Na Ezekiel Mtonyole, Iringa.
Wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda iliyopo mkoani Iringa Oscar Herman amebuni kifaa kitakachoweza kutoa taarifa pindi inapotokea hitilafu ya umeme inayoweza kusababisha jengo uungua moto.
Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea shule hiyo ikiwa ni ziara ya kutembelea miradi ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia amesema aliamua kubuni kifaa hicho kwa lengo la kuzuia majanga ya moto hasa kwenye mabweni.
"Hivi karibuni yametokea majanga mengi shule kuungua moto na mabweni ndio maana nikaamua kuja na ubunifu huu hii itakuwa suluhisho" amesema Mwanafunzi Oscar.
Amebainisha kuwa ufanisi wa kifaa hicho ni kwamba kumekuwa na tabia ya wanafunzi kukata nyaya juu ya dali za mabweni kwa lengo la kutumia umeme kwa kificho lakini kwa sasa akikata nyaya ya umeme kifaa hicho kitatoa taarifa kwa msimamizi wa bweni.
Ameongeza kuwa "ni miezi sita tangu nianze ubunifu huu hata nikiwa likizo naendelea na pindi nikirudi shule naendelea na sasa niko hatua nzuri tu kukamilisha kifaa hiki" amesema.
Aidha akishirikiana na mwanafunzi wa kidato cha kwanza Isaya Faustine wanabuni Roboti Maalum litakalokua linasaidia wakulima kupulizia dawa kwenye mazao yao mashambani.
Akizungumzia ubunifu huo, Isaya Faustine wa kidato cha kwanza amesema wamekuja na wazo hilo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwainua wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.
Amesema kwa sasa wako kwenye hatua za awali za utengenezaji wa roboti hiyo na wanatarajia kukamilisha ndani ya wiki moja kwani tayari washapata kibali cha kuanza mradi wao huo wa kutenegeneza roboti hilo.
" Wote tunafahamu kilimo ndio uti wa mgongo wa Nchi yetu hivyo sisi kama wabunifu tumeona tuje na kifaa hichi ambacho kitasaidia wakulima kuweza kupuliza dawa kwenye mashamba yao wakiwa majumbani mwao.
Roboti hili tutalitengeneza kwa mfumo wa Gari lakini halitokua na matairi bali minyororo kama vilivyo vifaru vile vya Jeshi, halafu Mkulima atapaswa kuwa na application kwenye simu yake ambapo akitaka kunyunyuzia dawa Mazao yake analipigia simu na lenyewe linafanya kazi hiyo," Amesema Isaya.
Amesema kukamilika kwa kifaa hicho siyo tu kitakua kinaokoa muda wa wakulima lakini pia kitawaepusha wakulima na maradhi ambayo wamekua wakiyapata kutokana na upulizaji wa dawa wanaoufanya kwenye mazao yao," Amesema Isaya.
Kwa upande wake Oscar Metwa ambaye amebuni pia kifaa cha kuzuia madhara yanayosababishwa na umeme ameiomba Serikali kuwatupia macho wabunifu vijana ili nao waweze kutoa mchango wao kwa Taifa lao.
" Mbali ya mpango wetu huu wa Roboti lakini pia nimebuni kifaa hiki cha kuzuia madhara yanayosababishwa na shoti za umeme ambapo tayari kifaa hiki kimefungwa kwenye mojawapo ya mabweni hapa shuleni na kinafanya kazi," Amesema Metwa.
Ametoa wito kwa wanafunzi wenzake nchini kutoogopa masomo ya Sayansi kwa kisingizio cha kwamba ni magumu bali waweke bidii katika kujisomea kwani hakuna somo gumu endapo utaliwekea bidii na kulipenda.
Nae Mkuu wa Shule hiyo, Yusuph Mwagala amesema katika kusapoti vipaji vya wanafunzi wao ambao wamekua wakifanya ubunifu mbalimbali wamekua wakiwaunganisha na Taasisi zinazokuza wabunifu pamoja na Vyuo mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Chuo Cha DIT kwa ajili ya kujiendeleza zaidi.
" Kama Shule tumekua tukiunga mkono juhudi za vijana wetu wanaofanya tafiti na ubunifu kwa kuwaunganisha na taasisi zinazokuza ubunifu lakini pia kuwaunganisha na Vyuo kama MUST na DIT ambapo kote huko wanaenda kujiendeleza zaidi.
Kuna ubunifu mbalimbali ushafanywa na vijana wetu ikiwemo kutengeneza pampu ya kumwagilia bustani lakini pia ubunifu mwingine ni huu wa kifaa cha kuzuia madhara yanayosababishwa na umeme ambapo kupitia kifaa hiki sasa tunatumia mfumo wa DC na siyo AC ," Amesema Mwalimu Mwagala.'
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.