ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, October 17, 2017

UPINZANI KENYA WASIMAMISHA MAANDAMANO, RUTO AMTAKA ODINGA ASHIRIKI UCHAGUZI.

Upinzani Kenya wasimamisha maandamano, Ruto amtaka Odinga ashiriki uchaguziMuungano wa upinzani nchini Kenya NASA umetangaza kusimamisha maandamano ya kushinikiza marekebisho kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuelekea uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

Katika taarifa, kinara wa muungano huo Raila Odinga amesema wamefikia uamuzi huo kufuatia mauaji ya makumi ya wafuasi wao katika maandamano hayo. Anadai kuwa waandamanaji hao wa upinzani waliuawa na maafisa wa polisi waliopata maagizo kutoka kwa Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang'i na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Joseph Boinnet.

Hapo jana, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yalisema polisi ya Kenya iliua watu wasiopungua 50 katika maandamano ya upinzani ya kushinikiza mabadiliko kwenye IEBC katika maeneo yanayoaminika kuwa ngome za upinzani jijini Nairobi kati ya Agosti 9 na 13.
Raila Odinga, kiongozi wa upinzani Kenya.
Odinga amesema Ijumaa ijayo, wakati ambapo taifa hilo litakuwa linaadhimisha Siku ya Mashujaa, watatoa mwelekeo wa hatua watakazochukua kuhusu mustakabali wa muungano huo katika siasa za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
 
Huku hayo yakiarifiwa, Naibu wa Rais wa Kenya, William Ruto amesema chama tawala cha Jubilee kingependa sana Odinga ashiriki katika uchaguzi huo wa marudio ili kuimarisha hadhi na uhalali wa uchaguzi huo.

Amesema kinara huyo wa NASA alijiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa kuwa anaogopa kudhalilishwa atakaposhindwa.
Rais Uhuru Kenyatta (Kulia) na Naibu wake William Ruto.
Viongozi wa upinzani nchini Kenya wamekuwa wakisisitiza kuwa katu hawatoshiriki uchaguzi huo iwapo masharti waliyoyatoa hayatatekelezwa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa ofisini Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Ezra Chiloba na maafisa wengine wa tume hiyo ya uchaguzi wanaodaiwa kuhusu katika uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.