ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, July 3, 2018

HOTUBA YA RAIS DKT.JOHN MAGUFULI BAADA YA KUWAAPISHA VIONGOZI IKULU JIJINI DSM.JULAI 2,2018



GSENGOtV
Rais Magufuli amewataka viongozi hao kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa huku wakizingatia kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 na kuhakikisha wanatimiza matarajio ya Watanzania katika taasisi wanazoziongoza.
Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Mbarawa kushughulikia kikamilifu matatizo ya maji ambayo bado yanawakabili Watanzania licha ya Serikali kupeleka fedha nyingi katika wizara hiyo, kwa kuhakikisha miradi yote iliyokuwa inasuasua inaendelezwa kwa kasi zaidi ikiwemo kusimamia vizuri Shilingi Trilioni 1.2 ambazo Serikali imekopa kutoka India kwa ajili ya miradi ya maji katika mikoa 17.
Kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa wizara hiyo na hivyo amemtaka Mhe. Lugola kushughulikia matatizo yaliyopo katika wizara hiyo yakiwemo maelekezo ya kamati ya Bunge iliyotaka hatua zichukuliwe dhidi ya mkataba wa ufungaji vifaa katika vituo 108 vya Polisi uliogharimu Shilingi Bilioni 37, uagizaji wa magari 777 ya polisi ambayo yamekwama bandarini na baadhi yake kuonekana yametumika, kashfa ya ununuzi wa sare za Polisi, uhaba wa magari katika Jeshi la Zimamoto, kudhibiti mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo hayana maslahi kwa Taifa, utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni na ongezeko kubwa la ajali za barabarani, ambapo amemtaka kuwawajibisha mara moja Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Usalama wa Barabarani wa Mkoa huo kufuatia ajali 3 zilizotokea mkoani humo na kusababisha watu 40 kupoteza maisha ndani ya wiki mbili.
Kwa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mhandisi Kamwelwe kuhakikisha miradi mikubwa ya ujenzi ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege, utengenezaji wa meli, barabara za juu na njia za mabasi yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam inatekelezwa kwa kasi zaidi pamoja na kusimamia vizuri Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na maendeleo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
“Serikali imenunua ndege 7, nataka ieleweke hizi ni ndege za Serikali sio za ATCL, lakini lengo letu ni kuiwezesha ATCL ilete watalii wengi ili tunufaike na utalii, asilimia 70 ya watalii husafiri kwa ndege, kwa hiyo kwa kukosa ndege tunapata Watalii Milioni 1 tu kwa mwaka, wakati nchi za wenzetu ambao hawana vivutio vingi kama sisi mfano Misri wanapata Watalii zaidi ya Milioni 10 kwa mwaka” amesema Mhe. Rais Magufuli. Walioapishwa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji - Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano - Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Alphaxard Lugola, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira - Mhe. Mussa Ramadhani Sima na Naibu Waziri wa Kilimo - Mhe. Omary Tebweta Mgumba.
Wengine ni Katibu Mkuu Ikulu - Dkt. Moses Mpogole Kusiluka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi - Meja Jen. Jacob Gideon Kingu, Katibu Mkuu Uvuvi – Dkt. Rashid Adam Tamatamah, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi - Bw. Kailima Ramadhani Kombey, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi – Bw. Mathias Bazi Banduguru na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo – Prof. Siza Donald Tumbo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Jaji Mbarouk Salim Mbarouk kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Thomas Bashite Mihayo kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Balozi Mstaafu Omary Ramadhani Mapuri kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Bw. Athuman Juma Kihamia kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC na Bw. Mohamed Ali Ahmed kuwa Naibu Msajili wa vyama vya siasa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.