ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, October 17, 2024

Wednesday, October 16, 2024

RAIS RUTO KUMTEUWA MAKAMU WA RAIS MPYA IWAPO SENETI ITAIDHINISHA KUBANDULIWA KWA GACHAGUA


Rais William Ruto anatarajiwa kumteua naibu rais mpya iwapo Bunge la Seneti litaendelea na hatua ya kumtimua Rigathi Gachagua. Picha: Rigathi Gachagua/William Ruto.

Kuondolewa kwa Rigathi Gachagua ofisini kutakuwa ni tukio la kihistoria, kwani itakuwa mara ya kwanza kwa naibu rais aliye madarakani kukabiliwa na mashtaka ya kutokuwa na imani naye katika historia ya Kenya. 

Tumaini la mwisho la Gachagua kuokoa wadhifa wake ni nini? Hatima ya Naibu Rais sasa iko mashakani huku Seneti ikitarajiwa kuanza kujadili mashtaka yake Jumatano, Oktoba 16, na uamuzi wa mwisho ukitarajiwa kufanywa Alhamisi jioni, Oktoba 17.

Matokeo ya mchakato wa kuondolewa kwake yanategemea ikiwa theluthi mbili ya maseneta watapiga kura kumuondoa ofisini. 

Akizungumza na NTV, Wakili wa Mahakama Kuu Steve Ogolla alisema kuwa hatima ya Gachagua sasa iko mikononi mwa Seneti, kufuatia mahakama kukataa kusimamisha Seneti kuendelea na mjadala wa mashtaka ya kutokuwa na imani naye. 

"Hii ilikuwa nafasi yake ya mwisho kusimamisha mchakato huu na hakufanikiwa. Ukweli ni kwamba hatima yake sasa iko mikononi mwa Seneti. Lakini, naamini pia amejiandaa kwa Seneti, tumeona amewasilisha majibu yake kwa hoja hiyo," Ogolla alisema. 

Ni nini kitafuata ikiwa Gachagua ataondolewa na Seneti? Kuondolewa kwa Gachagua kutoka ofisini kunaweza kuacha pengo kubwa ndani ya serikali ya Kenya Kwanza, na kumlazimu mkuu wa nchi kuteua naibu rais mpya kufikia Ijumaa, Oktoba 18. "Kinachoweza kutokea baada ya kuondolewa ni kwamba rais anaweza kuteua mrithi wa Gachagua haraka. 

Lakini kifungu cha 149 bado kinahitaji kuwa mgombea huyo apitishwe na Bunge la Kitaifa ndani ya muda wa siku 60, lakini wanaweza kufanya hivyo haraka," Ogolla aliongeza. 

UANDIKISHAJI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA WAFIKIA 45% NCHINI - WAZIRI MCHENGERWA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka wananchi kuendelea kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.

Amesema hayo wakati akizungumza na  waandishi wa habari jana Oktoba 15, 2024  katika ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa lengo la kufikisha elimu na hamasa kwa Wananchi  juu ya umuhimu wa kujiandikisha.


Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wenye sifa na wanaokidhi vigezo vya kugombea wajitokeze kuchukua fomu kuanzia Oktoba 26, 2024 mpaka Novemba 1, 2024 ili waweze kugombea  nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za Mitaa na Vijiji.

Vilele Waziri Mchengerwa  amewataka wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, kanuni, miongozo pamoja na maelekezo ya usimamizi wa uchaguzi.

"Maelekezo yangu kwa wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia kanuni viapo na kutekeleza majukumu kwa mujibu wa viapo vyao". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Aidha Mhe. Mchengerwa amewataka Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kutoa elimu kwa wanachama wao juu ya kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Zoezi la kujiandikisha katika daftari la makazi limeanza rasmi  Oktoba 11, 2024 mpaka Oktoba 20, 2024 ambapo kila Mwananchi mwenye sifa na vigezo anatakiwa kujiandikisha katika eneo analoishi ili aweze kushiriki zoezi la Uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Tuesday, October 15, 2024

MAFIA BOXING PROMOTION WAUNGA MKONO KAMPENI YA RAIS DKT SAMIA SULUHU YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 

  

Na Oscar Assenga,TANGA

KAMPUNI ya Mafia Promotion Boxing imetoa msaada wa majiko ya Gesi kwa wanawake wanaojishughuli na uuzaji wa vyakula katika masoko ya Mgandini, Makorora na Mlango wa Chuma yaliyoko jijini Tanga ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu ya matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.

Licha ya kugawa mitungi hiyo ya gesi lakini wametoa msaada mwengine wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulea watoto yatimacha Green Cresent Ophanege Foundation cha Jijini humo .

Hatua ya kampuni hiyo kuunga mkono juhudi hizo inatokana na ushindi walioupata mabondia mbalimbali wanaodhaminiwa na kampuni hiyo ambao walipata ushindi katika mapambano yao walipopanda hivi mwanzoni mwa mwezi 0ctoba mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Mkurugenzi wa Matangazo na Uzalishaji kutoka Kampuni ya Mafia Promotion Omari Clayton alisema pambano hilo lilichagizwa na Technical Knock Out ‘KO’ ya Rais Dkt. Samia Suluhu.

Alisema baada ya ushindi huo wapewa fedha taslimu kama zawadi kwa mabondia hao ambayo imewatia hamasa kuhakikisha wanazidi kuijengea heshima Tanzania kupitia mchezo wa ngumi.

Alisema kwamba jambo ambalo wameifanya kwa kugawa majiko hayo ya gesi ni kama sehemu ya kurudisha kwa jamii ikiwa ni utaraibu wao na wanaungana na watanzania kupitia Kampeni ya Rais Dkt. Samia ya kuhamasisha juu ya matumizi ya nishati safi na kuachana na matumizi ya mkaa na kuni katika kupikia na shughuli nyingine hali ambayo inasababisha mabadiliko ya tabianchi na uzalishaji wa hewa ukaa.
Alisema kwamba kampuni hiyo ya Mafia wanaunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kupambana na kuhamasisha watanzania kuhama kutoka kwenye matumizi ya mkaa na kuni kupikia na kwenda kwenye matumizi ya nishati safi.

“ Ndio maana leo tumegawa majiko ya gesi kwa mama zetu wanapika vyakula katika masoko yaliyopo katika jiji la Tanga” Alisema Clayton.
“Tumehamasika na tunampongeza sana Rais wetu Dkt. Samia kuja na ‘KO ya Mama’ na kuwazawadia mabodia wetu ambao walipambana kuhakikisha wanabakisha mikanda hapa Tanzania na walifanikiwa na tunamuahidi kwamba mama kupitia Mafia Boxing tutazidi kuiheshimisha Tanzania”Alisema .

Akizungumza kwa niaba ya mabondi wenzanke Ibrahim Mafia alisema kwamba haikuwa rahisi kupamba ulingoni kutokana na mpinzani wake kuwa imara lakini kupitia maombi ya watanzania alipambana kuhakikisha anawapa furaha kwa kupata ushindi .

“Ule ushindi ni ushindi ni ushindi wetu lakini pia ni ushindi wa watanzania walikuwa wakituombea tumepokea zawadi kutoka kwa Rais wetu mama Samia tukaona hatuwezi kuitumia peke yetu bali tushirikiane kile ambacho tumepata kwa kuwapa majiko ya gesi na kutoa msaada kwa kituo cha watoto yatima tunaomba mzidi kutuombea dua ili wakati mwingine tuweze kutoa kikubwa zaidi. Alisema Mafia”

Bondia Ibrahim Mafia alipanda ulingoni kuzichapa na mpinzani wake Enoch Tettey raia wa Ghana kuwania mkanda wa dunia ‘World Boxing Council Bantamweight’ wenye uzito wa Kg 53 katika ukumbi wa City Center Hall Magomeni Sokoni na hatimaye kufanikiwa kubwaga chini mpinzani wake kwa KO.
Hata hivyo wakina mama mntilie ambao walipata majiko hayo waliwapongeza mabondia wote kwa ushindi walioupata pamoja na kuishukuru Kampuni ya Mafia Boxing Promotion kwa kuwapatia mitungi ya gesi ambayo itawasaidia katika shughuli zao.
Tunawashukuru kwa zawadi zenu na sisi tunaendelea kuwaombea kwa Mungu hakika atawalipa tulikuwa na changamoto ya kupata mkaa kwa ajili ya kupikia lakini sasa kupitia majiko haya yatatusaidia kurahisisha shughuli zetu za kupika kila siku .

Monday, October 14, 2024

RAIS SAMIA APOKEA MWENGE WA UHURU KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO MBIO ZA MWENGE WA UHURU MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi wakati akihitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge ambazo kitaifa zimefanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba tarehe 14 Oktoba, 2024.

 "Nimehitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na Wiki ya Vijana hapa mkoani Mwanza. Ninawashukuru wote waliojitokeza kushiriki tukio hili la kihistoria ambapo Mbio za Mwenge wa Uhuru zimefikisha miaka 60."

"Pongezi kwa wote walioshiriki kuukimbiza kwa mwaka huu na kazi nzuri waliyofanya ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo"


"Nimepokea taarifa ya miradi yote iliyotembelewa katika mbio hizi ambayo inakwenda kunufaisha wananchi kwenye kila kona ya nchi yetu. Nimepokea mapendekezo na salamu za wananchi wa maeneo yote ulikopita Mwenge wa Uhuru, na kwa umakini na uharaka tutayafanyia kazi yale yote yaliyoainishwa kwa manufaa ya Taifa letu"

RAIS wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 14, 2024 amewaongoza Viongozi na Wananchi mbalimbali kwenye kilele cha mbio za Mwenge zilizoambatana na Wiki ya Vijana na Nyerere Day katika uwanja CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Rais Samia akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa mbio hizo Ndugu Godfrey Eliakim Mzava kwenye Kilele cha Maadhimisho Mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Matukio mbalimbali katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.


TASAC YAFANYA MAZUNGUMZO NA KANALI MTAMBI KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

 





Katika jitihada zake za kuendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kuzungumzia masuala ya usalama wa usafiri wa majini kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kanali Mtambi ameipongeza TASAC kwa hatua mbalimbali wanazochukua kuimarisha masuala ya usafiri wa majini na ushirikiano wanaoutoa katika Mkoa wa Mara na hususan usalama wa wasafiri katika katika Ziwa Victoria.


Kanali Mtambi ameiomba TASAC kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria na kanuni zinazohusiana na usafiri wa majini kwa wananchi na taasisi za Serikali na binafsi ili kupunguza ajali na athari za ajali za vyombo vya usafiri wa majini.


“Sisi kama Serikali tunatakiwa kuendelea kuwahakikishia usalama watumiaji wa Ziwa Victoria ikiwemo wasafiri wanaotumia vyombo vya usafiri vya majini kuhusiana na usalama wao wanapotumia usafiri wa majini,” amesema Mhe. Kanali Mtambi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira na Usafiri wa Majini, Bi. Leticia Mutaki amesema TASAC inaendelea na jukumu lake la utoaji wa elimu ya usalama wa usafiri majini kwa wadau wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo taasisi na Halmashauri kuhusiana na usimamizi wa usafiri wa majini.


“Tuna mpango wa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Halmashauri zote zinazopakana na ziwa ili Halmashauri zisaidie kusimamia usafiri wa majini kwa niaba ya TASAC,” amesema Bi. Mutaki.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC, Bi. Judith Kakongwe amesema Sheria na kanuni za sasa zinawabana zaidi wenye vyombo vya usafiri kuweka jaketi okozi lakini haziwabani abiria kuzivaa jambo ambalo linaleta changamoto kwa sababu wamiliki wakiweka bila kuvaliwa hazisaidii kama inatokea ajali.


“Tupo kwenye mchakato wa kubadili vipengele vya sheria na kanuni ili abiria nao wabanwe kuvaa jaketi okozi na sio tu wamiliki wa chombo kama ilivyo sasa ili kusaidia kupunguza madhara ajali zinapotokea” amesema Bi. Kakongwe.


TPA kuanza usimamizi wa mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela

 

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatarajia kuanza rasmi usimamizi wa shughuli zote za kibandari katika mwalo wa Kirumba ulipo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kufuatia tangazo lililotolewa kwenye gazeti la Serikali.

Akitoa taarifa kwa umma Ijumaa Oktoba 11, 2024 kupitia waandishi wa habari, Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa tangazo la Serikali namba 855 la tarehe 24/12/2023 ambalo linaipa TPA mamlaka ya kusimamia mialo yote iliyo rasmi.

Lugenge aliongeza kuwa shughuli za usimamizi wa mwalo huo zitaanza kesho rasmi Jumamosi Oktoba 12, 2024 zikihusisha usimamizi wa usalama wa vyombo vya majini.

Awali mwalo huo ulikuwa ukisimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ukiwa ni miongoni mwa mialo 10 katika Ziwa Victoria iliyotangazwa kusimamiwa na TPA.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza
Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge akitoa taarifa kwa umma kuhusu TPA kuanza kuusimamia mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela.
Meneja Bandari Kanda ya Ziwa Victoria, Erasto Lugenge akizungumza na wanahabari jijini Mwanza.
Tazama Video hapa chini

Thursday, October 10, 2024

KAMATI YA BUNGE YAMPONGEZA RAIS DKT SAMIA SULUHU KWA KUCHOCHEA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI NCHINI

 

 Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Suleiman Jafo akizungumza wakati wa ziara ya  ya siku moja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara ilipotembelea eneo Kituo cha Forodha za Tanzania na Kenya eneo la Mkinga Mkoani Tanga kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mariam Ditopile Mzuzuri akifuatia Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian
 Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mariam Ditopile Mzuzuri akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo



Na Oscar Assenga, MKINGA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imempongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya kuchochea uwekezaji nchini pamoja na kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara.


Pongezi hizo zilitolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mariam Ditopile Mzuzuri wakati wa ziara ya siku moja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara ilipotembelea eneo Kituo cha Forodha za Tanzania na Kenya eneo la Mkinga Mkoani Tanga.

 

Alisema kwamba mazingira hayo mazuri yamewekwa kwa wafanyabiashara ambao tayari wapo kwenye biashara na viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbal nchini

 

“Leo tumepata fursa ya kuja hapa kituo cha Forodha Horohoro kuona namna kituo hicho cha pamoja baina ya Tanzania na Kenya sisi kama kamati tunawapongeza kwani kituo hiki kazi yake kubwa kukusanya mapato kuhakikisha wafanyabishawa kutoa Kenya wanaoleta bidhaa hawapitia njia za panya wanapitia hapo kutoa ushuru na kodi stahiki pia bidhaa zinazotoka nchini na kwenda nchi jirani zinatoa ushuru stahiki “Alisema

 

Alisema wanawapongeza kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye kituo hicho kwa maana mwaka jana walipanga kukusanya jumla ya sh.Bilioni 77 lakini walikusanya Bilioni 90 na kwa mwaka huu wa fedha wa 2024/2025 kota ya kwanza Julai hadi Sept walipangiwa kukusanya Bilioni 25 lakini wamekusanya bilioni 34 wanaona ni mafanikio.

 

“Sisi kama Kamati tunaiomba serukali na tutalisimamia lazima waongeze ufanisi katika kituo hicho na kikubwa cha kwanza ambacho kimeelezwa ni ununuzi wa scana kwa namna tulivyoona ukusanyaji wa mapato unaridhisha lazima tupate scana na focklift kwa ajili ya kunyanyua mizigo tuweze kuongeza ufanisi na mapat kupanda”Alisema

 

Aidha alisema kwamba inawezekana wanaotumia njia za panya ni kutokana na kukaa muda mrefu wakati wa kupitisha mzigo na hivyo kuona shida kupitishia hapa hivyo tunaiagiza Serikali ndani ya muda mfupi na wizara zote husika na Waziri Dkt Jafo akae na Waziri wa Fedha ili kwa haraka scana na focklift ziweze kupatikana na kuongeza ufanisi na kituo kifanye kazi ile inayokusudiwa chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu na Serikali yake ya wamu ya sita.

 

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Suleiman Jafo amesema kwamba Serikali itahakikisha bidhaa zote zinazopitishwa kwenye vituo vya Forodha katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani zinaendelea kuwa na viwango vinavyokidhi na kudhibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Wakala wa VipimoTanzania ( WMA) na Tume ya Ushindani (FCC).

 

Alisema kwamba lengo la kuhakikisha hilo ni kuwalinda watanzania na walaji wa mwisho wa siku wafanye biashara na kamati imetoa maelekezo kuhakikisha eneo hilo linakuwa na scana ambayo inaweza kuhakikisha mizigo inakwenda kwa haraka sana.

 

“Hili la scana hapa tumelichukua na sio muda mrefu kupitia Wizara ya fedha tutahakikisha Scana hiyo inapatikana pamoja nyenzo za kufanyia kazi ikiwemo Focklift itakayokuwa ikinyanyua mizigo lakini niwashukuru Kamati ya Bunge kwa kazi kubwa na niwaambie serikali itahakikisha mambo yote muhimu yanatekelezwa lengo kubwa ni kuboresha utoaji huduma”Alisema Waziri Jafo.

 

 Aidha alimshukuru R ais Dkt Samia Suluhu kutokana na kazi kubwa inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya kimaendeleo na hata kamati ilivyotembelea eneo la Horohoro imeona kuna mafanikio makubwa kwenye ongezeko la mapato.

 

“Lakini kuona jinsi gani Taasisi zinasaidia kuhakikisha biashara eneo hilo mizigo isafirishwe vizuri baina ya nchi ya jirani kenya na bidhaa zinazopita lazima zinakidhi viwango vilivyowekwa na kuthibitishwa na TBS na WMAna FCC lengo kuwalinda watanzania na walaji mwisho”Alisema Waziri Dkt Jafo.

 

Akizungumzia suala la ubinafsishaji lililofanyika miaka ya nyuma nchini alisema Serikali ilikuwa na nia njema kufanya ubinafsishaji lakini kwa bahati mbaya malengo yalienda tofauti wengi waliopewa viwanda hawakufanya vizuri.

 

“Kama mnakumbuka hivi karibuni Rais Dkt Samia Suluhu alitoa maelekezo kwamba viwanda hivyo vifufuliwe maeneo mbalimbali na nilikuja Tanga na hivi karibuni tumekaa kikao na Hazina kubainisha viwanda vyote na kuona hatua za kuchukua“Alisema

 

Waziri Dkt Jafo alisema mojawapo ya hatua hizo ni kuhakikisha viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi waangalia namna bora ya kufanya kazi kwa utaratibu wa kisheria na wapate wawekezaji wengine au waliokuwepo wahakikishe ndani ya muda mfupi wanafanya uwekezaji ili viwanda viweze kufanya kazi na kutengeneza ajira kwa watanzania.