KOREA Kaskazini imesema kuwa, katika
utekelezaji wa siasa zinazotajwa na Marekani za 'Uvumilivu wa Kimkakati'
hakuna utofauti yoyote baina ya Rais Donald Trump au mtangulizi wake
Barack Obama.
Gazeti la Rodong Sinmun la chama
tawala nchini Korea Kaskazini limeandika kuwa, Rais Trump anakusudia
kuendeleza njia ile ile ya makosa ya mtangulizi wake na kwamba kile
kinachoshuhudiwa hii leo hakina tofauti yoyote baina ya viongozi hao
wawili. Gazeti hilo limeongeza kuwa, siasa za Marekani zinazoitwa
'mkakati' au 'Uvumilivu wa Kimkakati' hazitakuwa na faida yoyote ghairi
ya uharibifu.
Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni Rex W. Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alinukuliwa akisema kuwa, siasa za uvumilivu wa kimkakati zilizotekelezwa kwa miongo miwili iliyopita kwa ajili ya kusimamisha mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini, sasa zimefikia tamati. Wakati huo huo, Pyongyang imesema kuwa, hata hapo awali serikali ya Barack Obama iliwahi kutangaza kufikia mwisho siasa hizo za uvumilivu wa kimkakati na kwamba pamoja na hayo haikuweza kuchukua hatua yoyote na badala yake iliendelea kufanya makosa ya muda mrefu.
Gazeti la Rodong Sinmun la chama tawala nchini Korea Kaskazini limesisitiza kuwa, makosa ya siasa za Marekani hayatailetea faida nchi hiyo, bali yatazidi kuisukuma Pyongyang kuweza kujiimarisha zaidi kijeshi sambamba na kustawisha silaha zake za nyuklia kwa lengo la kukabiliana na chokochoko hizo za Washington.
Ripoti hiyo imetolewa
katika hali ambayo duru za jeshi za Korea Kusini zimearifu kwamba, kuna
uwezekano mkubwa Korea Kaskazini ikafanya jaribio la sita silaha zake za
nyuklia katikati ya mwezi ujao wa Aprili, suala ambalo limeitia
tumbojoto serikali ya Seoul na waitifaki wake, yaani Marekani na Japan.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.