ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, February 2, 2018

VIDEO:- MASUALA MUHIMU YALIYOSISITIZWA NA KAMATI YA MAUDHUI YA TCRA KWA WANAHABARI KANDA YA ZIWA



MAUDHUI YANAYOLENGA MAENDELEO
Mada Iliyowasilishwa na Bwana Joseph M. Mapunda, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Katika Warsha ya Wahariri na Watengenezaji wa Vipindi vya Redio na Televisheni, Mwanza ,Februari01, 2018.

Utangulizi
Nchi yetu imejaliwa  kuwa na rasilimali nyingi za kuiwezesha kupata maendeleo  makubwa katika nyanja zote za uchumi, huduma  za jamii, utamaduni, habari na michezo bila kusahau suala zima la demokrasia (siasa). Kuna fursa nyingi za kuliwezesha Taifa kupata maendeleo ya haraka ikiwa rasilimali zilizopo zitatumika kikamilifu  na kwa umakini mkubwa.

Kwa upande wa sekta ya habari na utangazaji, sera na sheria zilizopo zimetoa  nafasi na uhuru mkubwa kwa sekta ya umma(Serikali) na sekta binafsi kumiliki na kuendesha vyombo vya habari na utangazaji kwa lengo kuu la kuvifanya viwe  chachu ya kuhamasisha  wananchi na wadau wengine ndani na nje ya nchi yetu kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mipango ya maendeleo kwa faida ya vyombo vyenyewe, wananchi na Taifa kwa ujumla.


Ukuaji wa Sekta ya Habari na Utangazaji
Vyombo vingi vya habari na utangazaji vimeanzishwa hapa nchini tangu miaka ya 1990 wakati mfumo wa uchumi ulipoanza kushirikisha rasmi Sekta binafsi tofauti na huko nyuma ambapo shughuli zote kuu za uchumi na kijamii  zilikuwa zikimilikiwa na kuendeshwa na Serikali.

Utaratibu huo pia ulihusisha masuala ya kisiasa ambapo nchi ilikuwa ikitawaliwa  katika misingi ya demokrasia ya Chama kimoja cha siasa (one Party democracy).

Idadi ya Vyombo vya Habari na Utangazaji
Hadi sasa kuna vituo 32 vya televisheni; vituo 155 vya redio na idadi kubwa ya mitandao ya kijamii. Hali kadhalika kuna magazeti na majarida 432 yaliyosajiliwa kisheria. Vyombo vingi zaidi vya habari na utangazaji vinaendelea kusajiliwa na hivyo kutoa fursa nyingi za uwekezaji na ajira katika Sekta hii muhimu ambayo baadhi ya watu wamezoea kuiita Mhimili wa Nne (Fourth Estate). Zaidi ya asilimia tisini na tisa (99 per cent) ya vyombo vilivyopo  vinamilikiwa na Sekta binafsi.

Utajiri huu mkubwa wa idadi ya vyombo vya habari na utangazaji ni ushahidi tosha kuwa sekta hii ni nyenzo  muhimu na ya kutegemewa katika kuwapa habari,  kuwaelimisha  na pia kuwahamashisha wananchi kushiriki kikamilifu na kwa uelewa mkubwa katika kuibua na kutekeleza mipango ya maendeleo ya nchi yetu.

Kwa vile zaidi ya asilimia sabini na tano (75 per cent) ya Watanzania wanaishi vijijini wakishughulika na kilimo---ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa--- ni wazi kuwa vyombo vya habari na utangazaji vina wajibu mkubwa wa kuelekeza nguvu na rasilimali zake huko ili kutangaza mafanikio, matarajio na changamoto za kilimo, ufugaji, afya, maji, elimu, utamaduni na michezo pamoja na mambo mengine mengi ya msingi.

Hali Ipoje?
Pamoja na idadi hiyo kubwa ya vyombo vya habari na utangazaji, sehemu kubwa ya makala na habari zinazorushwa na vyombo hivi zinahusu matukio na shughuli za mijini ambako kuna wananchi wachache. Hali hii inamaanisha  kuwa juhudi na matukio ya watu wengi waishio vijijini na wilayani hupewa nafasi kidogo sana katika matangazo ya vyombo vyetu.

Natoa rai kwa wamiliki na watendaji wakuu wa vyombo vyote vya habari na utangazaji kuonyesha uzalendo usioyumba (unshakable patriotism) ili kuhakikisha kuna kuwa na uwiano mzuri/sawia wa habari na matukio ya mijini na zile za vijijini ili kutoa fursa na hamasa kubwa kwa wananchi wote kujuzwa juu ya mambo muhimu yanayoendelea nchini na hivyo kuwawezesha kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mipango mbali mbali ya maendeleo.

Kuelekea Uchumi wa Kati
Serikali imedhamiria  kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati ( middle income economy) ifikapo mwaka 2020. Mkazo hapa umewekwa katika kujenga na kuimarisha Sekta ya Viwanda kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa bidhaa  za viwandani hasa zile zinazotokana na malighafi za kilimo na ufugaji na shughuli nyingine  nyingi za kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa. Mkakati huu pia unahusu ufufuaji wa viwanda vilivyokufa na vile ambavyo ujenzi wake haujakamilika. Mafanikio ya juhudi hizi yatawezesha kupatikana ajira nyingi, ongezeko la uzalishaji mali,  mapato ya Serikali na maslahi ya wananchi kwa ujumla.

Vyombo vya habari na utangazaji vina nafasi kubwa ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuielewa dhana  nzima ya uchumi wa viwanda na jinsi wanavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa azma hii ya Serikali kwa vitendo.

Twende Vipi?
Uchumi wa viwanda ni dhana pana sana. Inahusisha sekta zote za uchumi na jamii (production and service sectors). Sekta zote hizi zinaingiliana na kushabihiana katika mfumo wake wa utendaji. Naomba tuangalie kwa muhtasari baadhi ya sekta na jinsi gani vyombo vya habari  na utangazaji vinaweza kuchukua nafasi yake katika kurusha matangazo yenye kuendana na dhana ya viwanda nchini.

Kilimo
Hii ni  sekta kiongozi katika uchumi wa Taifa letu na itaendelea kushika nafasi hiyo kwa miaka mingi ijayo. Kwa kuzingatia hilo, ni vema wakulima na wafugaji wakaelimishwa mbinu za kilimo cha kisasa ili kuzalisha mazao bora yenye kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi na ziada kwa ajili ya soko la nje.

Matangazo yazingatie kuwaelimisha wananchi juu ya misingi bora ya kilimo na ufugaji hasaupatikanaji kwa wakati wa pembejeo na zana nyingine muhimu za uzalishaji na pia jinsi ya kuyafikia masoko kirahisi ili bidhaa zitakazo zalishwa zisiozee mashambani.
Elimu zaidi pia itolewe na kutiliwa mkazo kuhusu uanzanzishwaji wa viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo katika ngazi ya vijiji ili kuyaongezea thamani. Mkakati huu utawahakikishia wananchi ajira nyingi, mapato makubwa, afya bora na huduma muhimu za kijamii.

Kupitia viwanda, wananchi wataweza kula vyakula safi na salama vilivyosindikwa hapa nchini. Hali hii itatuondolea  tatizo sugu la kula vyakula vibovu na hatarishi  kutoka nje ya nchi. Wengi wetu hapa tumewahi kusikia uvumi kupitia mitandao ya kijamii na kwingineko kuwa soko letu limevamiwa na mchele wa plastiki, samaki wa plastiki, mayai bandia ya kuku, maziwa, nyama, na bidhaa nyingine  zisizokuwa na viwango vinavyokubalika kiafya.

Hali kadhalika, Watanzania wengi huvaa nguo na viatu vya mitumba wakati tuna pamba na ngozi nyingi zinazoweza kuzalisha bidhaa bora. Suala la viwanda vidogo vidogo vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe katika ngazi ya vijiji na wilaya litiliwe mkazo.
Wananchi waelezwe na kuelemishwa ipasavyo kuhusu masuala haya muhimu na jinsi ya kuyakabili ili kutuwezesha kujitegemea, kulinda afya zetu na kujijengea miili imara na akili timamu.

 Elimu ni Kila Kitu
Wote tunafahamu umuhimu wa elimu katika uchumi na ustawi wa jamii. Shule na vyuo vyetu katika ngazi zote vihamasishwe  na viwezeshwe kutoa wahitimu au wataalam wa fani mbali mbali watakaoweza  kulisaidia Taifa kwa vitendo kuleta maendeleo na mapinduzi katika maisha yao.

Vyombo wa habari na utangazaji vijikite katika kurusha matangazo yanayolenga  maendeleo na kuhakikisha watu wote, hasa maskini, wanaondokana na hofu ya njaa na shida nyingine nyingi za daima ili kufikia kiwango cha maisha yanayomstahili  binadamu.

Kwa mfano, akina mama huko vijijini na baadhi ya miji yetu wakipunguziwa mzigo wa kujitwika mitungi na ndoo za maji kilometa nyingi wanaweza kupata fursa  za kujihusisha kikamilifu katika uzalishaji mali kwa upeo na ufanisi mkubwa. Tutilie mkazo dhana ya watu kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Kupitia tafiti mbali mbali vyombo vya utangazaji vinaweza kuandaa  makala na vipindi maalum vitakavyoonyesha au kuelekeza  mambo yanayowezekana kufanywa  na jinsi yanavyoweza kufanyika. Ni dhahiri kuwa watu wenye elimu na ujuzi wanaweza tu kuwa na manufaa kama watachanganyika na kushirikiana kwa dhati na jamii inayowazunguka. Haya yote yanaweza kutendeka  ikiwa moyo wa uzalendo utajengeka na kuimarishwa ndani ya vyombo vya habari na utangazaji.

Afya na Ustawi wa Jamii
Hii ni dondoo  yenye uzito mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Tunahitaji kuwa na watu wenye siha nzuri na ya kutegemewa  katika shughuli nzito na muhimu za maendeleo. Ili tuweze kupata  maendeleo ya kweli na ya haraka inabidi  suala la afya litiliwe mkazo maalum  na vyombo vya habari na utangazaji. Jukumu la msingi hapa ni kuandaa na kurusha vipindi na makala zenye kuelimisha watu kuhusu namna ya kuzuia na kujikinga na maradhi, kutunza mazingira, kula vyakula vyenye kujenga mwili, kunywa maji safi na salamana kuondokana na unywaji wa pombe zilizotengenezwa bila kuzingatia masharti na viwango vinavyokubalika kiafya.

Uzoefu unaonyesha kuwa makala na taarifa nyingi zinazorushwa  zinahusu matukio ya magonjwa ya mlipuko na majanga mengine ya kiafya na ya kijamii. Tuandike na tutangaze habari zinazowahamisisha na kuwashawishi watu  kuishi vizuri kwa kuzingatia masharti na matakwa ya afya bora.

Watu wengi wamezoea au wanalazimika kula vyakula vya mitaani katika mazingira machafu.  Juhudi za dhati zifanyike kuwahimiza mamalise na babalishe kupika vyakula bora na ambavyo vimeandiliwa kwenye mazingira bora na kupakuliwa kwenye vyombo  vinavyokubalika kiafya.

 Siku hizi Watanzania wenzetu wengi wanasumbuliwa na magonjwa yasiyotibika kama saratani, ambayo kwa kiwango kikubwa chanzo chake ni kula vyakula visivyokuwa na viwango sahihi. Shughuli za taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Vyakula na Madawa Tanzania (TFDA) zipewe kipaumbele katika matangazo ili mchango wao uweze kuwa wa manufaa zaidi kwa wananchi na ustawi wa jamii.

Vile vile, elimu ya kina itolewe kuhusu faida zinazotokana na kula vyakula vya asili (fresh foods) kama vile mboga zilizolimwa  katika mazingira safi na salama, matunda, nafaka za mafuta kama karanga, ufuta, alizeti, nazi na vingine vingi. Kwa bahati nzuri bidhaa hizi zote zinazalishwa kwa uwingi hapa nchini kwa bei ambazo watu wengi wanaweza kuzimudu. Tujihadhari na bidhaa zilizosindikwa  kutumia madawa/chemikali ili kuepuka athari za kiafya.

Utamaduni, Muziki na Burudani
Sekta  hii pia ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu. Vituo vya utangazaji viandae na kurusha vipindi vinavyohamasisha  ukuaji na uendelezaji wa muziki na burudani zenye  maudhui ya yanayoendana nautamaduni wetu wa Kitanzania. Pamoja na kuwepo umuhimu wa kurusha muziki na ngoma kutoka nje ya nchi ni vema busara ikatumika kuchagua maudhui yenye kulenga uendelezaji na udumishaji wa mila na desturi za  Kitanzania.

Ngoja niwashirikishe kitu kimoja hapa. Siku chache zilizopita nilipigiwa simu na mtu mmoja ambaye alinidokeza kuwa alikiona  kipindi cha muziki katika kituo kimoja cha televisheni cha Dar es Salaam ambacho kilirusha wimbo wenye maudhui ya kulidhalilisha Taifa letu. Sehemu ya wimbo husika una maudhui yanayosomeka “…..Bongo kubaya twende zetu Ulaya; Bongo maisha mabaya, Ulaya kuna raha tele…..”.Je, kwa maudhui kama haya tunaitendea haki nchi yetu?

Tuijengee heshima nchi yetu kwa kurusha vipindi vyenye maudhui ya kizalendo na yale yanayohamasisha sifa nzuri na umoja na mshikamano wa Taifa letu.

Amani na Utlivu
Nchi yetu imejizolea sifa nyingi sana duniani kama mahali penye amani, usalama na utulivu. Sifa hii imetujengea heshima namazingira mazuri kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Sekta yetu ya utalii na sekta za uwekezaji zimevutia wageni wengi kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza katika uchumi wetu kutokana na sifa nzuri za Watanzania. Kwa kuzingatia ukweli huo, vyombo vyetu vinapaswa kuendelea kutangaza kwa nguvu zote taswira ya Tanzania yenye amani, utulivu na usalama.

Jukumu hili lichukuliwe kwa uzito mkubwa hasa tukizingatia  kuwa tabia ya wageni kwa maana ya watalii na wawekezaji ni kwenda mahali ambapo usalama  wao na wa mali zao unalindwa kama mboni za jicho lako!

 Kutangaza kwa ushabiki vitendo vya uhalifu na matamshi ya kisiasa yanayoashiria uvunjifu wa amani yana athari kubwa sana katika juhudi zetu za maendeleo. Tuwahakikishie wageni wetu kuwa Tanzania ni nchi tulivu, inazingatia utawala wa kisheria na pia inaendesha mambo yake kwa uwazi na inazingatia kwa dhati suala zima la haki za binadamu. Dondoo yetu kubwa iwe kutangaza habari zenye maslahi kwa Taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

HITIMISHO
Tanzania ni nchi yetu nzuri sana. Ina watu wapole na wakarimu. Majirani zetu na watu wengine duniani  wanaimezea mate. Tuna haki na wajibu kuilinda, kuiheshimu na kuienzi kwa uzalendo wa hali ya juu ili tuweze kuijengea mazingiria imara ya maendeleo katika nyanja zote.

Dhamana tuliyopewa ya kulitumikia Taifa hili kupitia vyombo vya habari na utangazaji tuiheshimu na tuitumie vizuri kwa maslahi ya Taifa na ya wananchi wote. Nawatakia mafanikio katika kazi zenu. Mungu awalinde na awaongoze daima.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.