WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amepokelewa kwa mabango na nyimbo za kudai huduma ya maji, Jimbo la Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Kero nyingine aliyokumbana nayo ni, huduma mbovu za afya kwa baadhi ya maeneo, dhuruma za ardhi na wanafunzi kukaa chini darasani.
Aidha, Waziri Mkuu alimuweka kitimoto Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwimba, Pendo Malebeja, kwa kushindwa kusimamia vema matumizi ya fedha za miradi.
"Maji, maji, maji, maji." walisikika wananchi wakiimba kwa sauti ya juu, wakati Waziri Mkuu Majaliwa, alipowasili Kijiji cha Igumangobo katika ziara yake wilaya hapa.
Aidha baadhi ya wananchi walimuonesha mabango mbalimbali kiongozi huyo, wakilalamikia kukosa maji.
"Mheshimiwa Waziri Mkuu ahsante umekuja. Tatizo kubwa ni maji. Maji, maji. Tusaidie maji.
"Mbunge wetu Mansoor (Hanif) katusaidia mambo mengi, tunampongeza sana. Mbunge mchapakazi, tuleteeni maji." Yalisomeka baadhi ya mabango hayo, yaliyotolewa mbele ya kiongozi huyo.
Awali Mbunge wa Jimbo la Kwimba, Shanif Mansoor, alimueleza Waziri Mkuu kuwa mradi wa maji Kijiji cha Shilima, mradi umekwama tangu 2013.
"Tatizo kubwa hapa mheshimiwa Waziri Mkuu ni maji. Miaka minne, mitano tunasubili maji.
"Tunababaishwa, tunababaishwa tu. Kwenye mradi wa maji wa Shilima mpaka mabomba yameoza, mradi umekwama," alisema Mbunge Mansoora.
Kufuatia hali hiyo, Majaliwa akizungumza na wananchi Kijiji cha Igumangobo, alilazimika kumuweka kitimoto Mhandisi wa Maji wilayani hapa, Pius Boaz, akitaka majibu ya kero hiyo.
Alisema licha ya Serikali kutiririsha fedha za miradi ya maendeleo nchini, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imekuwa shimo la fedha za umma.
"Yaani kila miradi ya maji tunayoiletea fedha hapa Kwimba haikamiliki. Kwa nini?
"Ipo miradi ya mwaka 2013, 2014 na 2016 fedha zimeletwa, miradi haiishi na fedha hazijulikani zipo wapi," alisema Waziri Mkuu huku baadhi ya wananchi wakisikika wakimuomba aondoke na watendaji wa halmashauri.
Awali, Mhandisi wa maji Wilaya ya Kwimba, Pius Boaz, wakati akihojiwa na Waziri Mkuu juu ya miradi ya maji kukwama, alijikuta akimuita kiongozi huyo 'Mwenyekiti.'
Akijibu suala hilo la maji, Boaz alikiri mradi wa Shilima kusimama kutokana na mabomba ya mradi yapo chini ya kiwango.
"Mheshimiwa mwenyekiti (kicheko)," alisema Mhandisi Boaz, huku Majaliwa akisema 'mimi siyo mwenyekiti.
Akiwa Ngudu mjini, Waziri Mkuu alionekana kuchukizwa na usimamizi mdogo wa fedha za miradi ya maendeleo, unaofanywa na Mkurugenzi Malebeja.
Hata hivyo, Mkurugenzi Malebeja alipoulizwa na Majaliwa fedha zilizotumika kujenga zahanati ya Hungumalwa, alisema hajui kauli aliyoirudia pia kwenye kikao cha ndani.
"Kipindi chako Mkurugenzi (Pendo Malebeja) umekuwa ukipata hati chafu, hati chafu, chafu tu.
"Halmashauri ya Kwimba imekuwa shimo la fedha za Serikali. Sasa mkurugenzi nitakuletea mrejesho.
"Kuna mchwa, fedha za miradi tunaleta miradi haikamiliki na fedha hazionekani. Sasa Mkurugenzi nitakuletea ," alisema Majaliwa akionekana kukerwa na matumizi mabaya ya fedha kwa halmashauri hiyo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.