Na PETER FABIAN, KALIUA.
MGOMBEA Ubunge Jimbo jipya la Ulyankulu Mkoa wa Tabora kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Kadutu amejinadi na kuahidi kumaliza kero ya maji safi, ujenzi wa vyumba vya madarasa sekondari na shule za msingi , nyumba za walimu na zahanati kwa kila kijiji pamoja na miundombinu ya barabara katika Kata ya Seleli.
Kadutu alisema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiwahutubia wanasnchi kwenye mikutano ya kampeni ya Chama hicho jana katika Kata za Seleli na Kona nne za jimboni humo ambapo aliwaomba wamchague ili awe Mbunge wa Jimbo hilo aweze kuwatumikia kwa vitendo kama alivyokwisha kuanza akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua kabla ya kuwa Jimbo la Ulyankulu.
Awali akiwa katika Kata ya Seleli alizitaja kero na ahadi zake atakazo anzanazo endapo atachaguliwa kuwa Mbunge kuwa ni pamoja na kuchimba visima virefu na vifupi kukabiliana na tatizo la maji safi katika vijiji sita katani humo, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Bulela na Sekondari ya Kata Seleli, nyumba za walimu, ukamilishaji nyumba ya Mkunga katika Zahanati ya Nyasa na Ofisi ya Kata.
“Mkinichagua mtakuwa mmenipa heshima kubwa ya kuwatumikia kwa vitendo kwa kipindi cha miaka mitano ambapo nawaahidi kushughulikia uboreshaji wa miundombinu ya barabara za vijiji na barabara kuu ya Mji wa Ulyankulu-Kahama ili ijengwe na serikali kwa kiwango cha lami, kupigania soko la zao la tumbaku liwe la uhakika na bei yenye tija kwa wakulima,”alisema.
Kadutu akiwa Kata ya Kona nne aliwaomba wananchi kati vijiji vitano kwenye mikutano ya kujinadi kumchagua, kumchagualia madiwani wa CCM na mgombea Dk John Magufuli kuwa Rais wa awamu ya tano ili kuwezesha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2015/2020 ambapo imelenga kushughulikia mambo mengi ya maendeleo na utolewaji huduma bora za kijamii.
“Nitahakisha fedha za Mfuko wa Jimbo la Ulyankulu zinachochea maendeleo katika maeneo yenye changamoto za upatikanaji huduma za kijamii na maendeleo katika Sekta za Afya, Elimu, Maji safi, Miundombinu ya barabara, Mawasiliano ya simu na mitandao, Michezo, Kilimo, Ufugaji na Ujasiliamali pamoja kukamilisha vipaumbele vya masoko ya mazao ya chakula na biashara,”alisisitiza.
Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Neema Adam, aliwaomba wananchi kwenye mikutano hiyo kutofanya makosa na kuwachagua wagombea wa vyama vya upinzani ambao hawajui hata Jiografia ya jimbo hilo lakini pia wamekuwa wakifanya mikutano ya kampeni na kutumia muda mwingi kutoa lugha zisizokuwa za kistaarabu ikiwa ni pamoja na kutukana.
“Wananchi watu wa aina hiyo wanakuja kwenu na kushindwa kunadi sera na ilani za vyama vyao na jinsi watakavyowatumikia msiwape nafasi ya kuwachagua kwa kuwa watatumia muda mrefu kujinufaisha kwanza badala ya kufikisha hoja na matatizo yenu kwa serikali ili zifanyiwe kazi hivyo ni vyema mkachagua wagombea wa CCM kuanzia Dk Magufuli (Rais), Kadutu (Ubunge) na Madiwani wote,”alisema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.