ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, January 15, 2013

MKUU WA WILAYA YA MAGU AKIPONGEZA KIWANDA CHA ALPHA CHOICE KWA KUFADHILI MAFUNZO KWA WAFUGAJI WA KATA YA KAHANGARA.

Meneja wa Kiwanda cha Alpha Choice Bw.Gaurav  Goel  akitoa ufafanuzi juu ya uendeshaji wa kiwanda hicho kupitia kitengo cha uzalishaji kwa mkuu wa wilaya ya Magu Bi. Jacline Liana (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi.Naomi Nnko (katikati) wakati walipo tembelea kiwanda hicho.

MKUU wa Wilaya ya Magu Bi.Jackiline Liana ameupongeza uongozi wa Kiwanda cha Kusindika nyama cha Kampuni ya Alpha Choice kwa ufadhili wao na kuwawezesha  wafugaji kupatiwa mafunzo ya elimu ya ufugaji wa kisasa ili kuondokana na ufugaji wa kizamani.

Akizungumza na wafugaji 50 waliopatiwa mafunzo na wataalamu wa Ugani wa Idara ya Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya wafugaji hao kutoka vijiji vitatu vya Bugabu na Kahangara vya Kata ya Kahangara na kijiji cha Ilungu cha Kata ya Nyigogo vya Wilayani humo baada ya mafunzo hayo kufadhiliwa na Kiwanda cha Alpha Choice.

Bi Liana alisema kwamba Mwekezaji wa Kiwanda cha kusindika nyama ameonyesha ushirikiano wa dhati na uongozi wa Wilaya,Halmashauri ya Magu na kuwajali wafugaji kwa kuzingatia ujirani mwema ambao utajenga mahusiano na Kiwanda cha Alpha Choice na kuwawezesha pia wafugaji hao kutumia mafunzo waliyopata kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri kufuga kisasa zaidi ili kuendana na Ufugaji bora na kuwawezesha kujiongezea kipato zaidi.

Aliongeza kuwa lengo la wafugaji hao kupatiwa mafunzo na elimu ni kuwasaidia kwenda kufuga kwa tija na kuachana na ufugaji wa mazoea (zamani) ambao umekuwa ukiwarudisha nyuma wafugaji na kuwapotezea mifugo yao kwa kukumbwa na maradhi ikiwemo kupata bei ndogo kutokana na mifugo yao kukosa uzito unaochangiwa na lishe duni.

Ndani kwenye uzalishaji.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kwamba lengo kubwa la serikali ni kuhakikisha watu binafisi,Taasisi mbalimbali,Kampuni na Mashirika yaliyopo nchi yanashiriki kuwaletea wananchi maendeleo na kutoa huduma bora kwa kuzingatia maeneo yaliyo wekezwa na kuwanufaisha wananchi na mwekezaji ili uchumi wa taifa uweze kuongezeka na pato la mwananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi.Naomi Nnko alisema kwamba mwekezaji huyo Alpha Choice, atasaidia kupatikana kwa ajira wananchi wa maeneo ya jirani na kiwanda hicho na kuchangia mapato ya halmashauri kutokana na biashara ya mifugo huku pia wafuaji wakinufaika na kuuza mifugo yao kwenye soko la kiwanda hicho ambalo litakuwa la uhakika kinyume na kusafirisha mifugo umbali mrefu kutafuta soko.

Bi.Nnko alieleza kwamba kuwepo kwa Kiwanda cha Alpha Choice kitasaidia wananchi kupata ajira na kuongeza mapato ya Halmashauri kufatia biashara itakayokuwa inafanyika kati ya wafugaji na kiwanda hicho huku pia wananchi wa maeneo ya jirani wakipata huduma za maji ambazo kiwanda hicho kimekuwa kikisaidia kuwekwa kwenye huduma za kijamii kama vile zahanati na nyumba za ibada.



Kiwamda cha Alpha Choice  kimekuwa mwekezaji wa kwanza kufadhili mafunzo ya garama kwa wafugaji hao kutoka vijiji vitatu jambo ambalo Mkurugenzi wake katika taarifa yake wakati wa ufunguzi wa Warsha hiyo,alidai kuwa anatimiza ahadi yake ya kushirikiana na wafugaji ,Serikali na Halmashauri baada ya kuamua kuwekeza ili kuwaongezea maarifa zaidi wafugaji,kuchangia uchumi wa Taifa na kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Magu kuongeza vyanzo vya Mapato huku pia akipanua wigo wa ajira kwa wananchi ili kuondokana na tatizo la ajira na umasikini wa kipato kwao.

Nae Meneja wa Kiwanda cha Alpha Choice Bw.Gaurav  Goel alisema kwamba lengo la kufadhili mafunzo hayo ni kutaka wafugaji kuwa na elimu ya kufuga kisasa na kuwawezesha pia kuwa na mifugo ambayo wakiamua kuuza kwenye soko la kiwanda hicho ikidhi ubora unaotakiwa wa kuanzia kilo 250 hadi zaidi kilo 500 kwa Ng’ombe mmoja ambapo bei ya soko itamkomboa mfugaji na muuzaji .

Meneja huyo pia amewataka wafugaji kuendelea kukipatia ushirikiano kiwanda hicho kwa kuhakikisha wanapeleka kuuza mifugo yao kwenye soko la kiwanda chake ili kiweze kuendelea na uzalishaji na kuhimili ushindani wa soko la ndani na nje la bidhaa na kuondoa tatizo la wafugaji kutembea umbali mrefu kutafuta soko la kuuzia mifugo yao.

Bw.Goel amewataka wafugaji waliopatiwa mafunzo yao kwa ufadhili wa kiwanda cha Alpha Choice kutumia vizuri elimu hiyo na kufuga kisasa ili kuwanufaisha kwa kupata kipato kikubwa na kuinua uchumi wao huku  kiwanda hicho pia kukiwezesha kuongezea uzalishaji na kupata masoko mazuri kutokana na bidhaa bora watakazo sindika baada kupata malighafi yenye ubora unaotakiwa .


Mkuu wa wilaya ya Magu Bi. Jacline Liana, Afisa Mifugo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi.Naomi Nnko wakipata maelezo kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho kitengo cha ukataji nyama vipande vipande kwaajili ya kuhifadhiwa kwenye mifuko maalum ya plastiki, wakati walipo tembelea kiwanda hicho.

Uchakataji ukiendelea na wakati huo huo mkuu wa wilaya ya Magu Bi. Jacline Liana pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi.Naomi Nnko wakiendelea kushuhudia yanayojiri wakati walipo tembelea kiwanda hicho.


Hapo vipi? ninapogeuka kuwa mfanyakazi wa Kiwanda cha Alpha Choice kilichopo Kahangara wilayani Magu mkoani Mwanza.


Sasa ni wakati wa ufungaji bidhaa hatua ya mwisho ambapo kabla ya ufungaji hupimwa kisha kufungwa tayari kuingia sokoni. 


Bidhaa ambazo tayari ziko sokoni toka Alpha Choice ni pamoja na soseji, nyama za kawaida kwa vipimo vya kilo mbalimbali pamoja na kadhalika.


Soseji za Alpha Choice.


Nyam iliyo tayari sokoni huwa ni kwa style ya ukataji tofauti tofauti, kuna ile ya vipande kwaajili ya mboga kawaida au hii ya kamba kamba. 

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.