CHANZO/MWANANCHI
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na wimbi la wanasiasa kuhama vyama vya siasa na kuhamia vingine, waziri wa zamani katika Serikali za awamu ya tatu na nne, Profesa Mark Mwandosya amesema ‘hamahama’ hiyo inatokana na vyama kukosa itikadi, dira na sera inayotakiwa na jamii.
Profesa Mwandosya ameyasema hayo ikiwa ni siku chache tangu wabunge wawili wa Chadema kujiuzulu nyadhifa na uanachama wao na kuhamia CCM.
Wabunge waliohama ni Julius Kalanga wa Monduli na Mwita Waitara wa Ukonga. Pia wapo madiwani zaidi ya 50 wa CUF, ACT-Wazalendo na Chadema waliohamia chama hicho tawala hivi karibuni wakidai kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli.
Akizungumza na Mwananchi jana, Profesa Mwandosya alisema hamahama ya vyama inatokana na changamoto inayovikabili vyama vya siasa barani Afrika na nchi zinazoendelea.
Pia alisema kuhama huko kwa wanasiasa kunatokana na vyama kukosa itikadi inayovisimamia, kwa maana ya mwelekeo na dira pamoja na aina ya jamii ambayo nchi husika zingependa kuijenga.
“Akikaa huko (katika chama alichomo), anaamua kurudi na kupokewa kwa shangwe (katika chama cha awali) mithili ya mtoto aliyepotea katika vitabu vitakatifu. Na kwa sababu anakohamia wanatafuta kuongeza namba, basi inaeleweka kwa nini anapokelewa kwa shangwe,” alisema.
Profesa Mwandosya alifafanua kuwa katika mazingira hayo ni vigumu kutoa sababu za msingi za kiitikadi na kiimani za wanasiasa kurudi katika vyama vya awali, bali mara nyingi ni za kibinafsi zaidi.
Alisema kibaya zaidi mwanasiasa anakorudi kuna watu ambao hata katika mazingira aliyoyaeleza wameendelea kubaki na kukitumikia chama anachohamia.
Alisema watu anaowakuta ndani ya chama husika wanaona “walioasi” wanarudi na kupanda ngazi haraka.
“Jambo hilo limekuwa dhahiri sana baada ya mwisho wa vita vya baridi kati ya nchi za Magharibi na za Mashariki,” alisema mwanasiasa huyo aliyewahi kujitosa kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais mwaka 2005.
Profesa Mwandosya alisema kujenga aina ya jamii inayotakiwa kunahitaji ufafanuzi wa itikadi na sera za uchumi zinazoambatana na itikadi hiyo. Alisema awali sera hizo zilijikita katika ukabaila au usoshalisti.
“Na kila nchi zilitafsiri nini maana ya itikadi na sera hizo katika mazingira yake. Lakini ilivyo sasa, mfumo wa kiuchumi unaongozwa kwa misingi ya soko. Kinachofanyika ni kujaribu kupata itikadi kutokana na mfumo wa uchumi badala ya itikadi kuongoza mfumo wa uchumi,” alisema.
“Vyama vimejikuta katika ombwe la tafakuri hiyo kiasi cha kwamba kushika dola kunakuwa ndio msingi wa kuwepo kwa vyama. Kinachotokea ni kwamba wananchi na wenye nchi hawaoni tofauti za vyama kwa misingi niliyoelezea.”
Alieleza kuwa kutokana na sababu hizo viongozi na wanachama wanaweza kuhama wakati wowote kwenda chama chochote.
“Kwani bila misingi ya kiitikadi, imani ya msingi haipo na masilahi yanakuwa kiini cha maamuzi. Katika hali hii mtu anatoka chama kimoja anaenda kingine, tena kwa jeuri kabisa,” alisema.
Aliongeza kuwa, “sina uhakika kwa kuwa wao ni binadamu wataridhika na hali hiyo. Kwa kawaida, hapo zamani wanaorudi kundini wangepita kwanza kwenye mafunzo au madarasa ya itikadi ili kuwapima kwanza.”
Alisisitiza kuwa ombwe lililopo linatokana na changamoto ya kiitikadi inayoendelea na si kwa Tanzania tu, bali nchi nyingi zinazoendelea.
Miongoni mwa wanasiasa waliohama vyama vyao katika siku za karibuni ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu aliyehamia Chadema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.