ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, November 15, 2015

LOWASSA AJIANDAA KUTOA SIRI NZITO.

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa. 
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI.
Arusha/Dar. Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana hakuhudhuria mkutano wa kampeni za ubunge mjini Arusha kwa maelezo kuwa anajiandaa kutoa tamko kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar.
Maelfu ya wafuasi wa Chadema jana walifurika kwenye Uwanja wa Ngarenaro mjini hapa kuhudhuria kampeni za ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini ambao uliahirishwa kutokana na kifo cha mgombea kutoka chama cha ACT Wazalendo, lakini wakakumbana na tangazo kuwa Lowassa hataweza kuhutubia na badala yake atakuja siku ya kufunga kampeni hizo.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia(NCCR- Mageuzi) naye alisema kuwa Lowassa yupo katika maandalizi ya kikao cha leo kutangaza hatma ya uchaguzi mkuu uliopita.
“Tulikuwa tumepanga Lowassa aje katika mkutano huu, lakini kutokana na kufanya maandalizi muhimu ya mkutano na waandishi wa habari kesho saa 5:00 asubuhi, ameshindwa kuja” alisema James Mbatia, mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NLD na NCCR Mageuzi.
“Lowassa atakuja siku ya kufunga kampeni za ubunge katika Jimbo la Arusha hivyo tunaomba radhi,” alisema Mbatia, ambaye pia ni mbunge mteule wa Jimbo la Vunjo na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Lowassa, ambaye juzi alikuwa na mazungumzo ya saa moja na nusu na mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif, anatarajiwa kutoa tamko kuhusu hali ya kisiasa visiwani humo ambayo imekuwa tete baada ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo.
“Mheshimiwa anaandaa mambo muhimu atakayozungumza kesho,” alisema Aboubakar Liongo, msaidizi wa Lowassa alipoulizwa kuhusu waziri huyo mkuu wa zamani jana mchana.
Liongo alisema, mbali na suala la Zanzibar, Lowassa pia ataeleza msimamo wake kuhusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, ambao yeye na chama chake cha Chadema wanaamini kuwa matokeo ya kura za urais yaliyokuwa yanatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni tofauti na waliyokuwa nayo.
Tayari Lowassa ameshaeleza kuwa kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka huu ni mwanzo wa awamu ya pili ya safari yake ya kuelekea Ikulu, akiwataka wanaomuunga mkono kutokata tama.
“Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini huwezi kuiondoa,” alisema Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07.
Kwenye mkutano wa kampeni mjini Arusha, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdalah Safari alisema Lowassa pia atazungumzia tamko la polisi la kuzuia mikutano ya Ukawa na maandamano licha ya kuwa hiyo ni haki yao.
Ukawa ndoto
Kaimu mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima alisema kwenye mkutano huo kuwa Ukawa haitakubali uchaguzi kurejewa kwa kuwa Maalim Self alishinda.
Alisema kinachoondelea Zanzibar sasa ni kuua uchumi wa nchi kwani, mambo mengi yamesimama, watalii wamegoma kwenda Zanzibar na serikali inashindwa kutambua kuwa dunia nzima inajua kilichotokea.
Simanzi mkutano Arusha
Jana kwenye Uwanja wa Ngarenaro, vilio na simanzi ya kifo cha mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alfonce Mawazo vilitawala mkutano huo, huku mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema  akishindwa kuomba kura  na kuishia kulia.
Hata hivyo, aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kulia na badala yake wajiandae kuchukua hatua kwa kuwa ameuawa Mawazo na mwingine anafuatia kwa kuwa ana taarifa za kupangwa kwa mpango huo.
Mawazo, ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Lema, alikuwa mmoja wa wanasiasa maarufu jijini Arusha. Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Bondeni inayomilikiwa na Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) na baadaye aligombea udiwani wa kata ya Sombetini na kushinda.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa na mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Aman Golugwa.
Akizungumzia kifo hicho, Mbatia alisema wote wanaoendelea kuhusika na mauaji, hata kama ni viongozi wa juu serikalini au wastaafu, watafikishwa Mahakama za Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kuwa hakuna kitu chenye thamani kama uhai wa mtu.
Imeandikwa na Mussa Juma, Moses Mashalla na Fidelis Butahe

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.