ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 15, 2022

MAJANGA MIKOPO YA ELIMU YA JUU.

 


Dosari katika mifumo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) zimesababisha baadhi ya wanufaika kuzidishiwa, wengine kupunjwa huku watoto kutoka kaya maskini pamoja na mayatima wakinyimwa kabisa.


Dosari hizo zinaanzia kwenye utambuzi wa wanufaika, upangaji wa viwango vinavyotakiwa kutolewa mpaka kwenye ugawaji wa fedha zinazotakiwa kutolewa kwa wanafunzi wanaostahili.


Kwenye ukaguzi wa ufanisi alioufanya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwa HESLB, amebaini dosari tatu kwenye utoaji wa mikopo hiyo. Makosa hayo ya kimfumo yamesababisha baadhi ya wanafunzi kuzidishiwa fedha kuliko wanavyostahili huku wengine wakipewa kiasi kidogo kisichotosheleza mahitaji na wengine wakikosa kabisa, licha ya kukidhi vigezo vilivyopo.


Waliostahili wakakosa mkopo

Kwa miaka mitano mfululizo, ukaguzi huo umebaini bodi ilitoa mikopo kwa wastani wa asilimia 72, ikimaanisha asilimia 28 ya wanafunzi waliostahili kila mwaka, walikosa mkopo hivyo kuhatarisha uhakika wao wa kuipata elimu ya juu.


“Timu ya ukaguzi ilibaini mwaka 2020/21 wanafunzi 43,053 waliokidhi vigezo walikosa mkopo. Wanafunzi hao waliihitaji Sh124.92 bilioni na katika kipindi cha miaka mitano, wanafunzi 192,039 waliotakiwa kupata Sh569.5 bilioni walikosa mkopo japokuwa walikidhi vigezo,” amesema Kichere.


Miongoni mwa maofisa wa bodi waliozungumza na CAG walisema ugawaji wa mikopo hutegemea upatikanaji wa fedha kutoka serikalini, wakimaanisha kuna wakati hutolewa kidogo ikilinganishwa na wanafunzi wanaostahili.


Aliyewahi kuwa Kiongozi wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TSNP), Abdul Nondo alisema ufinyu wa bajeti ni tatizo la siku nyingi ambalo wanafunzi hulipigia kelele.


“Bajeti inatakiwa kuongezwa na Serikali iwe na mfumo mzuri wa kuwatambua wahitaji wanaostahili,” alisema Nondo.


Yatima, Tasaf nao wachinjwa

Kati ya kundi linalopewa kipaumbele ukiacha wale wanaosoma masomo ya sayansi, ni wanafunzi wanaotoka kaya masikini au waliofiwa na wazazi wao kwani wengi hukosa msaada wa fedha kuwawezesha kulipia shahada zao.


Tofauti na ukweli huo, CAG anasema jumla ya wanafunzi 95 walioomba mkopo kati ya mwaka 2017/18 na 2020/21 ambao ni yatima waliowapoteza wazazi wa wote wawili, hawakupewa fedha walizozihitaji.


“Mwaka 2020/21 wanafunzi mayatima 12 waliohitaji Sh50.23 milioni hawakupewa fedha walizoomba kutokana na dosari ya mfumo na ugawaji wa mikopo,” amesema CAG.


Ukiacha mayatima hao, ukaguzi wa Kichere na wenzake uligundua wanafunzi 22 ambao familia zao zinanufaika na ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania (Tasaf), licha ya kuwekwa kwenye kundi la wenye uhitaji wa hali ya juu lakini walikosa.


“Wanafunzi hao walihitaji Sh84.48 milioni kati ya mwaka 2019/20 na mwaka 2020/21,” amesema CAG.


Akizungumza na Mwananchi, yatima mmoja mhitimu wa chuo kikuu mwaka 2016 ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema alikosa mkopo kwa miaka yote mitatu licha ya kukata rufaa kila mwaka.


“Nilihangaika sana wakati naanza mwaka wa kwanza lakini nilikosa mkopo, nilijaza upya mwaka huo ila nilikosa pia. Nilirudia tena nikiwa mwaka wa pili nikakosa, nilisoma kwa shida sana,” alisema mwanafunzi huyo liyejiunga chuo kikuu akiwa na diploma.


Kuhusu wanafunzi waliohitimu diploma kabla ya kwenda chuo kikuu, Nondo alisema ni kikwazo kwao. “Unakuta mwanafunzi amesoma diploma au QT (mfumo unaotumiwa na walioikosa elimu ya sekondari) anakosa mkopo kwa kigezo cha kwamba alikuwa katika mfumo binafsi hata kama ni mtoto wa maskini,” alisema Nondo.


Wazidishiwa, wapunjwa ada

Chuo kikuu, kila kozi ina gharama zake na mwanafunzi hupewa mkopo kwa kuzingatia shahada anayosoma. Kwenye ukaguzi wake, CAG alibaini mwenendo tofauti, kwani baadhi ya wanafunzi walipewa fedha nyingi za ada kuliko kiwango kilichopangwa na chuo husika, huku wengine wakiambulia kiasi kidogo kisichotosha ada wanayotakiwa kuilipa.


Idadi ya wanafunzi walioongezewa, ripoti inaonyesha walikuwa zaidi ya mara mbili mwaka 2020/21 wakilinganishwa na wa mwaka wa nyuma 2019/20.


Mwaka 2020/21, Kichere amesema jumla ya wanafunzi 4,839 walipokea kiasi kikubwa zaidi ya walichostahili. Idadi hiyo iliongezeka kutoka 2,097 waliokuwapo mwaka 2019/20.


Licha ya mwenendo huo, thamani ya mikopo iliyotolewa ilipungua kwa asilimia 30 katika kipindi hicho kutoka Sh4.71 bilioni mpaka Sh3.32 bilioni katika kipindi hicho.


Kwa miaka mitano iliyopita, Kichere amesema jumla ya Sh13.7 bilioni zilizidishwa kwa baadhi ya wanafunzi waliopokea mkopo wa HESLB.


“Upangaji mikopo zaidi ya kiwango stahiki au chini ya kiwango ulitokana na dosari za mifumo ya upangaji na ugawaji wa mikopo wakati wa zoezi la upangaji na ugawaji wa mikopo kwa wanafunzi,” inasomeka sehemu ya maoni ya CAG.


Mkakati wa kupunguza tatizo

Akizungumzia dosari zilizoainishwa na CAG kwenye ripoti ya mwaka 2020/21, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema wanaboresha mifumo yao ili kila mwanafunzi apate kadri anavyostahili.


“Wakati mwingine national database zinakuwa hazijaunganika vizuri kupitia mfumo wa Gasi. Kuna wanafunzi wanastahili lakini wanakosea kujaza taarifa zao hivyo mfumo unamkataa,” alisema Badru.


Ofisa Mawasiliano wa HESLB, Veneranda Malima alisema viwango vinavyotolewa ni kulingana na utafiti walioufanya katika mwaka husika wa masomo kwa kushirikiana na vyuo vikuu vinavyopokea wanafunzi.


“Tunaangalia hali ya maisha kwa kipindi husika ndio maana huwa tunabadilisha kila baada ya muda fulani. Viwango vya ada tunafuata vinavyotumika kwenye vyuo vya umma na hata inapotokea vyuo vinaongeza gharama ya programu fulani wanatushirikisha,” alisema Veneranda.


Kwa kutambua uwepo wa wanafunzi wengi wanaokosa mikopo kwa sababu mbalimbali, hasa kukosea kujaza fomu, Veneranda alisema bodi inaendelea kutoa elimu kwa wahusika kwa kuwafuata shuleni, wanapukuwa kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mafunzo ya kijeshi hata kupitia vyombo vya habari.


“Tumepunguza mifumo na hatua za kujaza fomu za mikopo, ikiwamo kuondoa baadhi ya nyaraka zilizotakiwa kuambatanishwa ili kupunguza idadi ya wanaokosea kwa sababu hizo,” alisema.


Bajeti ya mkopo

Kasoro zinazowanyima haki baadhi ya wanafunzi wanaostahili zinatokea, licha ya Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya mikopo hiyo kila inapobidi.


Katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa mfano, Serikali ilitenga Sh464 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 145,000 ambazo ni sawa na ongezeko la Sh14 bilioni ikilinganishwa na Sh450 bilioni zilizotengwa mwaka 2019/20 kuwanufaisha wanafunzi 128,285.


Serikali pia iliongeza fedha hizo kwa asilimia 23 mwaka huu wa fedha na kufika Sh570 bilioni.


Waziri wa mikopo wa serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Miseyeki Kijana alisema wanazo njia mbili za kuwaunganisha upya wanafunzi waliokosa mkopo wa bodi na inapobidi hufanya fundraising (uchangishaji wa hiari) kwa wadau, ndani na nje ya chuo.


“Mwaka huu 2021/22 kwa mfano, karibia asilimia 90 ya wanafunzi wa chuo hiki hawakupata mkopo kwa asilimia zote, lakini tuliwaunganisha kufanya maombi upya kwa HESLB na tumepata majibu. Kesho (leo) wanafunzi 300 wameongezewa viwango walivyotakiwa kupata,” alisema Kijana.


Waziri huyo alifafanua kwamba wanaokosa kabisa mkopo wa HESLB, huchangishiwa. “Utaratibu huu umewanufaisha zaidi ya wanafunzi 100 waliolipiwa ada mwaka huu,” alisema Kijana.


Naibu waziri wa mikopo na fedha wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tuamaini (Tudarco), Isaack Msenya alisema wanafunzi wanaokosa mkopo licha ya kuwa na vigezo, huwasiliana na bodi.


“Tunachokifanya tunapopokea malalamiko tunawaunganisha na bodi japo hiyo haitoi guarantee (uhakika) wa kupata ingawa wapo wanaofanikiwa,” alisema Msenya.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.