Kiwanda kikubwa cha kutengeneza dawa kinatarajiwa kujengwa nchini ili kupunguza adha na gharama zinazoikumba nchi wakati wa kuagiza dawa nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Julai 3 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati wa kujadili uwekezaji wa kiwanda cha dawa hapa nchini.
"Leo tumekutana kujadili jinsi ya kuwekeza na kiwanda cha kutengeneza dawa cha FOSUN PHARMA hapa nchini ili kupunguza changamoto za kuagiza dawa nje ya nchi na kutokomeza tatizo la upatikanaji wa dawa nchini,” amesema Waziri Ummy.
Amesema kujengwa kiwanda hicho kitapunguza asilimia kubwa ya fedha inayokwenda nje kwa ajili ya manunuzi ya dawa kwani mpaka sasa asilimia 94 ya fedha zinakwenda kununua dawa nje na asilimia 6 ndiyo inanunua dawa ndani ya nchi.
Waziri Ummy amesema uwekezaji huo utapunguza muda wa kuagiza dawa kwani muda mwingine huchukua miezi tisa mpaka 11 kupata dawa kutoka nje ya nchi hivyo kuifanya Serikali kuagiza mzigo mkubwa zaidi ili kukimbizana na mahitaji ya Watanzania.
"Tunatumia muda mrefu kupata dawa tangu tunapoagiza na wakati mwingine tunaweza kupata dawa zisizo na ubora kutokana na dawa hizo kukaguliwa na mdhibiti wa nje hivyo zinaweza zikaruhusiwa tu na zikija kukaguliwa na mdhibiti wa ndani unaweza kukuta hazina ubora,” amesema Waziri Ummy.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa kampuni hiyo inayotengeneza sindano za kutibu malaria kali ya ATESUNAT itaweza kutengeneza sindano nyingi zaidi na kuweza kuwahudumia nchi jirani ikiwemo Kenya, Uganda na Burundi.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kuwa hakuna kikwazo kwa kampuni hiyo kuanzisha ujenzi wa kiwanda cha dawa hapa nchini kwani kitasaidia upatikanaji wa dawa kwa urahisi na kukua kwa uchumi kupitia viwanda.
"Tumejadili na kuwakubalia bila ya kuweka kikwazo kwani tumeridhishwa na ubora wao katika utengenezaji wa dawa na mafuta nchini kwao hivyo tunawakaribisha kuja kufanya uwekezaji huo," amesema Waziri Mwijage.
Naye Mkurugenzi wa Kituo Cha Uwekezaji Nchini, Geofrey Mwambe amesema kuwa wameupokea uwekezaji huo na wanaufanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kuipeleka Tanzania kuelekea uchumi wa Viwanda.
"Kutokana na ahadi ya Rais Dk John Pombe Magufuli la kuipeleka nchi kwenye uchumi wa viwanda na kutokomeza kabisa tatizo la uhaba wa dawa hatuna budi kushirikiana na wawekezaji hao kutimiza lengo hilo," amesema Mwambe.
Mbali na mawaziri Mwalimu na Mwijage, kikao hicho cha kujadili uwekezaji wa kiwanda hicho cha kutengeneza dawa pia kimehudhuriwa na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Kituo cha Uwekezaji nchini TIC na wadau mbalimbali.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.