ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, December 8, 2019

KWA MARA YA KWANZA WAZEE WA MILA WAKUTANA NA KUUNGANA KWENYE VITA DHIDI YA VITENDO VYA UKATILI



 Wazee wa mila kutoka mikoa tisa nchini yenye kiwango kikubwa cha ukatili wa kijinsia wamekubaliana kutumia ushawishi walio nao ili kwenye mapambano dhidi ya vitendo hivyo ikiwemo ukeketaji, kutakasa wanawake, mimba na ndoa za utotoni.

Wazee hao wamefikia maazimio hayo Disemba 05, 2019 jijini Mwanza kwenye mkutano ulioshirikisha viongozi wa mila zaidi ya 200 kutoka makabila mbalimbali ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita, Kagera, Simiyu, Tabora, Katavi na Manyara ulioandaliwa na shirika la UN Women.

Hata hivyo mmoja wa wazee hao, Chifu Mfungo Charles kutoka mkoani Geita amesema changamoto waliyonayo ni kukosa nguvu kisheria na hivyo kuomba Serikali kuwarejeshea mamlaka waliyokuwa nayo hatua itawaongezea nguvu ya kupambana na yeyote atayekumbatia mila zinazochochea ukatili wa kijinsia.

Kwa upande Mkuu wa kitengo cha kupambana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike kutoka shirika la UN Women, Lucy Tesha amesema wazee wa mila ni wadau muhimu katika kutokomeza mila na desturi zinazorudisha nyuma maendeleo ya wanawake hivyo kuwashirikisha kwenye mapambano hayo kutasaidia kuleta mabadiliko katika jamii zao ikiwemo kuwashirikisha wanawake katika shughuli za kiuchumi.

Itakumbukwa mikoa yenye kiwango kikubwa cha ukatili nchini ni Mara asilimia 78, Shinyanga asilimia 78, Tabora asilimia 71, Kagera asilimia 67, Geita asilimia 63, Simiyu asilimia 62, Kigoma asilimia 61, Mwanza asilimia 60, Njombe asilimia 53, Dodoma asilimia 50 na Katavi asilimia 50.




  Wazee wa mila kutoka mikoa tisa nchini yenye kiwango kikubwa cha ukatili wa kijinsia wakifuatilia mkutano huo.
 Wazee wa Mila kutoka mikoa tisa nchini yenye kiwango kikubwa cha vitendo vya ukatili wa kijinsia wakiwa kwenye mkutano wa kujengeana uwezo na kuweka mikakati ya kutokomeza vitendo hivyo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.