Visa takriban 700 milioni vya maambukizi ya malaria vimezuiwa Afrika kutokana na juhudi za pamoja za kukabiliana na ugonjwa huo tangu 2000, utafiti umeonyesha.
Matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa katika jarida la Nature yanaonyesha jumla ya viwango vya maambukizi ilishuka kwa asilimia 50 kote barani.
Vyandarua vya kutumiwa vitandani kujikinga dhidi ya mbu vilichangia zaidi kupungua huku kwa maambukizi.
Kumekuwa na wito wa kuendeleza ufadhili unaosaidia kutolewa kwa vyandarua vya kujikinga mbu kuhakikisha mafanikio haya yanaendelea.
Hayo yakijiri, ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na shirika la umoja wa mataifa la Unicef inasema vifo vinavyotokana na malaria vimeshuka kwa asilimia 60 duniani tangu 2000 na maisha ya watu Zaidi ya milioni sita yameokolewa.
Ripoti hiyo inasema mataifa 13 yaliyokuwa na visa vya malaria 2000 hayakuwa na visa vyovyote 2014, na mengine sita yalikuwa na chini ya visa kumi vya maambukizi.
Hata hivyo, Afrika bado inachangia asilimia 80 ya visa vyote vya maambukizi ya ugonjwa huo na asilimia 78 ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
Mkurugenzi mkuu wa WHO daktari Margaret Chan amesema ufanisi wa vita dhidi ya malaria ni moja ya habari njema zaidi kutokea katika miaka 15 iliyopita.
“Ni ishara kwamba mikakati yetu imefanikiwa, na tunaweza kushinda ugonjwa huu ambao huua mamia ya maelfu ya watoto kila mwaka,” amesema.
Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Oxford walidadisi takwimu kutoka vituo 30,000 Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na wanakadiria visa 663 milioni vya maambukizi vilizuiwa katika miaka 15 iliyopita.
Neti za kuzuia mbu wanaoeneza viini vya malaria zilichangia kupungua kwa visa hivyo asilimia 68, dawa aina ya artemisinin asilimia 22 na dawa za kuua wadudu asilimia 10.
CHANZO:BBCSWAHILI
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.