Mwanza bado kinakabiliwa na changamoto za miundombinu ya mahala pa kulala, huduma za maji na umeme zimesitishwa kutokana na deni la muda mrefu pamoja na changamoto ya vitendea usafi kwa mazingira ya kituo.
Changamoto ya ukosefu wa chakula na huduma nyingine muhimu zimesababisha baadhi ya wazee wa kituo hicho ambao wengi ni walemavu, wasioona, walemavu wa ngozi pamoja na wakoma kutoroka kambini hapo na kwenda kuombaomba mitaani ili kupata fedha za mahitaji muhimu.
Nayo changamoto ya kukosa elimu ya jinsia, kujitambua pamoja na ufahamu wa magonjwa ambukizi imesababisha wazee hao kuzaliana bila mpango huku wengine wakifikia hatua ya kupata wajukuu kambini hapo hali inayo sababisha kituo kushindwa kutoa huduma stahiki.
Jumla ya wazee 137 wanaishi kambini hapo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.