ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, December 10, 2025

GAMONDI ATEMA MAJINA MAKUBWA STARS KUELEKEA AFCON 2025.

 

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Miguel Gamond ametaja kikosi cha wachezaji 28 kitakachopeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano wa kombe la Mataifa Afrika AFCON 2025 huko Morocco ambapo Stars ipo Kundi C, sambamba na Uganda, The Cranes, Nigeria na Tunisia

Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta, Simon Msuva, Kibu Dennis na Kelvin John ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kuongoza safu ya ushambuliaji huku kinara wa magoli kwenye Ligi Kuu bara, Paul Peter (magoli 5), mshambuliaji wa Simba Sc, Selemani Mwalimu na kiungo wa Young Africans Sc, Mudathir Yahya wakitemwa.

Tuesday, December 9, 2025

MECHI ZA LEO UEFA NI PRESHA TUPU....


Italia kutakuwa na mechi ya kukata Inter Milan vs Liverpool ambao hivi karibuni wamekuwa na matokeo ambayo hayaridhishi kabisa kwani kwenye mechi 13 amabzo amecheza ameshinda 3 pekee. Mara nyingi hawa wawili kukutana ilikuwa kwenye fainali na Jogoo wa Anfield alipoteza. 

Vijana wa Diego Simeone, Atletico Madrid watakuwa ugenini kukiwasha dhidi ya PSV kutoka kule Uholanzi lakini pia imeweza kupata matokeo dhidi ya timu kubwa kwenye michuano hii. 

AS Monaco atakuwa nyumbani kupepetana dhidi ya Galatasaray ambao walipoteza mechi yao iliyopita wakiwa nyumbani. Mwenyeji yeye alitoa sare, hivyo pointi 3 ni muhimu kwa timu zote siku ya leo. 

Marseille yeye atakuwa kibaruani kumenyana vikali dhidi ya Union St.Gilloise ambao wanahitaji ushindi siku ya leo ili wasogee mbele kwenye michuano hii. Tofauti ya pointi kati yao hadi sasa ni hakuna kwani wote wana pointi sawa. 


Bayern Munich yeye atakipiga dhidi ya Sporting CP ambapo mpaka sasa kwenye mechi 8 ambazo amecheza amekusanya pointi 10 huku vijana wa Kompany wao wakichukua pointi 12. Mwenyeji ametoka kupoteza huku mgeni yeye akishinda. 

Kwa upande wa Chelsea wao watakuwa ugenini kukipiga dhidi ya Atalanta baada ya mechi iliyopita kushinda, halikadhalika kwa wenyeji nao walishinda. 


Vijana wa Hans Flick, FC Barcelona watakuwa nyumbani kusaka ushindi dhidi ya Eintracht Frankfurt ambao wana pointi 4 pekee hadi sasa huku Wacatalunya wao wakiwa na pointi 7. Barca wanahitaji ushindi kwa namna yoyote ile ili wajiweke kwenye nafasi nzuri ya michuano hii.  

Tottenham  Spurs atakuwa kibaruani kukipiga dhidi ya Slavia Prague ambao kwenye mechi 5 wameambulia pointi 3 pekee. Huku wenyeji wao wakiwa na pointi 8 hadi sasa. 

"MSIWE NA HOFU MWANZA HALI NI SHWARI CLIP INAYOSAMBAA NI YA TAREHE 31 OCTOBA 2025" RC MTANDA


NA ALBERT G. SENGO/MWANZA

🛑Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ametoa taarifa rasmi kuhusu hali ya usalama mkoani Mwanza, huku akikanusha vikali uvumi unaoenezwa mitandaoni kuhusu kuwepo kwa maandamano katika jiji hilo. Katika taarifa hiyo, Mhe. Mtanda ameeleza kwa uwazi kuwa video inayosambazwa mtandaoni si ya leo, bali ni tukio la zamani linalotumiwa kupotosha umma. 👉 Fuatilia video kamili kupitia #youtube chanel yetu hapa ujue alichokisema kwa kina Mkuu wa Mkoa juu ya usalama, uzushi wa maandamano, na msimamo wa serikali mkoani humo.
#mwanza #maandamano
Vituo vingi vya wauzaji wa mafuta na gesi jijini Mwanza, vimesitisha huduma kwa siku ya leo.
Hakuna huduma, hakuna pilikapilika kama ilivyozoeleka, vituo vingi vya wauzaji wa mafuta na gesi jijini Mwanza, vimesitisha huduma kwa siku ya leo.
Maduka mengi mtaa wa Nyerere yamefungwa.
Ni tofauti na ilivyozoeleka, leo magari ni ya kuhesabu katika barabara hii yenye pilika pilika hapa jijini Mwanza.
Muonekano wa barabara ya kuelekea Kirumba.
Muonekano wa barabara ya Makongoro uelekeo wa uwanja wa ndege jijini Mwanza.
Hakuna usafiri wa daladala zaidi ya pikipiki na bajaji, barabara ya Nyakato National kuelekea Igoma, Kisesa.
Watu wa kuhesabu barabarani.
Muonekano kutoka barabara ya Nyerere hii ni barabara ya kuelekea mitaa iliyozoeleka kwa pilikapilika nyingi ya Rufiji na Uhuru, lakini leo watu wachache na magari ya kuhesabu.
Hakuna huduma kwa siku ya leo.
Muonekano.
Muonekano.

Monday, December 8, 2025

VITALIS MAYANGA AFUNGIWA MECHI TANO NA KUTOZWA FAINI.

 

Mshambuliaji wa Mbeya City, Vitalis Mayanga amefungiwa kucheza mechi tano sambamba na kutozwa faini ya Tsh Milioni 1 kwa kosa la kumpiga kiwiko kwa makusudi beki wa kushoto wa Simba SC, Anthony Mligo.

Uamuzi huo umetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) katika taarifa ya TPLB leo Desemba 8, 2025.

SIMBACHAWENE: HAKUNA TISHIO LA KUZIMWA INTERNET TANZANIA, HALI YA USALAMA NI SHWARI.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema kuwa hatua ya kuzima mtandao wa intaneti nchini ni chaguo la mwisho kabisa, na kwa sasa hakuna sababu yoyote inayoashiria uwezekano wa TCRA kuchukua hatua hiyo kuelekea maadhimisho ya Uhuru kesho, Desemba 09, 2025.

Akizungumza leo, Desemba 08, 2025, Simbachawene amesema kuwa taarifa zinazosambaa mtandaoni kuhusu hofu ya kuzimwa kwa internet hazina msingi, kwani hali ya kiusalama nchini imo katika kiwango cha kuridhisha.

“Kuhusu kuzimwa mtandao, kwa sababu nyenzo kubwa inayotumika na hawa wanaharakati wa mitandaoni ni taarifa za taharuki… mpaka sasa hatujaona tishio lolote la kusema mtandao umekuwa tatizo,” amesema.

Ameeleza kuwa mitandao ya intaneti ina mchango mkubwa katika maisha ya kila siku ya Watanzania, kuanzia shughuli za kibenki, usafiri, mawasiliano hadi huduma mbalimbali za kijamii, hivyo serikali haina sababu ya kuuzuia bila msingi wa kiusalama ulio wazi.

“Tufahamu mtandao huu ndio unatumika kutoa huduma nyingi za kijamii. Kwa hiyo kuzima internet ni chaguo la mwisho sana pale ambapo hali ikiwa mbaya… lakini mpaka sasa, tunaoangalia usalama wa nchi, tunaona hali ni shwari,” amesema.

Simbachawene amesisitiza kuwa hadi sasa hakuna tishio lolote linaloweza kuilazimu TCRA kuzima huduma za intaneti, na Watanzania wanapaswa kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila wasiwasi.

WANAFAMILIA 9 WALIOKUFA KATIKA AJALI WAKIENDA MAZISHI YA JAMAA YAO WAZIKWA PAMOJA

 

Waombolezaji wakitoa heshima za mwisho kwa ndugu na marafiki waliofariki kwa ajali hiyo. 


 Safu za majeneza meupe zilikaa kimya chini ya hema, picha ya kuhuzunisha ilinaswa na kusambazwa mtandaoni na mwandishi wa habari Bruce Kanzika. 

 Waombolezaji kutoka kila aina ya maisha walikusanyika kuwaaga waathiriwa ambao maisha yao yalikatizwa katika wakati mmoja, wa kuhuzunisha. 

 Msiba huo umetikisa kijiji cha Sango ambapo familia ilikuwa ikisubiri kwa hamu kuwasili kwa jamaa zao kwa mazishi ya bibi yao, Mama Perpetua Tsivona.

 Huenda swali likawa:- Jeh Waathiriwa walikuwa wakisafiri kwenda wapi?

Gari hilo, lililokuwa limebeba abiria 15, lilikuwa njiani kutoka Nairobi kwenda Lugari wakati ajali hiyo ilipotokea, na kuhitimisha safari iliyokusudiwa kuunganisha familia yenye huzuni. 

Simu iliyovunja mioyo ya familia nzima Kwa wazazi wa marehemu, maumivu bado hayajafikirika. Irene Haron, mama wa watoto tisa, alikumbuka kupokea simu kutoka kwa watoto wake, akimhakikishia kwamba walikuwa karibu na Naivasha na wangekuwa nyumbani alasiri. 

Muda mfupi baadaye, ulimwengu wake ulivunjika. “Sijui hata niseme nini. Watoto wangu wote tisa, wote wameenda,” alisema, akitetemeka huku akijitahidi kuelezea huzuni yake. “Kila ninapofikiria kuhusu hilo, mimi hutetemeka tu.” Mumewe, Mzee Haron Tsivona, anakumbuka kupokea simu kutoka kwa nambari ambayo hajui wakati yeye na jamaa wengine walikuwa wakiimba nyumbani kwa mama yake.

 Alipopokea simu, alikuwa polisi wa trafiki akimjulisha kwamba wanafamilia wake walikuwa wamehusika katika ajali. “Dakika chache tu mapema, watoto wangu walikuwa wamepiga simu kusema walikuwa karibu kurudi nyumbani,” alisimulia, sauti yake ikiwa nzito kwa kutoamini. 


Bajeti ya mazishi:-

 Wakati wanandoa hao wakikabiliwa na kazi isiyofikirika ya kuwazika watoto wao wote tisa, mzigo wa kifedha umeongeza safu nyingine ya uchungu. Familia ilikuwa na bajeti ya KSh milioni 4.5 kufidia gharama za mazishi, kiasi ambacho ni zaidi ya uwezo wao, na kulazimisha kutafuta msaada kutoka kwa wasamaria wema. 

Jamaa aliyetambuliwa kama Paulo Wawire alishiriki matumaini na ndoto ambazo watoto hao wa marehemu walikuwa nazo kwa wazazi wao, akiongeza kuwa walikuwa wameanza tu kupanga kujenga nyumba mpya kwa ajili ya wazazi wao. Miongoni mwa waliotembelea familia hiyo alikuwa Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera ambaye alitoa mchango wa KSh milioni 1 kutoka kwa Rais William Ruto ili kusaidia mipango ya mazishi. 


Je, ajali hiyo ilikuwa na manusura? 

Huku Chevaywa akijiandaa kuwazika tisa wake, manusura wa ajali hiyo mbaya wanaendelea kulazwa hospitalini wakipokea matibabu. Kijiji hicho, kikiwa kimezidiwa na huzuni, kinashikilia umoja na maombi huku kikikabiliana na moja ya nyakati za giza zaidi katika historia yake. Kwa familia ya Haron, njia ya kuelekea uponyaji itakuwa ndefu, lakini jamii imeapa kuitembea nao, hatua moja, siku moja baada ya nyingine. 

IMBEJU NI ZAIDI YA MPANGO WA KUTOA MIKOPO CRDB BANK

 

  
Dar es Salaam – Katika hafla ya Marketers Night Out iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, aliwasilisha mada iliyoangazia kwa kina mchango wa programu ya Imbeju katika kubadilisha maisha ya wananchi, hasa wanawake na vijana, kupitia uwezeshaji wa kiuchumi na kukuza ujumuishi wa kifedha nchini.

Akizungumza mbele ya wataalamu wa masoko, viongozi wa taasisi, wajasiriamali na wadau wa maendeleo, Mwambapa alisema Imbeju ni zaidi ya mpango wa kutoa mikopo pekee bali ni programu jumuishi inayolenga kujenga msingi imara wa ujasiriamali. Alieleza kuwa programu hiyo imejengwa juu ya nguzo tatu kuu; elimu ya ujasiriamali na uongozi, upatikanaji wa mitaji rafiki, pamoja na uunganishaji wa wajasiriamali na masoko pamoja na huduma rasmi za kifedha.
 
“Kupitia mafunzo ya vitendo, washiriki huwezeshwa kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi, kutumia fursa za teknolojia, kufuatilia mapato na faida kwa weledi na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji. mbinu hiyo imewezesha wajasiriamali wengi kuimarisha biashara zao na kuongeza ajira katika jamii”, alisema Mwambapa

Akizungumzia wanawake, Mwambapa alieleza kuwa wamekuwa walengwa muhimu wa programu kwani ndio mhimili wa ustawi wa familia na jamii. Wanawake wengi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za mtaji na elimu ya ujasiriamali sasa wameweza kuanzisha au kupanua biashara zao kupitia Imbeju, jambo lililosababisha kuongezeka kwa uzalishaji, kuboreshwa kwa kipato cha kaya na kuinuka kwa hali ya maisha ya familia zao. Alisisitiza kuwa uwekezaji kwa mwanamke mmoja hupelekea kuleta mafanikio kwa kizazi kizima.

Kwa upande wa vijana, alisema programu hiyo imekuwa chachu ya kubadilisha fikra bunifu kuwa miradi halisi katika maeneo ya teknolojia, kilimo-biashara, sanaa na biashara mtandao. Kupitia ushauri wa kitaalmu, mafunzo na ufadhili wa mawazo bunifu, vijana wengi wamepata uwezo wa kuzifikisha bidhaa zao katika masoko mengi zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo kuongeza ushindani na kupanua wigo wa biashara zao.
Mwambapa pia aligusia mchango wa Imbeju katika kukuza ujumuishi wa kifedha nchini kwa kuwawezesha wananchi waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa benki kufungua akaunti, kujiwekea akiba, kukopa na kufanya miamala kwa urahisi zaidi baada ya kupata elimu ya kifedha. Kupitia ushirikiano wa CRDB Bank Foundation na Benki ya CRDB, huduma hizi sasa zimefika hata maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma za kifedha ulikuwa mdogo awali.

Alisema hatua hiyo imeimarisha uthabiti wa biashara ndogondogo, kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa wananchi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akihitimisha mada yake, Mwambapa alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kuwekeza katika mipango inayowawezesha wanawake na vijana, akisisitiza kuwa mafanikio ya Imbeju ni ushahidi kuwa uwekezaji katika watu ndiyo msingi wa kujenga uchumi jumuishi, thabiti na wenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Friday, December 5, 2025

MANISPAA YA KIBAHA YAJA NA MPANGO WA KUSAIDIA KUPAMBANA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI

 

NA VICTOR MASANGU, KIBAHA 

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani imeweka mipango madhubuti na kujipanga vilivyo ambayo itaweza kusaidia kwa kiwangon kikubwa  katika kuhakikishwa kwamba  maambukizi mapya ya ugonjwa wa virusi vya ukimwi (VVU) hususan kwa upande wa  maambukizi ya  kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto  yanapungua kwa kiwango kikubwa.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa huduma za ukimwi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dr. Mariam Nganja kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji Dr. Rogers Shemwelekwa  wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani ambayo yamefanyika katika viwanja vya mwendapole na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali, wakuu wa idara  watumishi wa  afya pamoja na wananchi  kutoka maeneo mbali mbali.
Mratibu huyo amesema kwamba katika kutekeleza mipango hiyo ya kupunguza maambukizi ya VVU amewahimiza wananchi wote kujenga tabia ya kwenda kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kufahamua hali ya afya zao ikiwemo kufahamu na kujua utambuzi kama wameambukizwa lengo ikiwa ni kuanza kupatiwa dozi ya matibabu kwa haraka.


Aidha amebainidha kwamba kwa sasa hali  ya maambukizi wa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha bado yapo juu hivyo kunahitajika juhudi za makusudi ikiwemo kukemea vikali vitendo vya ubakaji,ilawiti,ukatili wa kijinsia pamoja na baadhi ya tabia ambazo zinapelekea tabia ya maambukizi ya ugonjwa wa VVU.

 Kwa upande wake Afisa utumishi wa Halmashaurii ya Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela ambaye ndiyr aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amewataka wananchi wote kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja katika kutokomeza maambukizi mapya  ya  ugonjwa wa virusi vya ukimwi.

Pia amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha nyingi katika Halmashaurinya Kibaha amabazo zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo amabzo zimeweweza kugusa katika sekta tofauti tofauti ikiwemo suala la kuboresha afya.

Pia amebainisha kwamba Rais katika kuhakikisha anaboresha huduma ya afya kwa wananchi ameweza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Liulanzi ikiwa sambamba na kununua vifaa tiba amabvyo vimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwasogezea huduma ya upapatikanaji wa huduma.

Naye Kaimu mganga mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dr.Abdulkadri Sultan ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuimarisha miundomibu katika  vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali ikiwemo suala la upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na madawa kwa ajili ya wananchi.

Maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani katika Halamshauri ya Manispaa ya Kibaha yamefanyika katika viwanja vya mwendapole ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu  inasema kwamba shinda vikwazo imarisha mwitikio tokomeza ukimwi kwa mwaka 2025.

CCM PWANI HAWANA DOGO WAMPA MAUWA YAKE RAIS DKT.SAMIA KWA HOTUBA YAKE YENYE TIJA KWA TAIFA

 


Na Victor Masangu,Kibaha


Katibu  wa Siasa ,Uenezi  na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Dkt. David  Mramba   amesema ameipongeza kwa dhati hotuba ya Mhe.Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan  aliyoitoa tarehe Disemba  2 mwaka huu alipozungumza  na wazee wa Jiji la Dar es Salaam na kubainisha kuwa  imegusa masuala  muhimu  yanayohusu Taifa  na kutoa dira na  matumaini  makubwa  kwa maslahi ya kuleta maendeleo  kwa  wananchi wa Tanzania.

  Dkt.Mramba amesema hayo leo tarehe 5 Desemba 2025  katika mkutano na Waandishi  wa Habari uliofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya CCM  wa.  Pwani.

" Chama Cha Mapinduzi  Mkoa wa Pwani  kinaunga mkono  kwa kauli moja kama ifuatavyo;kuimarisha  amani ya Muungano, tunaunga  mkono  msisitizo wa Mhe. Rais  juu ya kulinda amani, utulivu na mshikamano wa Taifa letu kwani amani ndiyo  msingi  wa maendeleo  na hotuba yake imeonesha  dhamira  ya dhati  ya kuendeleza maridhiano,umoja na kudumisha  muungano wetu.

Mramba  amesema kuwa katika kuchochea  uchumi na fursa  za maendeleo Chama Cha Màpinduzi  Mkoa wa Pwani  wanapongeza kwa moyo wote  maelekezo  ya Mhe. Rais  kuhusu  kuendeleza  mageuzi  ya kiuchumi ,kukuza utekelezaji, kuimarisha  miundombinu  na kutengeneza ajira kwa wanawake.

"Katika hotuba ya Mhe.Rais  ameweka wazi  kuwa Serikali  inaendelea  kujenga  mazingira  rafiki ya biashara  na kuhakikisha  matunda  ya uchumi  yanawafikia  wananchi wake" amesema Dkt. Mramba.

Aidha Dkt. Mramba amesema kuwa  Mhe.Rais amesema kuwa  atahakikisha anasimamia  utawala bora  na mapambano  dhidi ya rushwa pia  kwamba CCM  Mkoa wa Pwani  wanaunga  mkono kauli ya Mh.Rais ya kuendeleza  vita dhidi ya  rushwa ,ubadhirifu na matumizi mabaya  ya madaraka kauli yake imedhihirisha kuwa Tanzania  inaongozwa  kwa misingi  ya  haki  uwajibikaji na uwazi.

" Chama Cha Mapinduzi  Mkoa wa Pwani  tunapongeza dhamira  njema  ya Serikali  katika  maeneo yafuatayo:
kuimarisha  sekta  ya afya, kuboresha elimu,kutoa wigo mpana  wa upatikanaji wa maji safi, kuhakikisha huduma bora  za kijamii kwa wazee,vijana  na makundi zinapatikana  kwa wakati ,katika kipengele pia ikumbukwe kuwa  hotuba  ya Mhe.Rais  Inaonesha Uongozi  shirikishi  unaoweka mbele utu na ustawi wa Watanzania" amesisitiza  Dkt. Mramba.

Kuhusu ushirikiano  wa ushirikishwaji wa wazee  amesema ,"CCM  Mkoa wa  Pwani tunaunga  mkono kwa  dhati  utayari wa Mhe. Rais  kusikiliza ushauri wa wazee ,kuthamini mchango wao na kutambua  kama nguzo muhimu ya hekima na utulivu  wa taifa letu".

Dkt. Mramba amehitimisha kwa kusemakuwa  CCM Mkoa wa Pwani  wanaunga mkono hotuba ya Mhe. Rais Samia  kwa sababu kuu nne ikiwa ni pamoja na kuweka  mwelekeo  sahihi wa taifa ,inajenga
matumaini  kwa watanzania ,inasisisitiza mshikamano na inaweka  msingi  wa maendeleo  endelevu  kwa vizazi  vya sasa  na vijavyo.

" Sambamba na  na hayo yote ,Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa wa Pwani  tunampongeza  Mhe.Rais Dkt Samia  Suluhu  Hassan  kwa  uongozi wake  mahiri , wenye hekima  na wa kijasiri kwa kuonesha  uzalendo wa kweli  katika  kulipigania  Taifa. 
CCM  Mkoa wa Pwani kwa umoja wetu, tunaahidi, kushirikiana  na  serikali katika  kutekeleza maelekezo  yote  yaliyotolewa  kwa  manufaa na maslahi ya Taifa.

Tuesday, December 2, 2025

DC KIBAHA AKABIDHI GARI LITAKALOTUMIKA KUBORESHA HUDUMA KATIKA DIVISHENI YA ARDHI

 

NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon,(Hapo Juu Pichani Kushoto) amekabidhi rasmi gari jipya kwa Divisheni ya Ardhi na Mipango Miji, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi katika utatuzi wa changamoto za ardhi.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mhe. Simon alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka kipaumbele katika utatuzi wa migogoro ya ardhi na upatikanaji wa maeneo ya viwanda na uwekezaji.

“Hili gari limeletwa ili muweze kuwafikia wananchi kwa haraka na kuhakikisha changamoto za ardhi zinatatuliwa kwa wakati. Nawaomba mlitunze na mlitumie kwa kazi iliyokusudiwa,” alisema Mhe. Simon, huku akimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa kutekeleza maagizo kwa ufanisi.

Awali, akiwasilisha taarifa fupi, Dkt. Shemwelekwa alibainisha kuwa gari hilo linathamani ya shilingi milioni 170, na litakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza kasi ya utoaji huduma bora hususan katika Divisheni ya Ardhi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Ardhi, Denis Kahumba, amesema changamoto ya usafiri ambayo ilikua ikikwamisha utendaji sasa imepatiwa ufumbuzi.

“Ahadi yangu ni kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tunashukuru kwa vitendea kazi na mazingira mazuri ya kazi ambayo yameongeza morali kwa watumishi,” alisema Kahumba.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Rugambwa Banyikila, ametoa pongezi kwa uongozi wa Manispaa ya Kibaha kwa kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili ofisi ya ardhi na kuwataka watumishi kuongeza bidii na uwajibikaji.

Makabidhiano haya yanatarajiwa kuongeza kasi ya usimamizi wa ardhi, kutatua migogoro, na kuimarisha huduma kwa wananchi wa Kibaha, huku yakiendana na dira ya Serikali ya kujenga mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo.

DR. NICAS KUNOGILE AKWEA PIPA NAFASI YA UMEYA HALMASHAURI MANISPAA YA KIBAHA

 


Na Victor Masangu,Kibaha 


Diwani mteule wa Kata ya Tumbi  Dkt. Nicas Mawazo amechaguliwa kuwa Meya mteule wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha baada ya kupata kura 15 kati ya kura halali zipatazo  19 ambazo zimepigwa na madiwani  wateule wa chama cha mapinduzi (CCM)  huku Aziza Mruma akichaguliwa kuwa katika nafasi ya Naibu meya kwa kupata kura 10 .

  Akitangaza matokeo hayo ya uchaguzi wa ndani wa chama Katibu wa Chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Issack Mawazo amebainisha kwamba zoezi zima uchaguzi huo umemalizika  salama na kwamba viongozi  hao wateule wanatarajiwa kuapisha Disemba 4 mwaka huu  

Katibu huyo amefafanua kuwa zoezi hilo la uchaguzi limekwenda vizuri na kwamba  wagombea wote wameridhishwa na matokeo hayo na kuwahimiza viongozi hao kuvunja makundi na badala yake wawatumikie wananchi.


Kwa upande wake Meya mteule kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM ) Dr,Nicas Mawazo  amesema kwamba uchaguzi huo umeendeshwa kwa haki na uhuru na kwamba matarajio yake makubwa ni kushirikiana na madiwani wenzake katika kuwaletea chachu ya maendeleo ikiwa pamoja na kuwapambania wananchi walio wanyonge.

 Naye Naibu Meya mteule  waa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Aziza Mruma amesema kuwa lengo lake kubwa ni kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Viongozi hao waliochaguliwa katika nafasi za Meya na Naibu Meya   Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wanatarajiwa kuapishwa rasmi  Disemba 4 mwaka huu.

Monday, December 1, 2025

NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI ATOA MAAGIZO KWA WAKURUGENZI JUU YA KAMPENI YA KUWAPELEKA WATOTO SHULE

MWANDISHI:- VICTOR MASANGU, PWANI MTANGAZAJI:- ALBERT G.SENGO Naibu waziri Ofisi ya Waziri mkuu Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Reuben Kwagilwa anayeshugulikia masuala ya elimu amewaagiza wakurugenzi wote nchi nzima kufanya kampeni kwa ajili ya kuwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka na kuwaandikisha watoto wao shule za awali na msingi pindi ifikapo Januari mwaka 2026, Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo ameweza kugagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambayo imejengwa katika eneo la Disunyara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kumwagiza mkandarasi kumaliza mradi huo kwa muda uliopangwa.

Sunday, November 30, 2025

STANBIC BANK MWANZA YAFANYA KWELI SEKTA YA AFYA MWANZA

 NA. ALBERT G.SENGO/MWANZA

Benki ya Stanbic imeonesha tena dhamira yake ya kusaidia jamii kwa vitendo, baada ya kukabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 19 kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza. Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na vitanda vya wagonjwa, mashuka na viti mwendo, vitapelekwa katika Hospitali za Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, ili kusaidia katika utoaji wa huduma bora za afya. Kutoka kwa mwanahabari wetu Albert G. Sengo., anashuka na taarifa kamili

Wednesday, November 26, 2025

DKT. MWIGULU AWAONYA WAVUNJIFU WA SHERIA

 WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani vitekeleze sheria hizo bila upendeleo kwani tabia ya kuogopana na kuoneana aibu imechangia baadhi ya watu kukwepa wajibu wakati wengine wakibebeshwa mzigo wa sheria.


“Yeyote atakayevunja sheria akamatwe na hatua zichukuliwe kwa usawa. Huyu mmoja anavunja sheria anakamatwa, analipa. Huyu mwingine anavunja mbele yake anaachwa. Kama una haraka, toka mapema zaidi si kufidia kwa kuvunja sheria.”

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Novemba 26, 2025) wakati akifungua Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa haitakuwa uungwana kuona baadhi ya watu wakilipa adhabu papo hapo wanapokosea ilhali wengine wakiachwa kupita bila kuchukuliwa hatua.

Amewaonya baadhi ya viongozi na madereva wa Serikali ambao wanaelewa sheria vizuri lakini bado wanazikiuka kwa makusudi. “Ni muhimu kuwasaidia watumiaji wa vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji ambao kwa sehemu kubwa wanaweza kuwa hawazielewi sheria kikamilifu, badala ya kuwaadhibu kwa upendeleo.”

Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kuwapa Watanzania wote heshima na kuhakikisha sheria zilizowekwa zinatekelezwa kwa maslahi ya wote na kuongeza kuwa endapo zipo sheria ngumu kutekelezeka, basi zibadilishwe ili kila Mtanzania anufaike.


Ameviagiza vyombo vya usimamizi wa sheria vihakikishe kuwa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri wanazingatia usimamizi wa sheria na kuchukua hatua kwa yoyote anayevunja sheria akamatwe na kuchukuliwa hatua bila kuonewa aibu.

“Inaudhi mtu amebeba mgonjwa anafuata sheria, halafu mwingine anapita tu anavunja sheria, hapati adhabu. Mlalahoi akivunja sheria anapata adhabu, tunawapa kazi watekeleza sheria kuwaomba radhi watu waliovunja sheria. Naelekeza kila mtu afuate sheria, uwe wa serikalini ama uwe binafsi, tumeweka sheria, zifuatwe kama zilivyo.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema sekta ya uchukuzi ni mojawapo ya sekta wezeshi za uchumi duniani kota na kwamba watu wanahitaji njia za uchukuzi ili kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wa usafirishaji nchini ili kuhakikisha masuala ya nishati safi yanapewa kipaumbele. Akitoa mfano, Waziri Mbarawa alisema: “Uendeshaji wa reli ya kisasa (SGR) unatumia nishati ya umeme, mabasi ya mwendokasi njia ya Mbagala yanatumia gesi asili na baadhi ya taxi na bajaji zinatumia gesi asili.”

Tuesday, November 25, 2025

WATAALAM WA KIMATAIFA WATOA MWELEKEO MPYA WA UCHUMI KATIKA KONGAMANO LA TIA MWANZA


TIA Yasistiza Utafiti na Ubunifu Katika Kuchochea Uchumi – Kongamano la Kimataifa la 4 la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi Lafana Mwanza

Mwanza, 25 Novemba 2025 – Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) leo imeongoza Kongamano la 4 la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi, lililofanyika katika Ukumbi wa Nyerere, Gold Crest Hotel jijini Mwanza, likiwa na ujumbe mahsusi unaoangazia nafasi ya ubunifu, uvumbuzi na biashara katika kuchochea uchumi endelevu.


Akizungumza kumwakilisha mgeni Rasmi, Benjamin Magai ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali , amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, kama njia ya kutoa suluhisho la changamoto za kijamii na kiuchumi. Akibainisha kuwa utafiti ndio injini ya maendeleo, hasa katika maeneo kama ubunifu, teknolojia, tathmini, miundombinu na mikakati ya maendeleo yenye tija.


Dira ya Maendeleo ya 2050 Yawekwa 

Dhima: Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu

Kongamano la mwaka huu limebeba kaulimbiu “Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu.” Kaulimbiu hiyo imegawanywa katika mada 11, huku machapisho 41 ya tafiti yakitarajiwa kuwasilishwa.

Prof. Pallangyo alisema kuwa kabla ya mawasilisho ya tafiti, kutakuwa na watoa mada wakuu 8 (Keynote Speakers) kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambao ni wabobezi katika nyanja zao. Miongoni mwao ni:

Watoa Mada Wakuu ni kama ifuatavyo:-

Ephias Ruhode (Uingereza) – Amefafanua namna mkakati wa biashara unavyopaswa kuongoza kabla ya teknolojia, hasa katika zama za Akili Bandia (AI) kupitia mada “In the Age of AI, Business Strategy Comes Before Technology.”
Gaoua Abdelouahab (Algeria) – Ameeleza namna mabadiliko ya kidigitali na ujasiriamali yanavyoweza kuwa injini ya mapinduzi ya kiuchumi, akichambua “The Algerian Experience.”
Prof. Oksana Kiseleva (Urusi) – Amesisitiza umuhimu wa Ecosystem za Ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi duniani.
Dkt. Collin Kamalizeni (Afrika Kusini) – Amejadili nafasi ya uongozi shirikishi katika kuponya majeraha ya uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mada “Reimagining Inclusive Leadership as a Catalyst for Economic Recovery in Sub-Saharan Africa.”

Prof. Tandy Lwoga (Tanzania)
– Amezindua mjadala juu ya jinsi ubunifu unavyoungana na ujasiriamali katika muktadha wa mifumo ya kidijitali kupitia mada “Innovation Meets Entrepreneurship: Rethinking Digital Collection Development for the Future-Ready User.” 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Pallangyo,  amekumbusha kuwa TIA ni mojawapo ya taasisi kongwe na muhimu nchini katika kutoa elimu ya uhasibu, ugavi na fani nyingine za biashara. Ikiwa na kampasi 8 nchini na zaidi ya wanafunzi 32,000, na taasisi hiyo imeendelea kuimarisha mfumo wa mafunzo unaozingatia umahiri (Competence Based Training – CBET), sambamba na kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.

Akimkaribisha Profesa Goodluck Urassa kutoa salamu za Bodi, viongozi wote wametia mkazo umuhimu wa TIA kuendelea kuwa kichocheo cha sera na maarifa kwa taifa.

Baada ya mawasilisho ya tafiti, TIA imetangaza kuwa itachapisha kitabu maalum kitakachokusanya mapendekezo ya watafiti juu ya namna bora ya kutatua changamoto katika sekta za biashara na uchumi. Kitabu hicho kitasambazwa kwa wadau muhimu, ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama mchango wa TIA katika kusaidia sera na maamuzi ya maendeleo.


Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza utalii, washiriki wa kongamano wamepangiwa kutembelea vivutio vya Jiji la Mwanza. Hii ni sehemu ya mkakati wa kutumia kongamano kama nyenzo ya kuhamasisha utalii wa ndani.