Na Clara
Matimo, Mwanza
KAMPENI ya
kupunguza Maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, “Prevention of
Mother to Child Transmission”(PMTCT), na Ushiriki wa Wanaume katika Uzazi wa
Mpango,unakwamishwa na tabia ya mfumo dume ulioota mizizi Kanda ya
Ziwa, imefahamika.
Mratibu
Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto Jijini Mwanza, Sarah Mahumbuga, amesema kwa
miaka miwili ya 2011 na 2012, akina baba wachache walifika Kliniki na katika
vituo vya Afya,ili kupima afya zao na kushiriki Uzazi wa Mpango.
Anasema,Shirika
la Engender Health kupitia Mradi wa CHAMPION(Men Involvement), linalotoa huduma
katika baadhi ya mikoa hapa nchini, Mkoa wa Mwanza ukiwemo, wilaya za Ilemela na Nyamagana zinahusishwa na
mradi huo.
Hospitali ya
Nyamagana na Kliniki ya Makongoro huhusishwa na mradi huo kwa nia ya
kuwahamasisha akina baba kushiriki Afya
ya Uzazi na Maambukizi ya Ukimwi.
Sarah
Mahumbuga amesema, katika kipindi cha mwaka 2011,wanaume walioshiriki kupima
afya zao na Uzazi wa Mpango ni 3,370 sawa na asilimia 18 tu ya lengo lililokusudiwa, katika Jiji la
Mwanza.
Mahumbuga anafanua
kwamba, mwaka 2012 akina baba
walioshiriki katika zoezi hilo muhimu ni 8,541 sawa na asilimia 43.
Akilinganisha
na akina baba waliopima virusi vya Ukimwi mwaka huo 2010 amesema walijitokeza
akina baba 328 tu ambao ni sawa na asilimia 6.
Akaongeza
kuwa mwaka 2011 wanawake waliofika kliniki kwa mara ya kwanza walikuwa 18,726;
na kati yao waliopima Virusi vya Ukimwi ni 7,947 sawa na asilimia 42. Kati yao
waliokutwa wakiwa na maambukizi ya virusi hivyo vya Ukimwi ni 506 idadi ambayo
ni sawa na asilimia 6.3.
Mratibu huyo
Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto Jijini Mwanza, anasema katika mwaka huo 2011
wanaume waliofika Kliniki na wake zao na wakapima afya ni 374 sawa na asilimi
6.9.
Katika mwaka
2012,Mratibu huyo anabainisha kuwa wanawake waliohudhuria kliniki kwa mara ya
mwanzo walikuwa 19,946; na kati yao waliopima afya zao ni 11,299 sawa na
asilimia 57.Waliokutwa na maambukizi ya Ukimwi ni 523 sawa na asilimia 4.6.
Mratibu huyo
amesema wanaume waliohudhuria kliniki mwaka 2012 walikuwa 596 ambao ni asilimia
2.1 tu
Baba akimshuhudia muhudumu wa afya akipima ujauzito wa mkewe katika Kliniki ya Makongoro, Mwanza |
“Kama
wanawake wanaohudhuria kliniki wangekuwa wanafika na wenzi wao na kupima, akina
baba wangetambua umuhimu wa kushiriki zoezi hilo la kuokoa maambukizi kutoka
kwa wazazi kwenda kwa mtoto”, anafafanua.
Akizungumzia
changamoto zinazokabili Kampeni hiyo ya Afya ya Uzazi na Mtoto, katika utendaji wa kazi wa kila siku,
ameseka kuna uhaba wa vitendanishi( HIV TEST KITS) , akatoa mfano kwamba kwa
mwaka huu 2013 Jiji la Mwanza limepata kit 69 tu wakati vipo vituo 24
vinavyotoa huduma hiyo. Kit moja ina
vifaa 100 vya kupima ukimwi.
“Kufuatia
hali hiyo, mwaka 2011 wanawake waliofika kliniki mara ya kwanza walikuwa 18,726,lakini
waliopima walikuwa 7,947; hali hiyo husababisha waliobaki kukosa huduma
kufuatia vifaa hivyo vya kupimia Ukimwi kuwa vichache”, alisisitiza.
Amewataka
wanaume kujitokeza kwa wingi bila woga katika zoezi hilo ambalo lazima
lihusishe baba, mama na mtoto kwa kuwa mtoto hapatikani bila ya wazazi wawili kushiriki tendo la ndoa.
“Wanaume
wote wanapaswa kufika kliniki pindi wake zao wanapopata ujauzito; kwa sababu
kuna faida nyingi; kujua mama ana tatizo gani wakati wa ujauzito,dalili za
hatari; na ikitokea shida baba ajue cha kufanya ili kumsaidia mama mja mzito
kujifungua salama”,
Hatari za
akina baba kutoshiriki zoezi la upimaji wa afya ya uzazi humfanya mama mjamzito kuathiriwa
kisaikolojia,hususan anapopimwa na kubainika kuwa ameambukizwa.
“Wakipimwa
pamoja wakagundua tatizo ina kuwa rahisi wote kwa pamoja kujua namna ya
kumkinga mtoto aliyeko tumboni asipate maambukizi; na pia hujua namna ifaayo
kutumia dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”, Mratibu
huyo amesisitiza.
Imeelezwa pia kwamba,wanaume wengi wa Tanzania
hawapendi kupima Ukimwi ukilinganisha na wageni wanaofika nchini, ambao Mratibu
huyo wa Afya ya Uzazi na Mtoto amesema hawajifichi;lakini wanaume wa hapa
nchini hawapendi kujitokeza kuzungumzia hali zao za kiafya kwa wataalam wa
afya.
Mganga Mkuu
wa Jiji la Mwanza, Dk.Kimaro Daniel anasema kuna wanaume wengi waliojitokeza
kupima afya zao jijini Mwanza ukilinganisha na wanaume wa wilaya za Sengerema na
Ukerewe.
"Wanaume wa jijini hapa wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kushiriki katika suala zima la afya ya uzazi kwasababu elimu tunayowapatia wameielewa na kutambua umuhimu wake, japo elimu hii inapelekwa wilayani lakini kule ushiriki wa kule unakuwa mdogo kutokana na wanaume kujiona wao ni vichwa vya familia hivyo hawawezi kupangiwa na wake zao kwenda nao kliniki" anasema Dk. Daniel.
Akitoa
taarifa kwa Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii,Seif Rashid,Siku ya Utepe Mweupe,Machi 15 mwaka huu,Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo amesema mkoa huu una jumla ya wakazi 2,571,402
kulingana na SENSA YA WATU NA MAKAZI ya 2012,ongezeko ambalo ni sawa na
asilimia 2.7.
Ndikilo
anasema Mkoa wa Mwanza una watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja 106,360 na
wenye umri wa chini ya miaka mitano 488,851; wakati akina mama wenye umri wa
kuzaa ni 926,179.
Akizungumzia
idadi ya hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma ya Afya ya Uzazi na
Mtoto,Dk.Ndikilo amesema kuna vituo 353; na kati ya hivi vipo katika hospitali
14(mbili za rufaa);hospitali za wilaya,za binafsi na za mashirikika ya dini.
Kati ya
vituo hivyo 353,vituo 326 sawa na asilimia 92 hutoa huduma ya afya ya mama na
mtoto;wakati vituo 239 sawa na asilimia 73.3 hutoa huduma ya kuzuia maambukizi
ya Ukimwi toka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mhudumu wa Afya akiwapa huduma mama wajawazito |
Miongoni mwa
akina mama 926,179 wenye umri wa kuzaa, akina mama 121,530 walipata ujauzito na
kati yao 82,214 walipata huduma ya uzazi
wakati wa kujifungua sawa na asilimia 67.6
Mkuu wa Mkoa
anasema kiwango cha maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
kimeshuka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2011 hadi asilimia 4.2 mwaka jana.
Anasema
kwamba vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vimepungua kutoka 217 kati ya 100,000 hadi 95 kati ya 100,000
mwaka jana.
Mkuu wa Mkoa
amesema mkoani Mwanza sasa vifo vya watoto walio chini ya mwaka mmoja ni 11
kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai.Kiwango hiki ni cha asilimia 14.
Kulingana na
Mratibu wa Taifa wa Afya na Mama na Mtoto katika Wizara ya Afya, Dk. Koheleth
Winani,akina mama wa Tanzania wangali wanakabiliwa na hatari ya maradhi
yanayoweza kuzuilika.
Kiwango cha
akina mama wajawazito wanaofariki nchini
454 kati ya 100,000.Na watoto wanaokufa ni 26 kwa kila watoto 1000 wakati wanapozaliwa.
Kufuatia
halihiyo, Mkurugenzi wa Afya wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la
Marekani(USAID),Alisa Cameron alisema siku ya uzinduzi wa Kampeni ya Uzazi
salama Jijini Mwanza kwamba Kampeni ya ‘Wazazi Nipendeni’ inayotangazwa na
vyombo vya habari nchini iwafanye akina baba kuacha mfumo dume na kushiriki
ipasavyo katika zoezi la uzazi wa Mpango na kupima virusi vya Ukimwi,ili kuokoa
maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto.
“WAZAZI
NIPENDENI” inalenga kuwezesha akina mama wajawazito na wenzi wao kuchukua hatua
thabiti za uzazi salama, na kuzua maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto(PMTCT).
Sekamponge Makuki (24)mkazi wa jijini Mwanza ambaye
ni mjamzito, anasema yeye anafaraja sana kwa kipindi hiki cha ujauzito
kwa kuwa yeye na mumewe walipanga kupata mtoto,na pia wote wanahudhuria klinik
jambo linalowafanya kupata elimu ya pamoja kutoka kwa wataalamu wa afya,na pia
mumewe anafundishwa jinsi ya kuishi nae kwa kipindi cha ujauzito.
“Tangu
tulipofunga ndoa na mume wangu,tumekuwa tukishirikiana nae katika masuala yote
ya afya ya uzazi,hivyo na huu ujauzito nilionao tulipanga kwamba tazae,hata
kabla ya kupata ujauzito tulipima afya zetu na baada ya ujauzito tulipima pia
kwa pamoja, namshukuru MUNGU hatukupatikana na maambukizi ya ukimwi anasema na kuongeza kuwa “lakini kwa
kuwa tunashirikiana hata kama majibu yangekuwa mabaya tungeyapokea kwa
pamoja,ni vizuri akisikia mwenywe majibu
kutoka kwa mtaalamu wa afya kuliko kumwambia mimi’’”anaeleza Makuki.
Mhudumu wa Afya akiwahudumia watoto katika Kliniki ya Makongoro |
Mwanaume
anayeshiriki katiaka suala zima la Uzazi wa Mpango katika kliniki ya makongoro
iliyopo jijini Mwanza,Abel Luzibila (30)mkazi wa Bwiru jijini Mwanza anasema
amekuwa akienda kliniki na mke wake tangu mwanzo wa ujauzito ili kufahamu
maendeleo ya afya ya mke wake, kama wataalamu wa afya watabaini tatizo lolote
kutoka kwa mke wake wajue watajipanga vipi kiuchumi katika kulitatua.
Luzibila,
amesema kwamba mara ya kwanza alipofika Kliniki na mkewe ambaye ni mjamzito,
alisema alivutiwa na somo la namna
inavyopasa kumsaidia mama mjamzito.
“Kwa mfano,leo(Aprili
25 mwaka,2013) tumejifunza somo la unyonyeshaji, tumefundishwa lishe bora wakati
mama anaponyonyesha na sitabishia Bajeti inayotukabili kwa sababu tayari
nimeshiriki mafunzo hayo na najua umuhimu
na athari za kukosa lishe bora”, Luzibila anasema.
Ofisa Mawasiliano
wa Mradi wa CHAMPION unaoshughulikia
Ushiriki chanya wa Wanaume katika Mkakati wa kitaifa wa kupambana na Maambukizi
ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi (Engender
Health),Muganyizi Mutta, anasema akina baba wanaposhiriki kikamilifu katika
Uzazi wa Mpango watawezeshwa kupanga idadi ya watoto wanaowataka.
Mutta pia amesema
baba na mama wakishiriki kwa pamoja katika zoezi hilo watapata njia za uzazi wa
Mpango zinazofaa, na kuwa na familia zilizo bora.
“Shirika la
Engender Health,kupitia Mradi wa CHAMPION(Men Involvement) limetenga Dola za
Kimarekani milioni 16 kwa ajili ya kuhamasisha akina baba kushiriki kikamilifu
katika mkakati huu kitaifa wa kupambana na virusi vya Ukimwi kutoka ,mradi ni
wa miaka mitano unaomalizika Septemba
mwaka huu”, Mutta amesema
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.