ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, December 30, 2015

MEYA AMUAGIZA MKURUGENZI KUWABANA WAZABUNI NA VIKUNDI VYA USAFI KUONDOA TAKA, MCHANGA BARABARANI NA TOPE KWENYE MITALO

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza James Bwire.
Na PETER FABIAN, MWANZA.

MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, James Bwire, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Adam Mgoyi, kuwasimamia wazabuni wa shughuli za usafi na mazingira kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao na watakaoshindwa awachukulia hatua a kisheria ikiwemo kuvunja mikataba yao.
Kauli hiyo aliitoa jana akiwa ofisini kwake katika jengo la Halmashauri ya Jiji hilo, Bwire alieleza kwamba kumekuwepo na taarifa kutoka kwa wananchi wakilalamikia vitendo vya wazabuni na vikundi vinavyojishughulisha na usafi wa mazingira kuondoa uchafu kwenye mitaro ikiwemo tope na kuitelekeza kando ya barabara na uchafu kutozolewa kwenye madampo yasiyo rasmi. 
Bwire ambaye ni Diwani wa Kata ya Mahina (CCM), alisema kufatia hali hiyo kuwepo amemuagia Mkurugenzi Mgoyi, kuanza kumbana Afisa Afya wa Jiji hilo kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika maeneo waliyopo wazabuni na vikundi vya shughuli za usafi kwenye mitaa ya katikati ya Jiji na pembezoni katika Kata zote 18 za Jiji hilo.
“Kumekuwa na tatizo la ugonjwa wa mlipuko (kipindupindu) hasa maeneo ya Kata za Igoma na Nyegezi Wilayani Nyamagana, sasa nivyema tukaanza kuchukua hatua pia kuwabana wazabuni na vikundi vilivyona mikataba ya shughuli za usafi wa mazingira kwani imebainika kutokuwepo uwajibikaji wao vizuri katika maeneo ya mitaa ya Kata zote 18 za Jiji letu hivyo watekeleze wajibu wao,”alisisitiza.
Meya alieleza kwamba baadhi ya wazabuni na vikundi vimeonekana kushindwa kuondoa michanga iliyojaa kwenye barabara za lami na mawe na kuonekana hazifanyiwi usafi lakini pia kumekuwepo na mrundikano wa taka kwenye maeneo ya kukusanyia taka kuzozolewa kwa muda mrefu pamoja na kutolewa tope kwenye mitalo na kutozolewa kwa wakati na kusababisha adhaa kwa wananchi.
“Nimemuagiza Mkurugenzi Mgoyi kuhakikisha hili linafanyiwa kazi ukizingatia kipindupindu kimeripotiwa kurejea tena katika baadhi ya maeneo ya mitaa ya Kata za Igoma na Nyegezi lakini kuhakikisha uchafu uliokusanywa kwa muda mrefu unazolewa na kuwabana wazabuni kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kama mikataba inavyowataka,”alisema.
Bwire pia alisema kwamba Mkurugenzi na wataalam wake wahakikishe wanafanya ukaguzi kwenye soko kuu, masoko ya jioni, mialo na maeneo ya minada kuwaelimisha wananchi juu ya suala la kufanya usafi kwa kuwa ni zoezi endelevu la kuliweka Jiji la Mwanza katika mkakati wake wa kurejesha ushindi wa kwanza wa usafi na mazingira iliyoupoteza mwaka huu na kuchukuliwa na Jiji la Arusha.
Meya huyo ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kata zote kuendelea na shughuli za usafi wa kila siku huku akisisitiza kuwa kila jumamosi ya kwanza ya mwezi kufanyika shughuli ya usafi kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kufanyika kwa usafi nchini kote.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.