ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, October 5, 2016

MAKOPO 44 YA DAWA BANDIA YAKAMATWA MWANZA

NA ANNASTAZIA MAGINGA,Mwanza. 

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) Ofisi ya Kanda ya Ziwa imekamata makopo 44 ya dawa bandia za kutibu Malaria kwenye duka la kuuza dawa za binadamu la Magira Phamarcy lililopo Jijini Mwanza.

Mamlaka hiyo pia imelifungia duka hilo kutokana kuuza dawa aina tatu  zilizoisha muda wake na zisizo na usajili kinyume na sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya sura 219 ya mwaka 2003.

Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Kanda ya Ziwa Mtani Njegere amesema  dawa  zilizokamatwa  ni  makopo 20 ya dawa bandia za kutibu malaria aina ya Quinine Sulphate BP toleo namba 150002 iliyotengenezwa Mwezi Mei 2015 na ambayo tarehe ya mwisho wa matumizi ni April 2019 inayodaiwa kutengenezwa na kiwanda cha Shelly Pharmaceuticals cha Jijini Dar es Salaam na makopo 24 ya dawa bandia za Asprin (vidonge) toleo namba 66436 inayodaiwa kutengenezwa mwezi Mei 2016 ambayo mwisho wake wa matumizi ni Aprili 2019.

“Tuligundua kuwa dawa aina ya Quinine Sulphate BP ni bandia kwa sababu taarifa juu ya lebo zilikuwa zinatofautiana na herufi (font Size) katika tarehe ya kutengeneza na matoleo zilikuwa tofauti jambo ambalo si utaratibu wa viwanda vinavyofuata taratibu sanifu za kutengeneza dawa (GMP) kama Shellys na Asprin alama muhimu katika lebo zinazotambulisha dawa kuwa ni ya kiwanda cha Labs & Allied hazikuwepo “amesema Njegere.

Njegere amesema  bandia nyingine zilizokutwa katika duka hilo ni chupa  30 za dawa ya Penicillin G (Sodium benzylpencillin) inayodaiwa kutengenezwa na kiwanda cha CSPC Zhongnhuo pharmaceutical for Dawa Limited na kopo moja la dawa ya caredomet (indomethacin) inayodaiwa kutengenezwa na kiwanda ch Shanxi Xinxintong Co. L TD cha nchini China.

Mbali na kukutwa na dawa bandia pia duka hilo lilikutwa na dawa ambazo hazikuwa na usajili kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Ambazo ni  Folic Acidi (Tablets), Ampimed (Ampicillin inj), Chlorpromazine inj), Adrenaline injection na Zithromax (Azithromax).

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.