Airtel Fursa yawafikia vijana Mkoani Manyara
Mkuu wa wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Crispin Meela amewataka vijana mkoani humo kuchangamkia fursa ya mafunzo ya ujasiriamali na msaada wa vifaa vya kuendeshea biashara vinavyotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, kupitia mradi wake wa Airtel Fursa.
Meela ametoa wito huo mjini Babati mkoani MANYARA, wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya Aritel Fursa ambapo zaidi ya vijana 200 wameshiriki mafunzo hayo.
Amewahimiza vijana hao kubuni miradi inayohusiana na kilimo kwa kuwa sekta hiyo ndio yenye uhakika wa kuajiri idadi kubwa ya watu hivyo kujikwamua kiuchumi
"Ni lazima vijana muwe wabunifu na mjiunge kwenye vikundi vya wajasiriamali ili muweze kutumia vizuri fursa zinazotolewa na Airtel pamoja na serikali kufanyabiashara kwa viwango vinavyokubalika" amesisitiza Meela.
Aidha ameongeza kwa kusema mafunzo haya ambayo yanatolewa bure kwa vijana yatachangia kiasi kikubwa katika kupata ujuzi na kuboresha uendeshaji wa biashara zao na kuongeza ufanisi. Na kuwapongeza sana Airtel kwa kuwekeza katika vijana mbalimbali nchini
Akizungumza na vijana hao, Meneja huduma kwa jamii Bi Hawa Bayumi amesema kuwa vijana wengi zaidi wanatarajiwa kufikiwa nchini kote katika awamu ya pili ya mradi huo.
Amesema Airtel Fursa haitoi mikopo bali vijana watakaokidhi vigezo watapatiwa ruzuku itakayotumika kununua zana zitakazotumika kuinua uzalishaji katika miradi wanayoiendesha
"Kuna timu ya wataalamu watakaopitia miradi itakayowasilishwa ambao watapitia vigezo vilivyoainishwa na washindi watasaidiwa vifaa ili ndoto zao za kujikwamua kiuchumi ziweze kutimia' Alisisitiiza Bayumi.
"Katika awamu ya kwanza ya Airtel Fursa tuliweza kuwafikia vijana 2500 kupitia mafunzo kama haya tunayoya fanya Leona vijana 13 walifanikiwa wakawezeshwa kwa kupewa vitendea kazi na hivi sasa wanafanya vizuri katika biashara zao"
Amesema AIRTEL imefanya utafiti nchi nzima na kubaini changamoto lukuki zinazowakabili vijana ikiwemo ukosefu wa mitaji, ubunifu na elimu ya Ujasiriamali ndio maana ikaamua kuwekeza katika kundi hilo.
"Tunaamini kuwa vijana watakao saidiwa watakuwa chachu ya kuwawezesha vijana wengine kwa kuwaajiri na baada ya miaka michache vijana watakuwa wamejikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini" aliongeza Bayumi.
Amewashauri vijana nchini kote kuchangamkia fursa hiyo kwa kujipatia elimu ya ujasiriamali inayotolewa na kampuni yake ili waweze kufaidina mradi huu
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.