PPF YASAIDIA SHULE VITABU VYA KIADA NA ZIADA
Na Baltazar Mashaka,MAGU
MFUKO wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, umetoa msaada wa vitabu vya masomo mbalimbali,kwa shule ya Sekondari Mwamanga,Katani humo Wilaya ya Magu,Mwanza.
Vitabu hivyo vyenye thamani ya sh.2 milioni,vilikabidhiwa jana kwa Mkuu wa shule hiyo, Oscar Deogratius na Meneja wa Mfuko wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshach Bandawe na kushuhudiwa na baadhi ya walimu, wanafunzi na watumishi wa mfuko huo.
Bandawe alisema, vitabu hivyo vitasaidia kukuza uelewa wa wanafunzi hasa wa masomo ya sayansi ambayo kwa kipindi kirefu sasa, baadhi ya wanafunzi wanakwepa kuyasoma kwa sababu ya ukosefu wa vitabu vya masomo hayo.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu kuwa urithi pekee kwa vizazi vyetu,mfuko umekuwa ukisaidiana na serikali kutatua changamoto za elimu, kuhakikisha kizazi cha sasa kinanufaika na huduma zinazotolewa na PPF.
“PPF tunaongozwa na sera, kushiriki masuala ya kijamii katika sekta ya afya na elimu.Pamoja na kulipa mafao ya wanachama wetu,fao la elimu na ujenzi wa Vyuo Vikuu kama Dodoma na Nelson Mandela cha Arusha, wanaofaidika ni watoto wa wanachama wetu na wasio wa wanachama.Ni wajibu wetu kuisaidia serikali kuhakikisha taifa linakuwa na vijana walioelimika,”alisema Bandawe
Alisema watoto hao wakipata elimu na kuingia kwenye soko la ajira, watasaidia kukuza uchumi wetu ikiwa ni pamoja na kujiunga na mfuko huu na kuufanya uwe endelevu kwa vizazi vijavyo.
Msaada huo wa vitabu unahusisha masomo ya Hisabati, Kemia, Bailolojia,Jiografia,Fizikia, Kiswahili, Kiingereza na Uraia vyote vikiwa vya mtaala mpya.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo ya sekondari Mwamanga,Deogratius, alisema msaada huo wa vitabu umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya wanafunzi sita kuchangia kitabu kimoja.
Alisema vitabu hivyo vitachechemua ari na morali ya wanafunzi kujifunza, tofauti na hapo awali na kuahidi watavitumia vizuri kufundisha na kujifunzia wanafunzi ili kuwajenga vizuri kitaaluma, hatimaye waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Aidha akitoa shukurani kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo, mwanafunzi wa kidato cha tatu, Philipo Bukesi aliupongeza mfuko wa PPF kwa msaada huo na kuomba mashirika na makampuni mengne kuiga mfano huo,katika kuboresha elimu nchini na sasa kitabu kimoja kitatumiwa na wanafunzi wawili badala ya sita.
Mwingne ni Veronica Sylvester waa kidato cha tatu pia,alisema walikuwa wakipata shida ya kujifunza masomo ya sayansi na kuazimika kusoma kwa makundi kutookana na uhaba wa vitabu,lakini sasa hali hiyo itapungua.Shule hiyo ina wanafunzi 514.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.