ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, December 30, 2015

WABUNGE MWANZA WAMTAKA WAZIRI SIMBACHAWENE KUANDA UTARATIBU UTEKELEZAJI AHADI MLIONI 50 ZA MAGUFULI

Maria Kangoye, Mbunge kupitia Kundi la Umoja wa Vijana wa CCM taifa.

Na  PETER FABIAN, MWANZA.

WABUNGE wamuomba Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora, Geroge Simbachawene , kuandaa mkakati wa utekelezaji ahadi ya Rais Dk John Magufuli, kuhakikisha Sh 50 milioni zinawafikia wananchi kwenye vijiji na mitaa kwa walengwa ili kupata mikopo kwa lengo la kupambana na kuondoa umasikini.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Stanslaus Mabula wa CCM, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (Mwanza) na Maria Kangoye, Mbunge kupitia Kundi la Umoja wa Vijana wa CCM taifa jijini Mwanza wakilieleza GSENGO BLOG kuwa ili kuondokana na tatizo la vijana kuilalamikia serikali suala la ajira na utekelezwaji wa ahadi ya Rais Dk Magufuli ni vyema Wizara ikaanza kuanda mkakati mzuri wa utekelezaji.
 
Mbunge Mabula, alisema kwamba suala la serikali kutoa kiasi cha Sh. 50 milioni kwa kila mitaa na vijiji nchini kote kwa lengo la kuwakopesha wananchi ni jambo zuri lakini linahitaji umakini mkubwa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia na kuwagusa wananchi wa hali ya cini ili kuwasaidia kukopa na kuendesha shughuli zao za kilimo na ujasiliamali ili kupambana na kujikwamua na umasikini.
 
“Waziri Simbachawene, pamoja na watalamu wake waanze kuandaa taratibu mzuri ambao utawezesha fedha kufika kwenye Halmashauri na kuwakopesha wananchi waliosajili vikundi vyao hasa vile vya wananchi wenyehali za chini badala ya kutoa mikopo hiyo kwa vikundi ambavyo vimeisha kuwa na mitaji mikubwa,”alisema.
 
Mabula alisema kwamba Wizara na Halmashauri zisipoweka utaratibu mzuri wa fedha hizo na unaweza kupelekea wananchi watakaokopeshwa kuwa wale ambao si walengwa bali wajanja watakaotumia mwanya huo kuanzisha vikundi kwa ajili ya kukopa fedha hizo na kuacha wananchi ambao serikali inalenga kuwawezesha ili kujikwamua na umasikini.
 
Naye  Kangoye akizungumza juzi baada ya kumalizika Kikao cha Baraza la UVCCM Mkoa wa Mwanza, amemuomba Waziri Simbachawene kuzibana Halmashauri za Majiji, Manispaa na Wilaya kuhakikisha zinatekeleza utaratibu wa utoaji fedha asilimia 5 kwa vikundi vya vijana na asilimia 5 vikundi vya wanawake pamoja na kuandaa mazingira ya kuwawezesha wananchi kupitia ahadi ya Rais Dk Magufuli na Serikali ya awamu ya tano ya kuwakopesha fedha katika vijiji na mitaa.
 
“Tulikuwa na mabilioni ya JK lakini yalitolewa kwa watu ambao hawakuwa walengwa hivyo kwa kasi na utendaji wa serikali ya awamu ya tano ni vyema tukajipanga na kuandaa utaratibu mzuri ambao utawezesha wananchi kufikiwa na mikopo hiyo ili kujikwamua na kuondokana na umasikini wakizingatia kujiajiri na hili lazima tulipiganie wabunge wote na kuibana serikali kulitekeleza,”alisema.
 
Kangoye ametoa rai kwa vijana wenzake kujipanga na kuanzisha vikundi ambavyo watavisajili ikiwa ni pamoja na kuoanisha shughuli watakazozifanya baada ya kupata mikopo hiyo na wasianzishe vikundi kwa ajili ya kutaka kujipatia fedha tu, pia wathubutu kufanya kazi na shughuli za ujasiliamali uliolenga kuwaingizia kipato badala ya kukaa vijiweni wakisubiria ajira za serikali ambazo ni vigumu kuchukua vijana wengi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.