Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza
wasiwasi wake kuhusu kushamiri vita vya maneno kati ya Marekani na Korea
Kaskazini na kusema kuwa, kuna haja ya pande mbili hizo kukumbatia
diplomasia.
Antonio Guterres amesema taharuki katika Peninsula ya Korea
imetanda kwa kiasi kikubwa, ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika miongo
ya hivi karibuni na hivi sasa kuna haja viongozi wa Washington na
Pyongyang wakomeshe vita vya kisaikolojia.Katibu Mkuu wa UN amesema dunia inafaa kujifunza kwa kudurusu historia ili isijikute inakariri makosa yaliyopelekea kutokea vita vya Korea miaka 67 iliyopita, ambapo watu zaidi ya milioni 3 waliuawa.
Mgogoro kati ya Marekani na Korea Kaskazini ulishtadi baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutoa vitisho vikali hivi karibuni kwa kusema kuwa, Pyongyang itashuhudia moto na hasira ambazo hazijawahi kushuhudiwa na walimwengu, ikiwa ni radiamali kwa kauli ya Korea Kaskazini kuwa itashambulia kisiwa cha Guam.
Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini.
Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini amesema kuwa, sharti la
kusitishwa mashambulizi ya makombora dhidi ya kisiwa cha Guam cha
Marekani, ni Washington kuhitimisha mivutano katika Peninsula ya Korea.
Sambamba kutoa sharti hilo kwa Washington, Kim Jong-un amesema kuwa, ikiwa nchi hiyo itaendelea na harakati zake za uhasama katika Peninsula ya Korea, basi Pyongyang haitabadilisha msimamo wake wa kukishambulia kisiwa cha Guam wakati wowote.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.