ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, January 13, 2015

SAKATA LA IPTL NA AKAUNTI YA ESCROW: HAYA NDIYO MASWALI YA KUJIULIZA.


SAKATA la IPTL na Akaunti ya Escrow ya Tegeta  bado linafukuta hasa katika uwanja wa siasa na maongezi ya kawaida ya watanzania. 

Katika hali ya kawaida, mfukuto wa sakata la IPTL Akaunti ya Escrow ya Tegeta  ungekuwa ni mada nzuri ya utafiti ambao ndio chanzo cha taarifa sahihi zinazoweza kuongoza maamuzi na mijadala katika maeneo mbalimbali. 

Mpaka sasa nachelea kusema kuwa jamii haijapata kuambiwa ukweli wote kuhusu sakata la IPTL Akaunti ya Escrow ya Tegeta; kinachoelezwa ni taarifa nusu nusu ambazo zinalengo la kuendeleza vurugu, kuchafuana, kupakana matope, na kuleta mifarakano isiyo na tija kwa ustawi wa taifa letu.

Aidha taarifa nyingi kuhusu IPTL Akaunti ya Escrow ya Tegeta zinajengeka katika hali ya watoa taarifa  kutumia vibaya imani ambayo watanzania walionayo kwao kuwaaminisha uongo kiasi kwamba ni vigumu kuangalia upande mwingine wa maelezo.

Sakata la IPTL Akaunti ya Escrow ya Tegeta liliibuliwa na Mheshimiwa Mbunge David Kafulila; lakini marejeo yaliyo msingi wa makala haya yanaonyesha pasina shaka kuwa  Mh, Kafulila ni pango la mwangwi wa sauti, maneno, mawazo, na matakwa ya rafiki yake Mheshimiwa  Mbunge Zitto Zuberi Kabwe. 

Aidha Mh. Zitto kwa  nafasi ya Uenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali pia  ni pango la mwangwi wa washindani  wa kimaslahi  katika sekta ya nishati na umeme.


Mh. Zitto kwa kutumia nafasi yake na karama yake ya upotoshaji ameiaminisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Bunge lenyewe, na umma kiasi cha bunge kupitisha azimio la kutaifisha mitambo ya IPTL.


Prince Bagenda katika makala yake Standard Chartered yaliazima Bunge hoja ya ubinafsishaji tunapata ushaidi wa kutumika kwa wabunge na bunge letu kutetea na kulinda maslahi ya watu kwa manufaa ya wachache. 

Bagenda anajenga hoja yake kwenye barua ya Benki ya Standard Chartered ya Septemba 22, 2009  iliyoiandikia TANESCO. Barua hiyo ndefu ilikuwa na mapendekezo mengi, yaliyokuwa yanataka serikali itaifishe TANESCO ili fedha ambazo serikali itaifidia IPTL zitumike kulipa deni la Benki ya Standard Chartered. Kutumika kwa Bunge kutekeleza matakwa ya Benki ya Standard Chartered kumejidhihirisha wazi na kunadhalilisha misingi ya utawala bora.


Marejeo mbalimbali ya maandiko ya Mh. Zitto yanakinzana sana na ukweli na hali halisi duniani kote kama yalivyoandikwa na watu wengine wasiosukumwa na maslahi binafsi kama ilivyo kwa Mh.Zitto.

Mh Zitto anajaribu kuonyesha kuwa IPTL ni mradi uliobuniwa kutengeneza pesa kwa ajili ya wachache tena bila kuwekeza hata sumuni. 

Hoja hii inapingwa ukirejea makala za kitafiti hasa zile za The Program on Energy and Sustainable Development (PESD) taasisi mtambuka ya Kimataifa inayohusisha wachumi,,wanasayansi ya siasa, wanasheria, mameneja , ambao huchunguza uhalisia katika soko la nishati na umeme wakilenga teknolojia na uwezo wake, athari za kisiasa, sheria na kanuni kwenye uwekezaji wa miradi ya nishati na umeme juu ya gharama  na ufanisi.


PESD na professa Anton Eberhard was Chuo Kikuu cha Capetown Afrika Kusini wanabainisha kuwa Independent Power Producer (IPP) ni watu au taasisi binafsi zinazozalisha nishati ya umeme kwa makubalianao ama na Serikali au taasisi ya Serikali inayozalisha au kusambaza nishati ya umeme. 

Kwa mujibu wa marejeo nchi 50 na miradi 200 ya IPP ilikuwa imeanzishwa duniani kote hasa katika nchi zinazoendelea. 


Kwa Tanzania ipo miradi mitatu  ya  IPP ambayo ni:- IPTL(MW 100-mafuta), Songas (MW 190,gesi asilia) Mtwara (MW 12, gesi asilia)

Professa Anton Eberhard anabainisha sababu za kutumika kwa IPP kuwa pamoja na uwekezaji mdogo katika taasisi za serikali za nishati na umeme; udhaifu wa menejimenti na utawala wa taasisi za serikali za nishati na umeme; kupata mtaji wa kuongeza uzalishaji wa nishati na umeme; mabadiliko ya mfumo wa uchumi;kuingiza teknolojia mpya; na sera za Dunia. 


Kwa wanafuatilia mambo hayo yaliyobainishwa yalilikumba shirika letu la ugavi wa nishati ya umeme (TANESCO). 


Aidha hali ya ukame ilizidi kufanya hali kuwa mbaya zaidi na ya dharula.


PESD na wengine wanabainisha sifa za IPP kuwa pamoja na:- kuendeshwa na watu au taasisi binafsi; zinazalisha nishati ya umeme unaounganishwa kwenye mfumo wa taifa; unakuwa na mkataba wa kati ya miaka 20 na 30 (Ogutug, 2007, financing of power projects in developing countries: what is the overall effect of these risks to the lender? Uk.9); na hofu ya hisia za rushwa.

IPP nyingi kama siyo zote zinamilikiwa na watu au taasisi kutoka nje zinazoingia ubia na watu au taasisi za ndani ambao mara nyingi kazi yao kubwa ni kuleta kinga ya kisiasa na kiutawala kutokana na kufahamika na mahusiano yao na mamlaka na watawala.

Miradi ya IPP ina sura tatu za ujenzi, uendeshaji na umiliki. Sura ya kwanza watu au taasisi binafsi zinajenga, kumiliki na kuendesha mradi( Build Own and Operate-BOO) mfano IPTL, SONGAS, na Mtwara; sura ya pili watu au taasisi binafsi zinajenga, zinaendesha na mwishoni zinamilikisha (Build Operate Transfer-BOT); na sura ya tatu ni watu au taasisi binafsi zinajenga, zinamiliki, zinaendesha , na hatimaye zinamilikisha kwa mlaji ( Build Own Operate Transfer-BOOT). 

Njia zote tatu zinaweza kutumika kutokana na mazingira, lakini sura ya BOO inapendelewa zaidi kwa kubebwa na moyo wa kukuza ushurikiano wa umma na watu au taasisi binafsi (PPP)

Mkataba wa IPP unapawa kubainisha na kuungwa mkono na mikataba mingine kila mmoja na lengo maalum kama kuhusiana na ununuzi wa nishati ya umeme( Power purchase agreement -“PPA”); ugavi wa mafuta (Fuel Supply Agreement,“FSA”); uendeshaji wa mitambo (Operation and Maintenance agreement-“O&M”); na ugavi wa mitambo ( Engineering Procurement Contract -“EPC”).

Kipengere cha muhimu sana ni utatuzi wa migogoro kama itatokea ambacho kwa kulinda haki za mwekezaji hasa kama anatoka nje ya nchi kinapaswa kueleza kuwa msuluhishi atoke nje ya nchi husika ambako mitambo ipo.

PESD na wengine wanabainisha kuwa kwa sababu ya hofu na mashaka makubwa yanayohusiana na miradi ya IPP ni vigumu sana kupata mikopo. 

Aidha nchi nyingi zilizoendelea zimekwepa kuifadhili miradi hiyo na kuziachia nchi maskini zijibebe zenyewe huku zenyewe zikibakiza haki ya kutoa lawama na makosa.


Kwa mfano zabuni za Songas zilipotangazwa wazabuni 16 walionyesha nia, wakachukua karatasi za zabuni, lakini ni wawili tu waliorejesha. 


Mradi wa IPTL ulikosa mkopo mpaka pale serikali ya Malaysia ilpotoa dhamana kwa mabenki matatu ya Malaysia (Eberhard, Gratwick, Ghanadan, 2006, Generating power and controversy: Understanding Tanzania’s independent power projects: uk.49).


Kwa upande mwingine marejeo ya PESD na wengine wanabainisha kuwa IPP zimeleta matokeo mchanganyiko. Kuna sehemu yamepokewa vizuri na kwingine kama hapa kwetu yameleta kelele na kutokuaminina. 

Lakini yakiangaliwa kwa upana wake kwa wakekezaji (IPP) yamewapa faida kubwa wakati kwa watumiaji wa umeme yameleta vyazo mbadala na angalau umeme wa uhakika. Cha mhimu katika huduma ni upatikanaji wa huduma kisha vingine kama wangapi wanapata, wamgapi wanamudu gharama, na ubora wa huduma huja baadaye.


Mh. Zitto na mwenzeke Brian Cooskey wamezingeuza sifa hizo za IPP kuwa dhambi na nia ovu na kwa kutaka tuwaamini sana wamenukuu maneno ya Baba wa Taifa akisema: "Kama huu ni mfano wa ushirikiano wa nchi za Kusini, basi ukoloni ulikuwa afadhali." 

Julius Nyerere ( Mh. Zitto,2012, Jinsi Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP) ilivyoichukua Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) bure na kujichotea Dola za Marekani 128 milioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT, UK.2); ‘Kama huu ndiyo ushirikiano wa nchi za kusini, bora ukoloni urudi.’(‘If this is ‘South-South co-operation’, then colonialism is preferable.’) Julius K Nyerere commenting on IPTL (Brian Cooksey,  The Power and the Vainglory: Anatomy of a $100 Million Malaysian IPP in Tanzania: UK.11)

Baada ya kuangalia kwa ujumla hali na tabia za IPP duniani, sasa tuzitumie kwa mfano halisi wa kwetu, tujielekeze kujibu maswali yafuatayo:-
IPTL na mitambo yake ya MW 100 iliyoko Tegeta ni mali ya nani?
Je ni mazingira gani yalisababisha kuja kwa IPTL? 
Je ni IPTL pekee yake ndo yupo?
Kama wako wengi kwanini wengine hawasemwi? 
Je IPTL ilikuwa na mkataba halali na TANESCO? 
Huo mkataba ulisainiwa lini na nani alikuwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini? 
Je IPTL alikuwa anampa Ankara TANESCO na malipo yalikuwaje? 
Kwa nini akaunti ya ESCROW Tegeta ilifunguliwa? 
Ni nani alikuwa anaweka pesa kwenye akaunti ESCROW Tegeta? 
Je kulikuwemo na pesa ya umma? 
Ni nini lilikuwa jukumu la Benki kuu ya Tanzania? 

Maswali matatu ya mwanzo kwa ujumla wake yanapata majibu kutoka kwenye tabia na sura za IPP na sababu za kuanzishwa kwake. IPTL ilianzishwa mwaka 1994 na maktaba wa ununuzuzi wa nishati ya umeme( Power purchase agreement -“PPA”) kati yake na TANESCO ukasainiwa mwezi Mei, 1995 wakati wa utawala wa serikali awamu ya pili. 

Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete, alikuwa Waziri wa Fedha wakati huo. Kwa hiyo wazo kuwa Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete alihuskika kama wanasiasa wanavyojaribu kutuamnisha ni muendelezao mwingine wa kuchafuana.

IPTL siyo IPP pekee yake iliyo saini mkataba wa ununuzi wa nishati ya umeme( Power purchase agreement -“PPA”). Ipo pia SONGAS ambayo kufanikiwa kwake kwa kiasi kikubwa kumetokana na mkopo wa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Dunia ambayo ilikataa kujihusisha moja kw moja na mradi huu kwa visingizio mbalimbali. 

Mkopo kwa SONGAS unakatwa kwenye malipo ya TANESCO ya capacity charges kwenda SONGAS na kuipa nafuu ya muda TANESCO kwenye mzunguko wake wa pesa. Lakini mwisho wake hapo baadaye watanzania tutalipa deni hili; ila dharula itakuwa imeshapita- na huo ndio uzuri wa kukopa.

Marejeo mengi ya Mh, Zitto yanaituhumu IPTL kama sababu ya kuichelewesha Tanzania kuvuna gesi asilia na kuitumia kuzalisha nishati ya umeme. Hoja yake hiyo haina ukweli. Mh.Zitto amerejea ripoti ya utafiti uliyofanywa na Prof.Eberhard na wenzake na ili kutopoteza maana ya walichosema tunukuu maneno yao wenyewe kwa lugha yao:

“the history of the development of Songas and IPTL is notably complex…. it is critical to understand that Songas preceded IPTL in the planning process. With delays in the Songas project and mounting power outages, however, additional proposals, including that of IPTL were considered. Recognized as contributing to South-South collaboration, IPTL emerged as an independently negotiated IPP among Malaysian investors, VIP, a local Tanzanian firm, and the GoT. The plant would be IPTL financed largely by two Malaysian banks, which were given a guarantee by the Malaysian government that their loans would be secure.” (Eberhard, Gratwick, Ghanadan,2006, Generating power and controversy:Understanding Tanzania’s independent power projects: uk.43).

Kutoka kwenye nukuu hiyo hapo juu tunaona kuwa SONGAS ilikuwepo kwanza kabla ya IPTL. Ni kweli kuwa kutangulia kwa IPTL kusaini mkataba  wa PPA na TANESCO na kuzalisha MW 100 kulitangulia mradi wa SONGAS na kuliathiri mradi wa SONGAS. Ambacho siyo kweli ni kuwa mchawi alikuwa IPTL Prof.Eberhard na wenzake wanatupa jibu wanapoandika:-

“The World Bank,…, was instrumental in postponing Songas due to the fact that IPTL made Songas redundant; Tanzania could not absorb the capacity from both plants (at the time).” (Eberhard, Gratwick, Ghanadan,2006, Generating power and controversy:Understanding Tanzania’s independent power projects: uk.43).

Wanaendelea kusema:
“Several points are noteworthy in this context. Firstly, delivery of Songo Songo gas was delayed,which, due to an acute power shortage necessitated  emergency generation, namely running existing Ubungo turbines on imported jet fuel as well as additional usage of IPTL. Secondly, Songas was not at full availability in its first year of operation, which also necessitated additional use of IPTL. Explanations for Songas’ delays and subsequent shortfall in capacity have been attributed to failure of a sub-contractor working on the gas infrastructure to deliver on time, expansion work and technical failure of existing turbines.” (Eberhard, Gratwick, Ghanadan,2006, Generating power and controversy:Understanding Tanzania’s independent power projects: uk.43).

Kwa hiyo kucheleweshwa kwa matumizi ya gesi asilia kulitokana na ushauri wa Benki ya Dunia kulikozingatia sababu za kiuchumi; sababu za kiteknolojia; na kuwepo kwa mbadala aliyetayari hata kama umeme wake ulikuwa ghali.

Hoja nyingine kuhusiana na gesi ni ya kiufundi zaidi. Mitambo ya gesi ni nafuu kuliko ile inayoendeshwa kwa mafuta. Hata hivyo kila uzuri una matatizo yake. Uendeshaji wa mitambo ya gesi unahitaji wataalamu waliobobea katika kuendesha mitambo hiyo. 

Kwa bahati mbaya watalaamu wetu wengi wamebobea katika ufundi wa mitambo ya mafuta kwa hiyo nafuu ambayo tungeipata kwa kutumia mitambo ya gesi ingemezwa na utumiji wa wataalamu na washauri wa mitambo ya gesi asilia kutoka nje ambao mara nyingi ni ghali sana.

Aidha IPTL pia ilikuwa ibadilishwe kutoka kutumia mafuta kwenda kwenye gesi asilia kwa mujibu wa PPA. Suala hili pia liligusiwa vilivyo na tuzo ya shauri la mgogoro kati ya IPTL na TANESCO lililopelekwa mbele ya International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID) ambao walisema:
Maswali Je IPTL ilikuwa na mkataba halali na TANESCO? Na Je IPTL alikuwa anampa ankara TANESCO na malipo yalikuwaje? Majibu ya maswali haya yanapatikana kutoka kwenye marejeo mawili. Rejeo la kwanza ni tuzo ya Baraza la Kimataifa la Usuluhishi la migogoro ya uwekezaji (International Centre for Settlement of Investment Disputes –ICSID). Rejeo la pili ni taarifa ya Ukaguzi Maulimu wa Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyofanywa na Ofisi ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Controler and Auditor General-CAG).

ICSID katika tuzo yake ya Shauri na ARB/98/8  ilyotolewa 12/7/2001 ilitaja wazi kuwa IPTL na TANESCO wanamkataba unaowabana na waopaswa kuhuheshimu na kuutekeleza. Tuzo ilisema:-

Aidha ICSID iliagiza katika tuzo yake kuwa:
Taarifa ya Ukaguzi Maalumu wa Akaunti ya Escrow ya Tegeta  iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( Controler and Auditor General-CAG) inabainisha kuwa IPTL ilikuwa ikitoaa ankara za madai kwa TANESCO kila mwezi. 

Msimamo huu pia uko kwenye tuzo ya ISCID iliyosema:
Maelezo hayo hapo juu yanatupeleka kwenye kiini cha kelele - Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Akaunti hii ni matokeo ya mgogoro kuhusu tozo la uwekezaji/uwezo\utayari wa uzalishaji wa mishati ya umeme (CAPACITY CHARGES). 

Dhana hii unaweza kuiliganisha na waiting charges Madreva Taxi waliokuwa wanawatoza wateja wao kama gharama ya kuwasubiri walikowapeleka. Au inafanana na gharama isiyobadilika wakodishaji wa magari wanayowatoza wateja wao pindi wanapokodi magari yao. Tozo hili hulipwa hata kama gari halitatembea. Ingawaje dhana hii si ngeni, Mh. Zitto na wenzake wanaionyesha kuwa ni kitu cha ajabu, wizi, ghiriba ambayo hajapata kutokea chini ya jua.


Chanzo cha mgogoro kati ya IPTL na TANESCO kulisababishwa na IPTL baada ya kubadilisha aina ya mitambo na kuweka ile ambayo haikutajwa kwenye PPA. PPA ilitaka mitambo iwe  5 ya Slow Speed Diesel (SSD) kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha MW 20 na kufanya jumla ya MW 100. Badala yake IPTL wakaleta mitambo 10 ya Medium Speed Diesel (MSD) kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha MW 10 na kufanya jumla ya MW 100.

PPA kati ya IPTL na TANESCO ilitaka uzalishaji wa MW 100. Aina zote mbili zilikuwa zinaweza kuzalisha MW 100 sasa kelele za nini? Kelele zinatokana na misingi ya Mkataba, teknolojia, gharama.  Mitambo ya SSD ni ghari kuwekeza lakini rahisi kuendesha wakati ile ya MSD ni rahisi kuwekeza na ghari kuiendesha. Kwa kubadilisha mitamno IPTL walikuwa wanakwepa gharama na kumsukumia TANESCO ambaye hakuwa tayari kubeba gharama hizo.

Lakini kwa upande mwingine PPA hiyo haikumlazimisha TANESCO inunue MW 100 wakati wote, TANESCO ingeweza kutaka MW 10 tu kwa wakati Fulani; kwa hiyo IPTL wangewasha mtambo mmoja tu. Hii pia ingepunguza gharama Aidha IPTL hawakuwa wawazi kwa TANESCO kuhusu gharama za jumla  ujenzi wa mradi wa Tegeta.

Kwa vile inaonekana wazi kuwa IPTL ilikiuka mkataba; je TANESCO walipaswa kuuvunja?
TANESCO walifanya hivyo kama ICSID wanavyosema.

TANESCO hawakulizishawa na mwenendo wa IPTL na wakachukua hatua zaidi kama ICSID wanavyotueleza: Je gharama za ujenzi zina umuhimu gani hasa ukizingatia sura ya PPA ya IPTL ilikuwa ni JENGA MILIKI NA ENDESHA (BOO). 

Gharama za Ujenzi ni muhimu kwa vile ndo msingi wa ukokotowaji wa gharama za uwekezaji/uwezo\utayari wa uzalishaji wa nishati ya umeme (Capacity Charges) Mh, Zitto na wenzake wanaushahidi kuwa Gharama za Uwekezaji wa IPTL pale Tegeta ni Dola za Kimarekani Mia moja (USD 100) ambazo kwa mwaka 1995 ni sawa ni shilingi za Kitanznia Elfu Hamsini (tshs 50,000/=). 

Kama wamesahau vile Mh, Zitto na wenzake wanatueleza kuwa IPTL walikopa Dola za Kimarekani milioni mia moja na tano (USD 105,000,000) kwa ajili ya mradi wa Tegeta, wameshindwa kulipa, na mdeni wao anataka kuuchukua huo mradi au fedha zinazopaswa kulipwa kwa wenye IPTL!!!


Katika usuluhishi TANESCO walikwenda na wazo kuwa Gharama za uwekezaji wa IPTL pale Tegeta ni Dola za Kimarekani Mia moja (USD 100) wakati IPTL walikwenda na madai kuwa uwekezaji wao ni Dola za Kimarekani 163,5 milioni. Tuzo ya ICSID iliamua kuwa gharama sahihi ni Dola za Kimarekani 127.2 milioni. Uamuzi huu ulipunguza Capacity charges kwa 25%. 

Ukweli huu unaungwa mkono na mmoja wa Mawakili wa TANESCO na Serikali ya Tanzania pale wanaposema: Tanzania Electric Supply Company Limited (TANESCO) v. Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ICSID ARB/98/8 (filed November 1998, Final Award July 2001) (Arbitrators: Kenneth Rokison (President), Andrew Rogers, Charles Brower). Hunton successfully represented TANESCO in reducing the cost of IPTL’s 100MW power plant located in Dar es Salaam, Tanzania. 


The Final Award reduced the cost of the power plant from a claimed $163.5 million to $127.2 million, resulting in a reduction of the monthly capacity charge for electricity by approximately 25%. (http://www.hunton.com/services/ 4.01.2015).

Kutoka hapo ilitegemewa kuwa mambo yameisha lakini mgogoro mwingine juu ya mwingine iliendelea kuibuka kwa mfano 2008 TANESCO ilienda tena ICSID kuomba ufafanuzi na kuliondoa shauri hilo 2010 (Tanzania Electric Supply Company Limited (TANESCO) v. Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ICSID ARB/98/8 (Interpretation Proceeding) (filed June 2008, discontinued August 2010).

2008 IPTL ilirudi ICSID dhidi ya serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kuomba kukaza hukumu ya tuzo; lakini ililiondoa shauri hilo 2010 (Independent Power Tanzania Limited (IPTL) v. The United Republic of Tanzania, filed July 2008).

Urefu wa migogoro hiyo isiyoisha ilipelekea kuzaliwa kwa wazo la ESCROW akaunti na kufunguliwa kwa  Akaunti ya Escrow ya Tegeta  wenye akaunti wakiwa IPTL na TANESCO na Benki Kuu ya Tanzania (BOT)akiwa wakala wao. 

Kwa mpangilio huo pamoja na kwamba Fedha ziliwekwa benki kuu, pesa hizi hazikuwa sehemu ya mfumo wa serikali. Benki Kuu ya Tanzania wanasema Fedha kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta  ziliwekezwa na Wakala kwenye hati fungani na hii iliipa nchi nafuu ya kiuchumi.


      2.0. Escrow Account
Tarehe 5 Julai, 2006, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia Wizara ya Nishati na Madini (GoT); IPTL na Benki Kuu yaTanzania (BoT) waliingia katika makubaliano ya kufungua Akaunti Maalum (Escrow Account) ambapo GoT ingetekeleza Makubaliano yaUtekelezaji (Impelmentation Agreement) chini ya PPA kwa kuweka fedha katika akaunti maalum.

Fedha hizo zingeendelea kushikiliwa na BoT mpaka pale IPTL na GoT wangekuwa wamemaliza tofauti zao kuhusu viwango vya malipo ya uwekezaji(BOT, 2014, MAELEZO KUHUSU MALIPO YA FEDHA KUTOKA KATIKA AKAUNTI MAALUM (ESCROW ACCOUNT), UK 1-2)

Je kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta  kulikuwa na fedha ya umma pamoja na kodi? Fedha za umma zilikuwemo kutokana kama tu Ankara za IPTL hazikufuata tuzo ya ICSID  ya 12,07.2001 hasa ukizingatia kuwa walianza kuuza umeme 2002. 

Hazikuwemo pesa za umma kwa sababu TANESCO walikuwa hawajalipa Ankara zote walizopelekewa na IPTL.

Kuhusu kodi inashangaza kuona mkanganyiko unatoka wapi. IPTL na TANESCO ni walipa kodi wenye utambulisho wa mlipa kodi (TIN) na usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (KOT-VAT). 

TANESCO wanapowapa wateja wake Ankara zao zinakuwa ni jumla  ya vitu vitano: umeme uliotumika (unit consumed); gharama ya huduma (Service charges); Kodi ya Ongezeko la Thamani (KOT-VAT); umeme vijijini (REA); na EWURA. Wateja wakilipa ikifika mwisho wa mwezi TANESCO wanaandika hundi na kulipa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) jumla ya VAT yote waliyolipa wateja; hivyo hivyo kwa REA na EWURA.

TANESCO wanabakiza umeme uliotumika (unit consumed);na gharama ya huduma (Service charges) ambazo wanapaswa kuzitumia kugharamia uendeshaji wa shughuli zao kama kulipa mishahara ya watumishi na uzalishaji wa umeme. 

TANESCO wapata umeme kwa njia mbili ya kuzalisha wenyewe na kununua kwa IPTL. Hapa ndo matumizi ya mapato kutokana na umeme uliotumika (unit consumed); gharama ya huduma (Service charges) ambazo pesa za umma kwa maana ya kodi zilishatoka- hazimo.

Hata hivyo TANESCO inapolipa Ankara za IPTL zilizowekewa VAT inakuwa inatengeneza mzunguko mwingine wa kodi na pesa za umma ambao wakala wa umma na Kodi ni IPTL na siyo TANESCO. Maana yake ni kuwa IPTL anakusanya VAT kutoka kwa TANESCO na analipa TRA. Malipo haya hayakatwi juu kwa juu na mlaji kama Kodi ya ZUIO. Inashangaza  kuona Mh, Zitto na wenzake hili linawapita?!

Kwa mujibu wa sheria na kanuni za VAT mtoa na muuza huduma akishatoa Ankara ya Kodi (TAX INVOICE) hata kama ni kwa mkopo lazima Ankara na Kodi hiyo ya VAT ionyeshwe kwenye ritani ya mwezi husika na kodi yake ilipwe. 

Nini kilitokea kwa IPTL? TRA walimpa msamaha? Au Ankara za IPTL hazikuwa na VAT? Hili halijasemwa kokote na yeyote, kwanini? Tunaficha nini? Na kwa faida ya nani?

Mh. Zitto na wenzake kama wanapendekeza kuwa Akaunti ya Escrow ya Tegeta
Ndio iliyopaswa kulipa kodi! Lakini Akaunti ya Escrow ya Tegeta  haijasajiliwa kama mlipa kodi! Sasa inawezakanaje?

Jambo lingine cha kushangaza ni kwamba IPTL na TANESCO bado wanafanya biashara; kama kuna kodi kweli kwanini isikatwe kwenye malipo yanayokuja badala ya kuitana majina na kunyoosheana vidole?

Swala lingine ni la kuhusu Benki ya Standard Chartered kudai umiliki wa IPTL na mitambo ya Tegeta kwa misingi kuwa ndiyo inayo miliki deni walilokopa kujenga mradi huo. Wanahisa wa IPTL wanapinga vikali na hasa VIPEM wa Tanzania hawataki kusikia kabisa habari hiyo.

Historia ya deni hilo inaonyesha mdhamini wake alikuwa serikali ya Malaysia na alimdhamini mmoja wa wanahisa wa IPTL Mechmar. IPTL (Mechmer) walishindwa kulipa mkopo huo kwa mujibu wa makubaliano na sababu walizotoa ni kuwa hawakuwa wameanza kuzalisha umeme na kulipwa na TANESCO. ICSID ARB/10/20 wanasema:

“46. Although the plant had been completed in 1998, the commercial operation of the facility
did not start until January 2002, after the ICSID 1 proceeding. ..the plant has been called upon to generate some electricity during each month from January 2002 to April 2007, as well as in June 2007, in March 2008 and from November 2009 to October 2011”.

Mkopo huo ulionekana kuwa hautaweza kulipika na ukawawekwa katika fungu la mikopo isiyoweza kulipika. Wakati wa mtikisiko wa uchumi huko Asia, ukanunliwa  na kuuzwa tena kwa thamani ya Dola za Kimarekani 70 Millioni kwa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong( Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited - SCB HK),

Mechmar wanakubali deni lakini Dola za Kimarekani 40 Millioni tu. Standard Chartered ya Hong Kong (Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited - SCB HK) wakapeleka mgogoro huo ICSID.

Shauri la kwanza mwaka 2010 na uamuzi wake ukatolewa 2012 ambapo  SCB HK ilitaka kwa kuzingatia makubaliano ya uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza, Tanzania iamuliwe kutaifisha mitambo  ya IPTL Tegeta na wapewe wao. 

Tanzania ikiwakilishwa na Hunton & Williams’ International Arbitration and Transnational Litigation ilipinga pendekezo hilo na kushinda (Standard Chartered Bank (SCB) v. The United Republic of Tanzania, ICSID ARB/10/12 (filed May 2010, Final Award rendered 2 November 2012) (http://www.hunton.com/services/ 4.01.2015).


SCB HK walienda tena ICSID  na kufungua shauri- Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited (SCB HK), as Assignee from Independent Power Tanzania Limited (IPTL) v. Tanzania Electric Supply Company (TANESCO), ICSID ARB/10/20 mwezi September 2010 wakitaka ICSID waiamuru TANESCO iwalipe wao badala ya IPTL kwa sababu ya kwamba wanaidai IPTL. 

ISCID ilisistiza maamuzi yake kuwa IPTL ilikuwa ikiwatoza zaidi TANESCO lakini ikalitupilia mbali ombi la kutaka yenyewe ijihusishe na kuamua mambo ya fedha na malipo kwa pande hizo na kuzitaka IPTL na TANESCO zikae na kukokotoa upya Capacity Charges.


“the Tribunal found TANESCO had been overcharged and ordered that the parties confer on recalculating and  reducing the tariff. The Tribunal further held it did not have jurisdiction to enter a money judgment in favor of SCB HK. (http://www.hunton.com/services/ 4.01.2015).

Je nini tofauti ya ICSID ARB/98/8 na hii ICSID ARB/10/20? ICSID ARB/98/8 ilikuwa baina ya pande mbili zilizokuwa na mkataba na ilihusu ukiukwaji wa uletaji wa mitambo kama PPA iliyoelekeza. Pia ulihusu gharama za ujenzi kwa ujumla. Ambazo IPTL ilionyesha kuwa ni kubwa kuliko hali halisi. Tuzo ICSID ARB/98/8 ilirekebisha mapungufu hayo na wahusika wakafuata ushauri wake.

Kiini cha ICSID ARB/10/20 ni umiiliki wa IPTL madai yaliyopelekwa na SCB HK wakidai kuwa wanahisa wa IPTL hawakuwa wamewekeza na kulipia hisa zao bali hisa zao zilitokana na fedha za mkopo. Kama madai hayo yangekuwa kweli yangeathiri tozo la Capacity charges IPTL alilikuwa akiwatoza TANESCO. 

Aidha hatima yake ingekuwa kwamba madai na malipo yote ambayo IPTL alipaswa kulipwa angelipwa mkopeshaji yaani SCB HK kutokana na kununua deni hilo. Marejeo yote yanaonyesha kuwa wanahisa walikuwa wamewekeza na kulipia hisa zao ingawaje si kwa kiasi chote. Hata hivyo uwiano kati ya mwenye hisa mkubwa na mdogo ulibaki kuwa 7/3 (70/30). Uwiano wa hisa na mkopo pia ulionyeshwa katika marejeo yote kuwa 70/30.


Tuzo ya ICSID ARB/10/20 inasema:
“36. IPTL had been formed in 1994 by Mechmar, a Malaysian corporation, and VIP, a
Tanzanian company. VIP held 30% of the shares of IPTL, and Mechmar held the remaining 70%. IPTL’s authorized share capital was of US$10 million and its paid up share capital was equivalent to US$100. 37. 

IPTL raised funds to establish the power plant by means of a credit facility extended to it by a consortium of Malaysian banks  under a US$105 million 1997 Loan Facility Agreement (the “Loan Agreement” or “Facility Agreement”) to be repaid over 8 years. The loan contemplated a debt/equity ratio of 70/30.”

ICSID ARB/10/20 pamoja na kukubali kuwa ndo wamiliki halali wa deni walikopa IPTL (Mechmer) bado hawakuona sababu ya SCB HK kufaidika moja kwa moja na IPTL ila wanaweza kufanya hivyo kwa kupitia IPTL wenyewe.

Kushindikana kwa mlango wa sheria nchini Tanzaia, Malaysia na Mamlaka za kimataifa kama ICSID kuliwafanya SCB HK kutafuta njia ya mkato na wabunge wetu na Bunge letu likaonekana njia ya kufanikisha hayo. Matokeo yake wote tunayafahamu.

Vurugu zote za kupinga na kuunga mkono mradi wa IPTL unaonyesha taswira ya ushindani ulivyo duniani kwa sasa. Katika mazingira ya ushindani ni vigumu kupata ukweli, kila upande unavutia kwake. Mvutano huu unaathiri ukweli na kuendekeza upotoshaji.

Sakata la IPTL linatupa sura nyingine za IPP. IPP ni neema kwa wanasheria lakini jinamizi kwa wawekezaji na watumia huduma (Prof. Eberhard, Managing competition for the market: lesson from the experience of IPPs in Africa, University of Cape Town).  Wanasheria kwa ushauri wao wamevuna pesa halili kabisa kutokana na kazi na taaluma zao na kuwaacha kwenye jinamizi kubwa wadau wengine.

IPP za Tanzania hasa IPTL zimeongeza swala la maadili hasa wanasiasa kama sura nyingine ya IPP. Wako waliochafuka na kwa misingi ya maadili wengine wamejiuzulu, wengine wameachichwa kazi, na wengine taratibu za kisheria zinafuatwa ingawaje watu hawataki kuzipa nafasi.

Lakini misingi ya utawala bora na sheria imetikisika na imetikiswa na baadhi ya wabunge ambao wamefanikiwa kuligeuza bunge kama soko au stendi ya mabasi ambako inatosha kutamka neno mwizi na kumnyooshea mtu kidole na watu wakaanza kumshugulikia. Bunge limegeuzwa na baadhi ya wabunge kuwa a one stop centre yenye kuweza kutaja tuhuma, kuchunguza, kushitaki, kuhukumu na kufunga watuhumiwa bila kujali chochote.

Kwa mfano uko wapi uadilifu wa kumfanya Mh. Zitto kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuchunguza, kushitaki, kuhukumu na kufunga watuhumiwa kutokana na tuhuma zilizotajwa na Mh. Kafulila ambaye ni mtoto wa kisiasa na kila kitu (isipokuwa kumzaa) wa Mh. Zitto; na katika kamati hiyo akiwemo Mh. Deo Filikujombe Makamu Mwenyekiti, Mpambe (Best man) wa harusi ya mtaja tuhuma. 

Na kwa mamlaka ya Mh. Zitto, Mweyekiti, wakaalika wabunge wageni mmoja wapo Mh. Kangi Lugola askari Polisi wa zamani kama Mh, Filikujombe kwa pamoja wakiwa wabunge wawili wa CCM walioungana na UKAWA kususia Bunge Maalum la Katiba. Wakaleta taarifa bungeni iliyosheni mambo mengi ambayo yalishaonekana kwenye mitandao ya kijamii yakiwa yamesambazwa na Mh. Zitto.

Bunge letu liliwezaje kumruhusu Mh, Zitto kushughulikia tatizo ambalo lilishazua kutishiana kati yake moja kwa moja na watuhumiwa. Aidha mtoto wake wa kisiasa Mh. Kafulila alishatishiwa na mmoja wa watuhumiwa na kuambiwa atoke nje ya bunge na mbali na kinga ya bunge waonyeshane kazi. Mh. Zitto na wenzake wanashindwaje kujipima kwa hili dogo na wakadhani ni rahisi kwa wenzao kupisha?

Swali hili linajibiwa na maneno ya Jaji Fedrick Werema mhanga wa sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta alipoeleza sakata hilo kwa kusema sentensi moja kwa Kiingereza- This is mob Justice. Mtu mmoja akatoa ushuhuda wa Mob Justice- Mtu mmoja alikuta kijana mmoja akipigwa na watu wenye hasira kali naye akachukua tofari akamponda. Huku akijifuta vumbi la tofari akamwuliza mmoja wa wale aliowakuta pale eneo la tukio- huyu mshikaji amekosa nini? Aliyeulizwa akajibu kuwa hata yeye hajui amekosa nini! 


NA : BITURO KAZERI
TASAJA - TANZANIAN ASSOCIATION OF SOCIOLOGISTS
Barua pepe tasaja@tasaja.org

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.