IFIKAPO mwezi Agosti mwaka huu 2019 Halmashauri ya Jiji la Mwanza inategemea kuanza kulivunja Soko kuu la jijini hapa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba mapema leo asubuhi wakati akipokea msaada wa vifaa vya kufanyia usafi na uzoaji vilivyotolewa na Benki ya Biashara na Mikopo ya 'Akiba Commercial' katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani iliyo adhimishwa ndani ya viunga vya soko hilo tegemeo kwa huduma za uuzaji jumla na rejareja mazao ya chakula na bidhaa mbalimbali lililopo kata ya Pamba wilayani Nyamagana.
Zaidi ya shilingi bilioni 23 zitatumika kwenye ujenzi wa soko hilo la kisasa ambalo tayari mkandarasi wake amekwisha patikana, nalo likitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imeambatana na zoezi la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko Kuu jijini Mwanza ambapo wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika pamoja na wafanyabiashara sokoni hapo kufanya usafi huo.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na zoezi endelevu la kufanya usafi katika soko hilo na kuweka mazingira katika hali ya usafi ili kuzuia magonjwa ya milipuko huku akitoa pongezi kwa Serikali kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba aliyepokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella na kuvikabidhi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza, amesema vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa wa kuimarisha usafi na hivyo wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira safi na salama kiafya.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.